26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Utafiti mpya wapinga nyama, maziwa kusababisha maradhi ya moyo

Vyakula vinavyotokana na nyama
Vyakula vinavyotokana na nyama

* Watupia lawama viazi mviringo, nafaka

LINAPOKUJA suala la maradhi ya moyo, wengi wetu watakuwa wamesikia visababishi vyake, na hivyo kujitahidi kuviepuka ili kukaa mbali na uwezekano wa kuyapata.

Miongoni mwa visababishi vya maradhi hayo ni pamoja na staili mbovu ya ulaji wa aina fulani ya vyakula, ambavyo ingawa hatukatazwi kuvila bali kuviingiza tumboni kwa wingi.

Vyakula hivyo ni pamoja na nyama na bidhaa zinazotokana na maziwa zenye wingi wa mafuta.

Hata hivyo, utafiti mpya uliochunguza tabia za mlo na maradhi ya moyo katika mataifa 42 ya Ulaya kwa kipindi cha miaka 16, unapingana na dhana hiyo tuijuayo kwa miaka mingi sasa.

Kwa maana hiyo unapingana na miongozo ya afya iliyowekwa na serikali za mataifa mengi linapokuja suala la kukabiliana na maradhi ya moyo.

Utafiti huo pamoja na mambo mengine umeonya ulaji wa viazi mviringo au vyakula vinavyotokana na viazi kama vile chipsi kwa wingi huongeza hatari ya kusababisha maradhi ya moyo.

Ulisema pia mazao ya nafaka yanaongeza hatari hiyo, huku ukionesha mazao kutokana na maziwa husaidia kupunguza hatari ya kupata maradhi hayo.

Lakini pia unapinga dhana kuwa ulaji wa nyama kwa wingi husababisha maradhi hayo.

Dk. Pavel Grasgruber, mwandishi kiongozi wa ripoti ya utafiti huo kutoka Chuo Kikuu cha Masaryk nchini Jamhuri ya Czech, alitoa mwito wa ushauri na mwongozo mpya kutolewa kuendana na utafiti huo.

“Hatari ya kupata maradhi ya moyo tuijuayo sasa imetokana na takwimu zisizo sahihi. Utafiti huu mpya ulikuwa wa kina na una hekima ya matumizi ya mlo sahihi.”

“Ni wazi kabisa matumizi ya mazao ya maziwa na nyama hayahusiani na hatari ya maradhi ya moyo, kama inavyoaminika kwa wengi.

“Tatizo kubwa ni wingi wa matumizi ya vyakula vya nafaka, mtama na viazi.

“Nina wajibu wa kutoa mapendekezo kwa watu kubadili milo yao na kupunguza ukubwa wa wanga wao mwilini.”

Utafiti huo ambao ulilinganisha takwimu kutoka nchi tofauti, ulionesha mahali ambako kuna matumizi makubwa ya vyakula vya wanga, kulikuwa na kiwango kikubwa cha maradhi ya moyo.

Pia ulionesha kuwa nchi zenye kiwango cha chini cha maradhi ya moyo zilikuwa na kiwango kikubwa cha matumizi ya mlo wenye utajiri wa mafuta na protini.

Takwimu zilizochapishwa katika Jarida la Utafiti wa Vyakula  na Virutubisho zimeonesha mazao kutokana na maziwa yenye kiwango kikubwa cha mafuta hasa jibini vilifanya kazi ya kupunguza marathi ya moyo.

Matunda jamii ya machungwa, mvinyo, jamii ya karanga, olive na mbogamboga, zote pia zimeonekana kuwa na uwezo wa kulinda moyo.

Utafiti ulionesha kwamba mwenendo wenye kuhatarisha zaidi maradhi ya moyo ni mlo wenye wanga, viazi mviringo na nafaka.

Dk. Grasgruber alisema kuwa utafiti unapingana na utamaduni na ufahamu wetu wa miaka mingi kuhusu vyakula vyenye mafuta yenye kusababisha madhara mwilini (saturated fat).

Kama utakumbuka mafuta haya ambayo kwa kawaida huganda katika mazingira ya kawaida ya joto la ndani hutokana na wanyama.

Ni tofauti na yale ‘unsaturated fat’, ambayo hupunguza lehemu mwilini na hivyo kupunguza uwezekano wa kupatwa na maradhi ya moyo, kiharusi, uzito mkubwa, kisukari na shinikizo la damu.

Unsaturated fat hupatikana zaidi kutokana na mazao ya mimea.

Mwongozo kuhus mlo salama wa Uingereza ulioanzishwa mwaka 1983, kwa mfano unashauri ulaji zaidi wa vyakula vya wanga ikiwamo viazi mviringo na nafaka.

Na unatoa ushauri watu ulaji kidogo wa vyakula vyenye mafuta hasa saturated fat.

Utafiti mwingine uliochapishwa Mei mwaka huu pia unatambua viazi kama chanzo cha hypertension, yaani shinikizo la juu la damu.

Utafiti huo ulibainisha kwamba ulaji wa viazi mara nne kwa wiki unaweza kuwa hatarishi na kuchangia hali inayosababisha kiharusi na maradhi ya moyo, ambayo ni wauaji wakubwa nchini Uingereza.

Utafiti huo unaendana na mwingine uliowahi kutoa matokeo ya kustaajabisha  ukionesha mataifa ambayo hutumia mvinyo na nyama kwa wingi watu wake huishi maisha marefu zaidi kulinganisha na yale yanayotumia zaidi wanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles