23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Ushindi ukiwa dhahiri kwa Clinton, Trump afanyeje?

clinton-trumpHUKU kura za maoni za kitaifa zikizidi kuonesha Hillary Clinton anazidisha pengo lake la uongozi la tarakimu mbili, ambalo mapema wiki hii limefikia asilimia 12, Donald Trump anaelekea kupunguza kasi aliyokuwa akija nayo.

Hilo linamwacha Clinton akichanja mbuga kuelekea Jumba Jeupe, yaani Ikulu ya Marekani, huku timu ya mgombea urais wa Republican kwa mara ya kwanza ikikiri mambo si mazuri kwao licha ya kwamba hawajakata tamaa bado.

Iwapo Clinton hatakumbwa na tatizo lolote kiafya au kashfa kama zile zinazovujishwa na mtandao wa WikiLeaks zikiaminika kuwa na mkono wa Urusi inayompigia chapuo Trump, hakutakuwa na kitakachomzuia kuwa mgombea huyo wa chama cha Democratic kuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais wa taifa hilo.

Clinton anaonekana kunufaika na uamuzi wa Serikali ya Ecuador kumzuia mmiliki wa WikiLeaks Julian Assange iliyempa hifadhi katika ubalozi wake mjini London, Uingereza kusitisha ufichuzi wa nyaraka za Clinton na chama chake cha Democratic kwa hofu ya kushawishi matokeo ya uchaguzi huo.

Uwezekano wa Clinton kuzitwaa kura 270 zinazohitajika kumtangaza kuwa mshindi wa kiti cha urais upo wazi hata kama atapoteza majimbo muhimu kama vile Ohio na Florida lakini akihakikisha anatwaa majimbo kama Pennsylvania na Colorado.

Chambuzi kadhaa zinakadiria kuwa Clinton tayari ana uhakika wa kupata kura 300 zikiwa ni zaidi ya zile zinazohitajika kushinda urais hata kama Donald Trump atashinda kila jimbo lenye ushindani mkali.

Bado, kuna njia zenye hatua nyembamba nne kwa mgombea huyo kutoka Chama cha Republican zinazoweza kumpatia ushindi.

Lakini pia haitakuwa rahisi sana kwa sababu Clinton anaonekana kujipanga kuvuruga kila hatua ikiwamo katika majimbo ya kimkakati kwa Trump, ambayo akitaka kushinda urais lazima ayatwae ya North Carolina, Ohio na Florida.

Kuharibu hatua moja kati ya hizo nne, kunamaanisha kuikabidhi White House kwa Democrats kwa muhula wa tatu mfululizo. Trump anatakiwa kuhakikisha anafanikisha yafuatayo ili kuingia Ikulu:

Kwanza; kubakisha kila jimbo aliloshinda Mitt Romney mwaka 2012

Trump lazima abakishe mikononi mwa chama chake kila jimbo ambalo mgombea wao wa urais, Mitt Romney alishinda mwaka 2012 wakati alipopambana na Rais Barack Obama. Hiyo ni pamoja na majimbo ngome za Republican ya Arizona na Georgia, ambako mume wa Hillary Clinton,  Bill aliyatwaa mwaka 1996.

Katika majimbo hayo, Clinton ameyasogelea mno na kufanya mchuano uwe wa karibu, kwa mujibu wa kura za hivi karibuni za maoni.

Katika jimbo la Utah, mgombea binafsi Evan McMullin ameonesha tishio kwa kuziteka kura kutoka waumini wa madhehebu ya Mormon na kuwa na uwezekano wa kushinda jimbo hilo.

Lakini jimbo linalompa changamoto zaidi Trump kulitwaa ni North Carolina, ambalo Mitt Romney alimshinda Obama kwa tofauti ya asilimia mbili tu mwaka 2012. Kura za hivi karibuni za maoni zilizoendeshwa na  CNN/ORC katika jimbo hilo zilionesha Clinton ana asilimia 48 dhidi ya 47 ya  Trump.

Pili: Lazima ashinde jimbo la Ohio

Hakuna mgombea urais kutoka Chama cha Republican aliyeweza kuingia White House bila jimbo la Ohio. Kwa kweli, Donald Trump ili aingie Ikulu lazima ashinde jimbo hilo pia. Matokeo ya kura za mapema yameonesha dalili njema kwa Trump, pengine ikisababishwa na kujitokeza kwa wana Democrats wachache kuliko ilivyokuwa 2012. Kura za maoni za karibuni zimeonesha uongozi mwembamba wa Trump tangu Septemba ukizidi kupungua siku hadi siku: kura za maoni za NBC/WSJ/Marist zimeonesha Trump ana asilimia 42 dhidi ya asilimia 41 za Clinton. Kura nyingine za maoni zilizoendeshwa na Chuo Kikuu cha Quinnipiac zimeonesha wakifungana kwa asilimia 45 kila mmoja.

Tatu: ashinde Florida

Jimbo la Florida linaweza kuwa silaha nzuri kwa kampeni za Hillary Clinton. Kura mbili za maoni zilizoendeshwa na Chuo Kikuu cha Quinnipiac wiki tatu zilizopita zilionesha uongozi mwembamba wa Clinton. Donald Trump hajawahi kuongoza katika jimbo hili tangu Julai mwaka huu na matokeo ya kura za mapema yanaonesha kumpendelea Clinton kulinganisha na ilivyokuwa kwa Obama mwaka 2012.

“Ni wazi kiwango cha kampeni ya Clinton kiko vizuri. Bila kushinda jimbo hili, uwezekano wa Donald Trump kupata kura 270 zinazohitajika kushinda urais utakuwa ndoto.

Nne; kugangamala kupata kura 17

Hata kama Donald Trump atafanikisha kuvuka hatua tatu hapo juu, atahitaji bado kutafuta kura nyingine 17 za kufikisha idadi inayotakiwa ya kura 270. Kwa ujumla amekuwa akiburuza katika kura zote muhimu za maoni tofauti na awali ikitokana na kuibuka kwa mkanda wa video anaosikika akitoa kauli za kudhalilisha wanawake. Hata hivyo, atahitaji moja ya yafuatano kupata kura hizo. Mojawapo wa njia hizo tatu ni pamoja na:

Kushinda jimbo la Pennsylvania. Wapiga kura wa tabaka la wafanyakazi weupe Pennsylvania wanaonekana kuwa fursa nzuri kwa Trump kulichukua jimbo hilo lenye kura 20. Lakini pamoja na kampeni zake na mmiminiko wa matangazo ya televisheni katika dakika za mwisho, kura za maoni za karibuni zilizotolewa na Bloomberg Politics zinaonesaha Clinton akiongoza kwa pengo la pointi tisa. Jimbo hili lingeweza kumsukuma Trump hadi karibu na mstali wa ushindi. Hata hivyo, Pennsylvania halijawahi kwenda kwa Republican tangu mwaka 1988.

Mjumuiko wa majimbo madogo. Mjumuisho wa majimbo yenye kura chache unaweza pia kumwingiza Trump Ikulu. Ushindi katika majimbo madogo ikiwamo Iowa, Nevada, New Hampshire na wilaya ya kibunge ya Maine – unaweza kumfikishia kura 270 zinazohitajika. Ijapokuwa majimbo ya Iowa na Nevada yanaonesha kuwezekana kuwa upande wake, kura za maoni za WMUR/UNH zinaonesha lile la New Hampshire limeegemea kwa Clinton akiongoza kwa pengo la asilimia 15.

Kuna mjumuiko mwingine wa majimbo ya karata za ushindi, ijapokuwa yana changamoto kubwa kwa Trump kumsogeza karibu na mstali wa ushindi, hata hivyo ikitokea muujiza Trump anaweza kufanikiwa azma yake.

Hata hivyo, kura za maoni za hivi karibuni za majimbo haya ya karata za ushindi kama Wisconsin, Virginia, Michigan na Colorado yanaonesha kutua kwa Clinton. Mbaya zaidi Trump hajatumia muda na rasilimali za kutosha katika majimbo haya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles