31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Siri ya kijana mtoboa macho Buguruni Dar

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam akiwa na kijana Said Ally aliyeruhuiwa kwa kutolewa macho na Scorpion
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiwa na kijana Said Ally aliyejeruhiwa kwa kutolewa macho na Scorpion.

JOHANES RESPECHIUS Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

MTUHUMIWA wa tukio la kumchoma kisu na kumtoa macho, Said Ally, maarufu kama ‘Scorpion’, anadaiwa kuwa ni mbabe ambaye anaogofya kila mtu mtaani kwake eneo la Buguruni kwa Mnyamani Wilaya ya Ilala,   Dar es Salaam.

MTANZANIA ambalo  lilipiga kambi katika eneo hilo jana liliweza kupata taarifa za ndani kuhusu kijana huyo ambaye tayari yuko mikononi mwa Jeshi la Polisi.

Jina la Scorpion lilianza kusikika katika vyombo vya habari mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya Kituo cha redio cha Clouds FM kutoa siri za kijana huyo aliyemjeruhi Ally ambaye ni kinyozi kwa kumtoboa macho na kumsababishia upofu.

Mmoja wa wauza kuku (jina tunalo) ambako Ally alijeruhiwa, aliliambia MTANZANIA kuwa Scorpion amekuwa akiogopwa na kila mtu katika mtaa huo na hata wakati anampiga na kumjeruhi Ally, hakuna mtu aliyejitokeza kumsaidia.

Alisema kila siku ‘mbabe’ huyo wa mtaa alikuwa akifika kwenye eneo hilo saa 12 jioni na kutangaza kwamba yeye ndiye mlinzi wa eneo hilo na hakuna ruksa kwa mtu mwingine kukatiza maeneo hayo.

Katika simulizi hiyo, ilielezwa Scorpion alikuwa na utaalamu wa karate ambao aliutumia kupora watu fedha na vitu mbalimbali.

Ilielezwa kuwa baada ya hapo huwapiga na kuwajeruhi kabla ya kuwarusha barabarani  wagongwe na magari au pikipiki ili kupoteza ushahidi.

“Mtaa mzima unamuogopa Scorpion ambaye alipenda kujiita ‘teacher’ kutokana na vitendo vyake vya kupiga na kupora watu bila kificho na wakati mwingine kuwasukumia barabarani  wagongwe na magari kwa lengo la kupoteza ushahidi.

“Yule alikuwa mtawala wa eneo hili, hata vibaka walikuwa wanamwogopa hawakuthubutu kukaribia katika eneo lake.

“Ni ukweli kwamba hata polisi wa Kituo cha Polisi Buguruni  walimlea kwa sababu taarifa zake walikuwanazo muda mrefu lakini hawakuchukua hatua hatua zozote.

“Na hata katika tukio la juzi, polisi walipofika walishindwa kumkamata huku wakiwataka  wananchi ndiyo wamkamate na kumpeleka kituoni,” alisema kijana huyo kwa sharti la kutotajwa jina.

Mkazi mwingine wa mtaa huo, alisema huenda Scorpion ni miongoni mwa vijana waliopitia mafunzo ya  jeshi na baadaye kuachwa mtaani hivyo alikuwa akitumia ujuzi huo kufanya uhalifu.

“Scorpion alikuwa anasema kuwa anazuia  wezi na kwamba ana kibali cha kufanya kazi hiyo na askari walikuwa wakimwona na kumwacha.

“Hata lile tukio alilolifanya la kumtoboa macho yule kinyozi hakuna mtu ambaye angejitoa mhanga kwenda kumkamata kwa  jinsi alivyojiweka mtaani hapa,” alisema mkazi huyo.

Mkazi huyo alisema Ally aliposhuka kwenye bajaji na kusogea  apate kununua kuku kwenye kibanda cha chips, Scorpion aliyekuwa amekaa karibu na  meza za kuku alinyanyuka na kwenda nyuma yake.

“Sijui alimuuliza jambo gani na Ally hakumjibu ndipo alipoanza kumchoma visu mgongoni, kisha kumtoboa macho na kumwacha pale.

“Polisi walipokuja kumchukua majeruhi   Scorpion alikuwa ameketi pembeni lakini askari hawakumgusa hadi walipokuja wenzao kutoka Kituo cha Stakishari ndiyo waliweza kumkamata,” alisema.

Meneja wa baa ya Kimboka iliyosemekana kuwa Scorpion alikuwa akifanya shughuli za ulinzi, Athumani Mwambe, alisema alikuwa akimwona nyakati za usiku lakini hakuwa analinda kwenye baa yake.

“Mtu huyu hakuwahi kuwa mlinzi wa baa hii labda alikuwa akionekana mtaani na kujifanya anazuia  wezi waliokuwa wakifanya matukio.

“Alishajifanya ndiye mbabe wa mtaa huu kwa hiyo watu wengi walimuogopa.

“Vibaka wote wa mtaa huu walikwishamkimbia  hivyo hata angefanya jambo gani hakukuwa na mtu wa kumgusa,” alisema.

Mkazi mwingine wa eneo hilo Salome Mgaya alisema: “Tumekuwa watu wa kuishi kwa hofu kwa kipindi kirefu na  inafikia mahali hata pale unapokuwa umechelewa kurejea nyumbani kutoka kwenye mihangaiko ya maisha unakuwa huna amani kwa kuhofia usalama wako.

“Kwani mtu huyu alikuwa akikukuta njiani basi utakachokuwa nacho ni halali yake… lakini shida huja pale unapokuwa huna kitu, utapigwa na kuumizwa vibaya”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles