31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

United walichelewa wapi kumsajili Bruno Fernandes?

Badi Mchomollo

SWALI kubwa kwa mashabiki wa Manchester United ni kwamba, wangekuwa wapi kwa sasa endapo wangefanikiwa kuinasa mapema saini ya Bruno Fernandes ambaye alikuwa anakipiga katika klabu ya Sporting Lisbon ya nchini Ureno.

United walikuwa wakiiwinda saini ya mchezaji huyo kwa kipindi kirefu, lakini wakaja kufanikiwa kuipata wakati wa uhamisho wa dirisha dogo la Januari mwaka huu kwa uhamisho wa kiticha cha pouni milioni 68.

Mipango hiyo ya kuitaka saini yake ilikuwa kwa lengo la kutaka kuziba nafasi ya kiungo wao Paul Pogba ambaye kwa sasa ni kipindi kirefu hajaonekana uwanjani kutokana na majeruhi, likini mchezaji huyo ameonesha dalili ya kutaka kuondoka ndani ya viwanja hivyo vya Old Trafford.

Pogba amekuwa akihusishwa kutaka kuondoka tangu mwishoni mwa msimu uliopita, huku klabu yake ya zamani ya Juventus wakihitaji huduma yake pamoja na Real Madrid, hivyo Manchester United walitakiwa kuliona hilo mapema na kutafuta mchezaji ambaye angeweza kuwasaidia kipindi hicho chote kwenye misimamo ya michuano mbalimbali.

Pogba ni mmoja kati ya viungo ambao wamesajiliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha duniani, hivyo Manchester walikuwa na imani na mchezaji huyo kuwa anaweza kuwasaidia hasa kwenye michuano ya Ligi Kuu England pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo hadi sasa hawajafanikiwa kuyachukua tangu alipoondoka kocha wao Sir Alex Ferguson.

Baada ya Pogba kuanza kusumbua kikosini huku akidai anataka kuondoka, kocha wa timu hiyo Ole Gunnar Solskjaer akaanza kumpa nafasi kinda Scott McTominay, Nemanja Matic, Jesse Lingard, lakini bado hawakuwa na msaada mkubwa wa kuifanya timu hiyo kuwa kwenye ubora wao.

Hapo ndipo ulikuwa wakati sahihi wa kuitafuta saini ya mchezaji mwenye uwezo wa Bruno au zaidi kwa kipindi hicho, lakini Manchester United wakaamua kumtafuta Bruno huku tayari timu hiyo ikiwa kwenye wakati mgumu katika michuano ya Ligi Kuu England pamoja na michuano mingine.

Bruno alikuwa mchezaji sahihi wa kujiunga na Manchester United mara baada ya kumalizika kwa msimu uliopita, ingewezekana kuwa Manchester miongoni mwa timu ambazo zinashika nafasi nne za juu kwa sasa kutokana na ubora na ubunifu wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 raia wa nchini Ureno.

Hadi sasa amecheza jumla ya michezo mitatu ya Ligi Kuu nchini England tangu amesajiliwa na kufunga bao moja, akitoa pasi mbili za mwisho moja kwenye ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Chelsea na nyingine kwenye mchezo dhidi ya Watford ambapo Manchester United ilifanikiwa kushinda mabao 3-0.

Juzi mchezaji huyo alifanikiwa kupata bao lake la kwanza kwenye michuano ya Kombe la Europa wakati Manchester United inafanikiwa kushinda mabao 5-0 dhidi ya Club Brugge katika hatua ya 32 bora ya michuano hiyo.

Mbali na kufunga bao hilo lakini alikuwa kwenye kiwango cha hali ya juu huku akihusika kwenye kutengeneza mashambulizi mengi yaliyofanywa na Manchester United. Mabao mawili yaliyofungwa na Scott McTominay, Odion Ighalo alihusika kwenye kutengeneza mashambulizi.

Tayari mashabiki wa Manchester United wameanza kutamba huku wakiamini wamepata mwokozi wao katika eneo la kiungo hata kama Pogba akitangaza kuondoka mwishoni mwa msimu huu mbadala wake amepatikana.

Kwa michezo mitano aliyocheza tangu ajiunge tayari ametoa pasi mbili za mabao pamoja na yeye mwenyewe kufunga mabao mawili, jambo ambalo linawapa matumaini makubwa sana.

Katika mchezo wa juzi, mashabiki wameanza kuliimba jina la Bruno hasa kutokana na kile alichokifanya kwenye mchezo huo japokuwa hakumaliza dakika 90 kabla ya kocha Solskjaer kumpumzisha.

Hii ni ishara tosha kuwa Pogba hana thamani kubwa tenda ndani ya kikosi hicho, hivyo anaweza kuondoka na mashabiki wasiwe na wasiwasi yoyote kwa kuwa wamepata mtu sahihi wa kuipigania timu hiyo.

Lakini kwa sasa Manchester United wanaweza wasiione thamani kubwa ya Bruno kwa kuwa amejiunga mwishoni mwa msimu japokuwa tayari ameonesha ana kitu ambacho wamekuwa wakikosa kwa kipindi kirefu.

Lawama kubwa zinakwenda kwa Mwenyekiti wa klabu hiyo Ed Woodward ambaye anadaiwa kuwa mgumu kuweka fedha mezani kwa ajili ya usajili huku timu hiyo inatajwa kuwa miongoni mwa timu duniani ambazo zinaingiza kiasi kikubwa cha fedha.

Kabla ya Manchester United kufanikiwa kuinasa saini ya Bruno Fernandes wakati wa Januari, mashabiki wa timu hiyo walikuja juu wakimtaka Woodward kuachia ngazi pamoja na viongozi wa timu kutokana na kushindwa kuwanasa baadhi ya wachezaji ambao walikuwa wanawahusisha kuwawinda.

Wapo mashabiki ambao walikwenda hadi nyumbani kwa Woodward na kutishia kuichoma nyumba yake moto, hivyo kutokana na hali hiyo wakaamua kuweka mezani kitita cha fedha na kuinasa saini ya Bruno Fernandes.

Lakini kama maamuzi hayo ya kumsajili mchezaji huyo yangefanyika mara baada ya kumalizika kwa msimu uliopita, basi Manchester United wangekuwa kwenye nafasi za juu kwa kuwa mchezaji huyo ni mbunifu kwenye kupiga pasi za mwisho kwa washambuliaji wake pamona na yeye mwenyewe kuwa na uwezo wa kufunga mabao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles