33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Uozo vyama vya siasa

Jaji Francis Mutungi
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi

Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2012/13, imeibua uozo mkubwa katika hesabu za vyama vya siasa.

Mbali ya uozo huo, CAG pia amebaini baadhi ya vyama havina ofisi badala yake vimepanga hotelini na vingine sehemu za uchochoroni.

Ripoti hiyo inaonyesha Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Tanzania Labour (TLP), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na NCCR-Mageuzi ambavyo vyote vina uwakilishi bungeni vimepata hati ya shaka katika hesabu zao.

Aidha ripoti hiyo imebaini kuwapo matumizi mabaya ya fedha yasiyozingatia sheria kwa vyama vya UMD, PPT-Maendeleo, ADC-Tanzania, NLD, SAU na CHAUMA ambavyo kwa pamoja vimepata hati chafu.

CAG alishindwa kufanya ukaguzi kwa Chama cha United Democratic (UDP), kutokana na kukosena kwa hesabu zake.

Akitoa taarifa ya ukaguzi wa vyama vya siasa mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) jijini Dar es Salaam jana, Mkaguzi Msaidizi kutoka ofisi ya CAG, Benja Majura, alisema pamoja na kubaini upungufu huo, baadhi ya vyama vinashindwa kufanya kazi zake vizuri kutokana na kukosa ofisi na samani.

Alisema katika ripoti hiyo, kumejitokeza matumizi mabaya ya fedha za rukuzu yanayotokana na kutokuwapo kwa wahasibu au wataalamu wa masuala ya fedha, jambo ambalo limesababisha viongozi wa vyama hivyo kufanya wanavyotaka.

“Katika vyama hivi, baadhi ya viongozi wameshindwa kutupatia ushirikiano ikiwamo kutoa vielelezo vya matumizi ya fedha za rukuzu kwenye vyama vyao hali iliyosababisha kufanya kazi katika mazingira magumu,” alisema Majura.

Undugu

Alisema kuna baadhi ya vyama vimeweka ndugu zao kushika nafasi ya uhasibu hata kama hawana taaluma wala vigezo.

“Kuna baadhi ya vyama vimepanga kwenye vichochoro, hata ukimwelekeza mtu anashindwa kuelewa ramani yake, lakini tulijitahidi kufika ili kutimiza wajibu wetu. Vyama hivi hivi ndani ya ofisi zao kuna meza na kiti kimoja hata mahali pa kukaa hakuna.

“Katika mazingira kama haya sijui tulikuwa tunakagua nini, ukimuuliza mhasibu wa chama hajui chochote kuhusu matumizi ya fedha za ruzuku.

“Wengine wana uhusiano na viongozi wa chama ndiyo maana wanawapa fursa ya kushika nafasi hizi hata kama hawana vigezo,” alisema Majura.

Vyama kuhama

Majura alisema licha ya kubaini hali hiyo, baadhi ya vyama vimekuwa vikihama ofisi zao siku hadi siku jambo ambalo linawafanya washindwe kujua mahali ofisi hizo zilipo.

Alisema matatizo mengine ni vyama kutoa karatasi moja ya matumizi ya fedha za ruzuku na vingine kuficha hesabu zao zisikaguliwe.

“Kuna baadhi ya vyama tumekuta mgombea alitumia fedha zake wakati wa kampeni, lakini alipomaliza alikwenda kudai alipwe fedha hizo bila ya kuwapo maelezo yanayojitosheleza,” alisema.

Alisema matatizo mengine yanayojitokeza ni kutokuwapo kwa utaratibu wa pamoja wa kukagua hesabu za vyama, jambo ambalo limesababisha vyama vingine kuwasilisha mwisho wa mwaka na vingine kufuata utaratibu wa Serikali wa kuwasilisha Machi ili ifikapo Oktoba mwishoni ripoti ya ukaguzi iwasilishwe kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

MSAJILI wa vyama

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alisema kati ya vyama 22 vyenye usajili wa kudumu, ni 12 tu vimekaguliwa hesabu zao na CAG.

Jaji Mutungi alisema kati ya vyama hivyo, ni 6 tu vimewasilisha ripoti kwa mujibu wa sheria.

Alivitaja vyama vilivyowasilisha taarifa zao kwake ni CCM, CUF, ADC, PPT-Maendeleo, UMD na NLD.

RUZUKU SHAKANI

Jaji Mutungi alisema kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa, chama ambacho kitashindwa kuwasilisha hesabu zake kwa msajili kinapaswa kukatwa ruzuku.

Alivitaja vyama vinavyopata ruzuku ya Serikali hadi sasa ni UDP, CCM, TLP, NLD, Chadema, NCCR-Mageuzi na DP.

Alisema changamoto iliyopo ndani ya vyama ni baadhi kutojipanga na upokeaji wa fedha za rukuzu, jambo ambalo wanaamini fedha hizo zinatumika kwenye mambo yao binafsi.

Jaji Mutungi alisema vyama vinatakiwa kuwasilisha hesabu ya fedha zote zinazoingia kwenye chama hata kama nyingine zimetolewa na wafadhili wa aina mbalimbali.

Alisema utafiti unafanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu kuangalia namna ya kuvisaidia vyama ambavyo havipati rukuzu ili viweze kujiendesha katika shughuli zao.

“Vyama hivi vitapewa asilimia fulani ya mapato na vile ambavyo vina uwakilishi pia vitapewa asilimia fulani. Hali hii itasaidia kuondoa malalamiko ya ukata kwa baadhi ya vyama jambo ambalo linaweza kuwasaidia kujiendesha,” alisema Jaji Mutungi.

ZITTO ANG’AKA

Akitoa agizo la Kamati ya Bunge, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alisema kamati hiyo itaunda timu ya wabunge wanne ambao watashirikiana na CAG na Msajili wa Vyama vya Siasa kwa ajili ya kwenda India kujifunza namna ya kufanya ukaguzi kwenye vyama vya siasa.

Alisema ripoti ya mafunzo hayo itawasilishwa kwenye kamati hiyo ili wajumbe waipitie na kuangalia maeneo ambayo yanaweza kuboreshwa.

“Kuwe na ‘condition’ za kutoa rukuzu kwa vyama, ikiwamo ya kuwapo kwa mhasibu anayetambulika kisheria na kwamba chama ambacho kitakwenda kinyume na utaratibu huo hakitakidhi vigezo vya kupewa rukuzu,” alisema Zitto.

Alisema ripoti ya vyama hivyo iwekwe kwenye tovuti ya msajili ili wananchi waweze kuona matumizi ya fedha na kuwawajibisha viongozi wa vyama vyao.

“Wahusika watakaobainika wametumia vibaya fedha za rukuzu kwenye vyama wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa vyama vingine,” alisema.

Oktoba 20, mwaka jana, Zitto aliibua mjadala mzito kuhusu ruzuku ndani ya vyama vya siasa ambapo aliitaka Ofisi ya CAG kuchunguza uzembe wa kushindwa kukagua hesabu za vyama vya siasa kwa muda wa miaka mitatu.

Alisema CAG ameshindwa kukagua ruzuku ya Sh bilioni 83 iliyotolewa kwa vyama vya siasa nchini tangu mwaka 2005 hadi 2010.

Zitto alisema ingawa kuna tatizo katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, CAG hawezi kumtupia mzigo huo pekee yake kwani naye anahusika.

“Ruzuku ya vyama vya siasa ni eneo ambalo huwa haliangaliwi kabisa, na fedha nyingi za walipakodi zinakwenda katika vyama. Kuanzia mwaka 2005 hadi 2010 Sh bilioni  83 zimetolewa kama ruzuku kwa vyama vya siasa,” alisema Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Nimeipenda hii “Alisema ripoti ya vyama hivyo iwekwe kwenye tovuti ya msajili ili wananchi waweze kuona matumizi ya fedha na kuwawajibisha viongozi wa vyama vyao”. Ni Zitto huyu huyu ambaye alishiriki kupitisha katiba inayopendekezwa ambayo inamnyima mwananchi aliyemchagua mbuge kumuwajibisha iwapo ataona hatekelezi majukumu yake. Shhhhhhhhh. Nasikia eti Ziro anamtaka awe waziri wake mkuu kwa sababu ni kijana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles