27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

USHAHIDI WA MAZINGIRA WAPELEKA LULU JELA

NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM


MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemtia hatiani na kumuhukumu kifungo cha miaka miwili jela msanii Elizabeth Michael maarufu Lulu, baada ya kujiridhisha kwamba alimuua Steven Kanumba bila kukusudia.

Hukumu hiyo ilisomwa jana na Jaji Sam Rumanyika, baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wanne wa upande wa Jamhuri na utetezi wa mshtakiwa, huku akisema ‘ushahidi wa mazingira unaweza kumtia hatiani pale ambapo ushahidi wote unamnyooshea kidole mshtakiwa peke yake mwanzo mwisho’.

Akianza kusoma hukumu hiyo, Jaji Rumanyika, alisema mshtakiwa alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aprili mwaka 2012, akishtakiwa kwa kumuua Steven Kanumba Aprili 7 mwaka huo, tukio lililotokea Sinza Vatican.

Alisema Jamhuri ilikuwa na mashahidi wanne na mshtakiwa kwa upande wake alijitetea mwenyewe pamoja na kielelezo cha Josephine Mushumbuzi.

“Jamhuri kwa upande wake imejikitika katika ushahidi wa mazingira, hapakuwepo hata chembe ya ushahidi wa moja kwa moja, mshtakiwa alikubali kwamba yeye ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu ambaye alikuwa mpenzi wake kwa miezi minne.

“Katika mazingira hayo ya mshtakiwa kuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu, sheria inamtaka kutoa maelezo ya kina kuhusu kifo cha marehemu na akishindwa yeye ndiye anakuwa muuaji.

“Ushahidi wa mazingira unaweza kumtia hatiani pale ambapo ushahidi wote unamnyooshea kidole mshtakiwa peke yake mwanzo mwisho… ushahidi wa shahidi wa kwanza ni kwamba kulikuwa na mzozo, ushahidi huo mshtakiwa alikubali kwamba kweli kulikuwa na mzozo akapigwa na marehemu.

“Mwingine anaweza kusema kapigwa au kulikuwa na ugomvi, tafsiri ya ugomvi ni ile kurushiana maneno ya kejeli, dharau, kizembe, kwa aliyeanzisha alikuwa na nia ya kumuudhi mwenzake… hilo si la msingi sana, kwa maoni yangu kutokana na tafsiri hiyo basi kuanguka ni miongoni mwa matukio yanayotazamiwa kutokea katika ugomvi,” alisema Jaji Rumanyika.

Alisema mshtakiwa katika utetezi wake alisema marehemu alikuwa kalewa na kwa msingi huo mlevi kati ya mambo anayofanya ni kuanguka ovyo.

“Kuhusu hili mshtakiwa alijikanganya, anasema marehemu alimfukuza akammudu kumkamata akafanikiwa kumrudisha chumbani kwa kumburuza, lakini hakusema wakati akimfukuza na kumburuza kama alikuwa akianguka.

“Maelezo ya Josephine Mushumbuzi sio taarifa ya hospitali, hayakuwa na hadhi ya cheti cha hospitali na mahakama haikuwahi kuambiwa Mushumbuzi naye alikuwa miongoni mwa madaktari wa uchunguzi.

“Daktari wa familia na mshtakiwa walitakiwa kueleza historia ya maradhi ya marehemu kwa sababu alikuwa mpenzi wake kwa miezi minne, lakini hawakufanya hivyo.

“Mazingira yanakinzana na hekima ya kawaida… hata pale marehemu alipoendelea kumpiga mshtakiwa, akaenda kiwango cha kutaka kumuua kwa panga, mshtakiwa hakurudishia wala kutaka kumsukuma… ni kama mshtakiwa alichukua taratibu za kwenye biblia… akipiga shavu la kushoto mgeuzie na shavu la kulia… Lakini hayo hakusema katika utetezi wake,” alisema.

Jaji Rumanyika alisema mshtakiwa alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu, hivyo alitakiwa kuelezea nini kilitokea.

“Tunabakia na watu wawili wa kusema kwa kina kuhusiana na tukio hili, ambao ni mshtakiwa na marehemu… Marehemu hata akifufuka kwa muujiza, mahakama haitasikiliza muujiza.

“Pengine anaweza akatokea mtu mwingine akasema Aprili 7, 2012 wakati tukio likitokea mshtakiwa alikuwa na umri wa miaka 17, hakuwa mtu mzima… kwa umri huo anaweza kusema asingeweza kujua mabaya.

“Hili lina mazingira yake makuu matatu… moja, alikuwa mtoto aliyefikia hatua fulani akiitwa mke alikubali, pili, mtoto wa aina yake mshtakiwa alithubutu na kuamua ndivyo sivyo kwa matakwa yake.

“Anajiamulia wapi aende na tatu, mtoto wa aina yake mshtakiwa anaamua kwenda matembezini usiku wa manane, akamtembelea mpenzi wake na kisha akaendelea na matembezi yake.

“Mshtakiwa huyu si wale watoto waliolengwa kulindwa katika sheria ya mtoto… Kama mtoto anaweza kufanya ya watu wazima na akajiamini kuyafanya ni mkomavu.

“Sitaki kuwa wa kwanza kuonyesha kushindwa… Kifo cha marehemu Kanumba kimetokana na mshtakiwa, kifo kinachotokana na ugomvi hupelekea aina hii ya mashauri,” alisema Jaji Rumanyika.

Alisema sheria ya kuua bila kukusudia ina lengo la kudhibiti vitendo hivyo na kwamba katika mashauri mengi muuaji si lazima ithibitike.

“Kwa kuwa mshtakiwa kasema marehemu alikuwa na wivu usio na msingi, wivu huo ndio ulisababisha kupigwa… hakuna mchezo usio na kanuni… mapenzi ni mchezo basi wivu ndio kanuni zake.

“Kama aliamua kuingia katika mchezo, basi afuate kanuni, wivu wa maendeleo huzaa maendeleo, lakini wivu wa mapenzi huzaa maangamizi. Mshtakiwa alijua marehemu ana wivu, basi alipoanza kushukiwa kuhusu simu, alitakiwa kwa kanuni ya mapenzi aache simu, lakini yeye aliamua kama noma na iwe noma.

“Kutokana na ushahidi huo, mahakama inamtia hatiani mshtakiwa chini ya kifungu namba 195 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu,” alisema Jaji Rumanyika na kuwataka mawakili wa pande zote kusema lolote dhidi ya mshtakiwa.

Kipindi chote baada ya kutiwa hatiani, Lulu alikuwa hatulii kizimbani, mara anapandisha dera lake na kulishusha, mara anafunga mikono maeneo ya tumboni, kifuani na wakati mwingine alikuwa akipeleka mikono yake yote miwili katika mashavu yake.

Akimtetea mshtakiwa apunguziwe adhabu, Wakili Peter Kibatala, aliomba mahakama impe kifungo cha nje. Aliomba apewe adhabu ndogo kwa sababu anategemewa na mama yake pamoja na mdogo wake.

Kibatala alisema mshtakiwa alipata fundisho, hivi sasa kabadilika, anasoma na amekuwa balozi katika taasisi mbalimbali.

Aliomba apunguziwe adhabu pia kwa sababu baada ya tukio hilo kutokea, alikaa gerezani miezi 10 hadi alipopewa dhamana Oktoba mwaka 2013.

Kwa upande wake, mawakili wa upande Jamhuri wao waliomba mshitakiwa apewe adhabu ili iwe fundisho kwa watu wengine.

Baada ya maelezo hayo ya mawakili, Jaji Rumanyika, alihitimisha hukumu yake kwa kusema: “Vitu vya kuangalia ni vingi, wahalifu ni mazao ya jamii, lazima mahakama izingatie matakwa ya sheria. Mshtakiwa anahukumiwa kutumikia kifungo cha miaka miwili jela.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles