26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Usiwe mwepesi kutoa ushauri kwa mtu

UMEWAHI kuombwa ushauri na mtu? Ulijisikiaje? Ilikuchukua muda gani kutoa ushauri ulioombwa? Tunaombwa ushauri na rafiki, ndugu, jamaa au mtu mwingine yeyote aliyefikiri tunaweza kumsaidia kupata ufumbuzi wa changamoto inayomkabili.

Tunaombwa ushauri na watu wanaotafuta ufumbuzi kwenye mahusiano yake ya ndoa, mapenzi, urafiki, utendaji wa kazi, imani na masuala mengine ya kimaisha. Ingawa hatuwezi kukiri moja kwa moja, wengi wetu tunafurahi kuombwa ushauri.

Unapoona watu wanakufuata kwa ushauri mara nyingi ni dalili kuwa watu wanaona kitu cha ziada ambacho pengine si wengi wanacho. Unapoombwa ushauri unajisikia kuwa mtu muhimu katika jamii.

Mtu mwenye uzoefu zaidi, maarifa zaidi, ujuzi zaidi na hata uelewa zaidi ya watu wengine ndiye anayeombwa ushauri. Kwa sababu hiyo tunakuwa wepesi kushauri.

Lakini hebu jiulize, unajisikiaje ukimpa mtu ushauri na akaupuuza? Chukulia mtu amekuja kwako akaomba umshauri namna ya kutatua changamoto fulani katika maisha.

Umempa ushauri ukiamini kuwa akiutumia tatizo lake litapata ufumbuzi. Kwa mshangao unakuja kugundua baadaye kuwa hakutumia ushauri wako. Ungejisikiaje?

Nakumbuka miaka ya nyuma nikiwa mwaka wa mwisho shuleni niliwahi kumshauri kijana mmoja kuachana na mchumba wake. Urafiki na ukaribu wetu ulinisukuma kumtahadharisha kuhusu tabia ya msichana aliyekuwa anapanga kumwoa baada ya masomo yetu.

Nilimfahamu msichana huyo na sikufikiri angefaa kuwa mke wa rafiki yangu wa karibu. Kwa hiyo bila kufikiri sana na bila kujua nini kilikuwa kinanisukuma kutoa ushauri ule, nilimwendea rafiki yangu na kumweleza ninayoyajua kuhusu mchumba wake kwa matumaini kuwa angefanya maamuzi ya kuachana naye. Ushauri wangu haukupokelewa vizuri. 

Kuona hajachukua hatua za kutosha, ilibidi nitafute muda mwingine niweze kumpa ufafanuzi wa kina na kisha kumshauri moja kwa moja kwamba mchumba yule hakuwa anamfaa.

Pengine kwa kulinda urafiki wetu, yule bwana alinishukuru kwa kumwambia ukweli ambao hakuwa anaujua na hatimaye baadaye aliniarifu kuwa amefanya uamuzi wa kuachana na mchumba wake huyo. Kusikia hivyo nilijisikia vizuri kwamba nimeeleweka.

Wakati huo nilifikiri ile ilikuwa furaha ya kuona rafiki yangu ameepuka hatari niliyokuwa naiona lakini leo hii ninaamini ile ilikuwa furaha ya kujiona mtu muhimu mwenye busara zinazoweza kusikilizwa na mtu angu wa karibu.

Nafikiri hiki ndicho kinachotokea tunapotoa ushauri kwa watu. Tunajisikia watu wenye uzoefu, uelewa, ujuzi, weledi zaidi. 

Lakini wakati mwingine inakuwa kinyume kama ilivyotokea kwangu. Miezi michache baada ya kumaliza masomo yetu, nikasikia rafiki yangu anamwoa mchumba yule yule aliyekuwa amekubali kuachana naye tukiwa shuleni.

Nilijisikia vibaya. Nikamwona rafiki yangu yule kama msaliti. Kwa nini? Kuukataa ushauri wangu kulimaanisha ule weledi, ujuzi, uzoefu niliokuwa nimefikiri ninao, kuna mtu ameupuuza.

Kwamba hakufanyia kazi kile nimemshauri, maana yake amenidharau. Huenda na wewe umewahi kukutana na matokeo kama hayo katika harakati za kutoa ushauri usiohitajika kwa watu. 

Lakini pia si mara zote unachomshauri mtu hukataliwa. Wakati mwingine unaweza kumshauri mtu jambo akalifanyia kazi kama ulivyomshauri lakini likamletea matatizo.

Chukulia umemshauri rafiki yako afanye biashara ambayo kwa uzoefu wako haitamwangusha. Rafiki yako anakuamini na kweli anaianzisha.

Miezi michache baadaye, anakufuata kuwa amepoteza fedha zake kwa sababu biashara uliyomwambia ingemlipa imekufa. Utajisikiaje? 

Namfahamu mwalimu mmoja mzoefu aliyemshauri mwanafunzi wake akasome masomo ya sayansi kwa kidato cha tano na sita. Moyo wa mwanafunzi yule ulikuwa kwenye masomo ya biashara.

Lakini kwa sababu mwalimu alikuwa amemshawishi kusoma sayansi na alikuwa anafaulu, ilibidi akasome masomo ya Fizikia, Kemia na Hisabati.

Miaka miwili baadaye matokeo ya kidato cha sita yalipotoa, mwanafunzi alimletea mwalimu mrejesho kuwa ameshindwa mtihani na maisha yake yameharibika.

Hiyo ndio hasara ya kutoa ushauri unaoleta matokeo mabaya kwa uliyemshauri.

Nimejifunza kutokutoa ushauri kwa mtu. Hata kama ninaweza kuwa na uelewa wa kile anachokihitaji kuliko yeye, lakini bado siwezi kuelewa undani wa mtu kiasi cha kuamini ninaweza kumwambia nini cha kufanya na kweli kikafanya kazi.

Kuepuka kumwingiza kwenye matatizo yanayoweza kutokana na ushauri wangu, nimejifunza kumpa taarifa. Kumweleza mtu jambo ninalodhani linaweza kumfungua macho badala ya kumwambia nini cha kufanya.

Kuliko kumwambia mtu aachane na mchumba wake, kwa mfano, ninaweza kumweleza matokeo ya kuishi na mtu mwenye tabia fulani. Badala ya kumwelekeza mtu maamuzi anayopaswa kuyachukua kuhusu maisha yake, ninaweza kumpa taarifa zitakazomsaidia kufanya maamuzi yeye mwenyewe.

Badala ya kumfanya mtu ajione hawezi kufanya kitu bila kushauriwa, ninamsaidia kujiamini ili aweze kuyatazama mambo kwa upana wake na kisha achukue maamuzi atakayowajibika nayo yeye mwenyewe. Unakubaliana na funzo hilo?

Je, inawezekana kumpa mtu taarifa bila kumshauri nini cha kufanya?

Na CHRISTIAN BWAYA – Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya Simu: 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles