33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Urais Zanzibar kaa la moto

*Vikao vya juu vyatoa onyo la mwisho, yapeleka hofu ya vigogo kuanguka madarakani

NA AZIZA MASOUD,DAR ES SALAAM

Chama  Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Halmashauri Kuu ya Taifa(NEC) kimetoa kalipio la mwisho  kwa wanachama wa chama hicho wanaokiuka  katiba,kanuni ya uchaguzi  na ya uongozi  na maadili  kwa kuanza kufanya kampeni za kificho  na za wazi za urais wa Zanzibar.

Kalipio hilo la kwanza kwa NEC lilitolewa jana katika kikao chake kilichoketi  jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Rais Dk.John Magufuli.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho Humphrey Polepole  ilisisitiza kuwa; “Kufanya hivyo ni  kwenda kinyume na utamaduni na desturi njema za  chama ambazo kwa pamoja zinatuongoza kuwapata viongozi wa CCM na serikali zake,”.

Onyo hilo limetolewa ikiwa imebaki miaka miwili  kufanyika Uchaguzi  Mkuu wa mwaka 2020  ambapo rais aliyepo madarakani kwa  sasa Dk.Ally Mohammed Shein atakuwa amemaliza muda wake  baada ya kuongoza Kisiwa hicho kipindi cha miaka kumi na  kwa mujibu wa Katiba hataruhusiwa kugombea.

Kwa mantiki hiyo ni jambo la kawaida kwa wanasiasa kuanza kujipanga au kupanga safu zao na mara nyingi uchaguzi kama huo huambatana na vikumbo vingi vya kisiasa kwa kila kambi kuhakikisha wanayemuunga mkono anasimamishwa kugombea urais.

Hii si mara ya kwanza kwa CCM kutoa onyo kwa watu ambao wameanza harakati za kuusaka urais Zanzibar.

Agosti  18  mwaka huu Katibu Mkuu wa CCM Taifa,  Dk.Bashiru Ally akiwa visiwani humo alitumia neno ‘wakome’ kuwaonya wana- CCM walioanza kampeni za wazi na kificho kuusaka ukuu huo wa dola.

Dk.Bashiru alisema amesikia wapo watu ambao wengine wana vyeo na wengine hawana  wana ndoto ya kushika madaraka ya  urais Zanzibar  na kuwataarifu kuwa nafasi hiyo bado haijatangazwa kama ipo wazi.

“Nafasi ya urais Zanzibar  haijatangazwa kuwa ipo wazi bado ina mwenyewe na kutakuwa na utaratibu wa kuijaza,utaratibu huo utasimamiwa na chama sio makundi hayo mnayoyapitisha pitisha mara kwenye hoteli mara kwenye ofisi za serikali komeni tabia  hiyo acheni,” alisema Dk. Bashiru.

Alisema CCM sio chama cha kusaka vyeo bali ni chama cha Mapinduzi na kwamba wataendelea kuwafuatilia  wasaka vyeo kwa kuwa wengine wanawajua na siku zao zinahesabiwa.

Aliwataka watu hao wamuache Dk. Shein amalize kipindi chake kwa heshima  na wakati ukifika  chama hicho kitasema na kuweka utaratibu wa kumpata mtu atakayejaza nafasi hiyo.

Mbali na Dk.Bashiru  kiongozi mwingine aliyetoa onyo hilo ni Rais Dk.Shein ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar  alipokuwa katika ziara yake ya kutembelea mashina ya chama hicho katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.

Dk.Shein aliwaonya baadhi ya watu wanaofanya kampeni za kusaka urais wa Zanzibar kabla ya muda wa kufanya hivyo kufika na kusisitiza kuwa yeye bado ni Rais wa Zanzibar.

Alisema kuna baadhi ya viongozi wa chama na serikali tayari wameanza kupanga timu za urais badala ya kushughulika na mambo ya msingi ya kufanya shughuli za chama zitakazofanikisha kuiweka serikali madarakani katika uchaguzi mkuu ujao.

“Nafasi ya urais ndani ya CCM haipatikani kwa kampeni na makundi yasiyo halali bali kwa utaratibu maalumu kupitia vikao vya kikatiba ambavyo vipo kwa mujibu wa Katiba na miongozo na kanuni  mbali mbali za CCM,” amesema.

Dk. Shein pia aliwatahadharisha kuwa watu hao wasipoacha tabia hiyo na kuvumilia hadi 2020, atawachukulia hatua kali za kinidhamu zikiwemo kufikishwa katika vikao vya usalama na maadili vya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) ili wahojiwe na kuchunguzwa dhidi ya mwenendo wao  usiokuwa na manufaa kwa CCM.

Bado haijajulikana kama katika kikao cha jana Dk. Shein alifikisha malalamiko hayo rasmi au la baada ya kuahidi kufanya hivyo.

Pamoja na hayo onyo hilo la mwisho la CCM tayari limeleta hisia tofauti tofauti ndani na nje ya chama hicho kwani wapo ambao wanaona kwamba endapo wahusika hawatasikia, huenda baadhi ya viongozi na watu walioteuliwa kushika madaraka fulani fulani wakaondolewa kutokana na ama wenyewe au makundi yao kuwa miongoni  mwa yale yanayotajwa kuanza harakati za kuusaka urais wa Zanzibar.

Mbali  masuala ya urais wa Zanzibar, kikao cha NEC pia  kimemteua Ramadhani Hamza Chande kuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi mdogo wa uwakilishi wa jimbo la Jang’ombe.

Uchaguzi wa jimbo hilo ambao utasimamiwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar(ZEC) unatarajiwa kufanyika Oktoba 27  baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Abdalla Maulid Diwani kuvuliwa uanachama wa CCM na kupoteza sifa ya kushika nafasi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles