24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

UNAZITAZAMAJE FURSA ZILIZOPO VIJIJINI?

Na ATHUMANI MOHAMED

BINADAMU aliyekamilika ni lazima atakuwa na fikra za namna gani anaweza kujikwamua na kutengeneza fedha ili maisha yake yawe mazuri. Hakuna anayependa kuishi maisha ya mateso.

Kwa hakika kila mtu anapenda kufanikiwa maishani mwake. Huo ndiyo ukweli. Jambo la msingi la kufikiri ni njia gani unaweza kutafuta mafanikio na kubadilisha maisha yako.

Wengi huwaza na kutafuta majibu ya swali hilo, maana mafanikio ndiyo jambo la msingi, lenye maana zaidi kwenye maisha. Asilimia kubwa huamini kuwa mafanikio yapo mjini. Inawezekana wazo hilo likawa na ukweli kwa namna moja ama nyingine.

Lakini ni vyema kujiuliza, ni kweli fursa zote za mafanikio zipo sehemu za mijini pekee? Jibu ni jepesi tu; si kweli. Siyo lazima watu wote wakimbilie mijini ndipo watakapoweza kufanikiwa.

Kuna fursa kubwa sana kwenye kilimo na hata biashara sehemu za vijijini. Tatizo wengi (na hasa vijana) hudanganyika na mafanikio ya nje. Labda kwa kule tu kuishi mjini, mtu anaona ni sehemu ya mafanikio, jambo ambalo kwa hakika halina ukweli wowote.

 

NI MAZOEA MABAYA

Achana na fikra za kizamani, kwamba maisha bora yapo mijini tu. Ndugu zangu, ukweli ni kwamba wapo watu wengi sana mijini ambao hawajui hata mchana utapita vipi, kwa namna wanavyopigwa na maisha.

Usifikiri kwa ‘shotikati’, hakuna njia ya mkato ya mafanikio. Wanasema hakuna mafanikio ya usiku mmoja. Ukitafakari hilo tu, litakupa ujasiri wa kufikiri tofauti na kuona njia za kuwekeza vijijini ambapo watu wengi wanapadharau.

Anza kwa kusugua bongo lako. Jiulize: “Hivi mimi nifanye nini ili nifanikiwe kimaisha nikiwa kijijini?”

Hili si kwa ajili ya wale ambao wapo vijijini pekee, bali hata kwa wale ambao wapo mijini, wanaweza kutafakari hili na baadaye kufikia uamuzi wa kwenda kuwekeza vijijini.

Kuishi mjini bila kuwa na kitu cha maana kinachokuingizia fedha, siyo ujanja. Tazama kwa mapana fursa zinazoweza kupatikana hata vijijini. Ukijipa muda, bila shaka utashangaa namna fursa zinavyofunguka zenyewe kiulaini kabisa.

 

KUNA FURSA GANI?

Vijiji vingi vinafikika, wajanja siku hizi wanaangalia namna ya kupata fedha wakiwa vijijini. Unaweza kuwa hata na bodaboda, ukawa unafanya biashara ya kuwatoa abiria kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine na ukaingiza fedha.

Kumbuka kwamba, hata kama utapata fedha ambazo si nyingi sana kwa kutwa, kwa sababu matumizi ya vijijini ni tofauti kabisa na mijini, maana yake utakuwa unaingiza fedha nyingi zaidi kwa mtindo huo.

Tazama biashara kwa jicho pana. Angalia tatizo linalowakabili zaidi katika eneo unalokusudia kufanya biashara. Wakati wenzako wakiangalia matatizo na kuona huruma, wewe tazama tatizo kama fursa ya biashara.

Mfano kama upo eneo kuna shida la viatu; watu wanatembea miguu peku na labda kama viatu vipo ni vya bei kubwa. Hiyo ni fursa kwako. Angalia namna ya kuweka oda ya viatu vya bei nafuu kiwandani, kisha uwapelekee kijijini, utauza kwa wingi na utapata faida kubwa.

Vipo vingi, ni kiasi cha wewe kuangalia na kuchagua kipi ufanye kama fursa yako ya kibiashara.

 

KILIMO NI BIASHARA YA UHAKIKA

Sekta ya kilimo kwa sasa imekua. Acha kudanganyika, ukichagua kilimo bora na hasa cha umwagiliaji, utakuwa na uhakika wa kutengeneza fedha nyingi zaidi kuliko kukimbilia kuuza mitumba mijini!

Mazao kama vitunguu, karoti, pilipili hoho, nyanya na mbogamboga kwa ujumla wake, kinalipa sana. Ufuta na alizeti pia ni kati ya mazao ya biashara yenye fedha nyingi za uhakika.

Fanya tafiti kuhusu mazao unayotarajia kulima, kisha anza kidogokidogo kabla ya kuwa mkulima mkubwa hapo baadaye. Achana na porojo za vijiweni, vijijini fursa zipo sana. Ni suala la kuzitazama kwa jicho pana na kufanyia kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles