26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Utafiti: Acheni nyama kuepuka vifo vya mapema

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

WAKATI kwa baadhi ikionekana ulaji wa nyama ya nguruwe ‘kitimoto’, ng’ombe na mbuzi kuwa ni ishara ya kipato kizuri, hata hivyo vitoweo hivyo vimetajwa kuwa miongoni mwa vyanzo vya vifo vya mapema, ikichangia kwa asilimia 23.

Utafiti huo mpya unakubaliana na ule uliowahi kufanywa na Taasisi ya Kansa nchini Marekani, ambao ulihoji watu 536,000 wenye umri wa miaka 50 hadi 71 waliojitaja kuwa ni walaji wa nyama nyekundu.

Majibu ya utafiti huo yalionesha kuwa asilimia 26 ya wale waliokuwa wakitumia nyama kwa kiasi kikubwa walikuwa wakisumbuliwa na magonjwa tisa sugu, ikiwamo saratani inayosababishwa na madini ya chuma aina ya Heme yanayopatikana katika nyama nyekundu.

Utafiti wa sasa uliofanywa hivi karibuni na Chuo Kikuu cha Eastern Finland na kuchapishwa na jarida la American Journal of Clinical Nutrition, nao umezidi kukazia mwelekeo ule ule.

Majibu yake yalitokana na watu 2,600 waliohojiwa juu ya mpangilio wao wa kula, wote wakiwa ni watumiaji wakubwa wa nyama nyekundu (ng’ombe, mbuzi n.k.) hapo ndipo watafiti walipobaini kwamba waliokuwa na kawaida ya kula gramu 200 za nyama kwa siku walikuwa hatarini zaidi, ukilinganisha na wenzao wa chini ya gramu 100.

Ikifafanua, ripoti ya utafiti huo ilieleza kwamba nyama nyekundu ni hatari kutokana na wingi wake wa mafuta, hivyo kuwa rafiki wa magonjwa hatari kama kisukari, moyo na saratani ya tumbo.

Hayo yanazidi kubainika licha ya kuwapo kwa tafiti nyingine nyingi za kutosha kutoka kwa wataalamu wa masuala ya lishe, waliowahi kufichua kuwa nyama nyekundu ni chanzo kizuri cha protini, vitamini na madini.

Kuliweka sawa hilo, Profesa wa masuala ya lishe kutoka Chuo Kikuu cha Eastern Finland, Jyrki Virtanen, anasema: “Ujumbe hapa ni kwamba kula protini nyingi, hasa nyama inapokuwa na chanzo kikubwa, si salama kwa afya.”

Katika kile kinachoakisi majibu ya utafiti huo, Shirika la Afya la Uingereza, linashauri ni vema kwa kila binadamu kula si zaidi ya gramu 70 ya nyama nyekundu kwa siku.

Wakati huo huo, timu ya Chuo Kikuu cha Eastern Finland haikuacha kutaja uvutaji sigara na ulevi kuwa sehemu ya vyanzo vya vifo vya mapema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles