30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

UNAVYOWEZA KUWA NA FURAHA KATIKA NYAKATI NGUMU

Na CHRISTIAN BWAYA,

FIKIRIA mwajiri wako anatishia kukuachisha kazi. Kosa ulilolifanya linastahili adhabu inayoweza kukugharimu. Unapofikiria matokeo ya kukosa kazi, fedheha ya kufukuzwa, unakosa usingizi.

Kukosa usingizi, kimsingi, kunaletwa na fikra za kujilaumu kwa kujiingiza kwenye matatizo usiyoweza kuyatatua. Wakati mwingine shida ni mawazo ya namna utakavyojinasua na matokeo ya kosa lako.

Unafikiria kwanini ulifanya ‘kosa la kijinga’ ambalo ungeweza kuliepuka. Unafikiri namna ya kujinasua na matokeo ya makosa yako mwenyewe. Haya yote yatakuongezea matatizo badala ya kukusaidia kutatua matatizo.

Usijilaumu kwa makosa usiyoyarekebisha

Kujilaumu kwa makosa tusiyoweza kuyarekebisha kunachangia kutunyong’onyeza. Mara nyingi, tunapoteza muda na nguvu kutafakari mambo magumu tuliyonayo hata kama hatubadili chochote. Kutokujilaumu kwa magumu tusiyoyabadili ni namna nzuri ya kulinda amani yetu.

Kama umefanya makosa kazini, kukubali kuwa tayari umefanya makosa ni muhimu. Unaposikitika na kujilaumu kwa makosa usiyoweza kuyabadili, unajiumiza bila sababu ya msingi. Hubadili chochote kwa kusikitika kwanini ulifanya hicho ulichokifanya. Hubadili matokeo kwa kuendelea kujilaumu.

Jenga tabia ya kujisamehe na kuachana na historia usiyo na uwezo wa kuigeuza. Hata kama ulifanya makosa yaliyokuingiza kwenye shida kubwa, ulifanya uamuzi mbaya unaokugharimu, jipe nafasi ya kuanza upya.

Tumelelewa kuamini kuwa binadamu ni mkamilifu na hapaswi kufanya mambo fulani fulani. Unapoyafanya hayo unayoamini hupaswi kuyafanya unajiona mkosaji asiyestahili heshima. Unajidharau. Lakini tunapofanya hivyo, tunajitengenezea mazingira yanayokunyang’anya amani. Fanya kinyume.

Usikwepe makosa yako

Kusahau historia mbaya hakuhalalishi tabia ya kukana makosa yetu. Hatutaki kukubali makosa. Tunatumia nguvu nyingi kufukia makosa yetu tukifikiri kwa kufanya hivyo tutapata amani. Mara nyingi, hatupati amani hiyo. Ni sawa na mbuni anayeficha kichwa chake mchangani.

Kujaribu kujinasua na makosa yetu ni kujitengenezea mzimu kwa mikono yetu wenyewe. Jenga tabia ya kukubali na kuwajibikia makosa unayoyafanya. Kukubali makosa yako si udhaifu kama wengi wanavyofikiri. Unapokubali makosa yako, unaufanya ufahamu wako uwe huru. Hutumii nguvu nyingi hujitetea na kuficha kile unachojua hakiko sawa.

Hata katika mazingira ambayo matokeo ya makosa hayo ni mabaya, kuwa tayari kuishi kwenye ubaya huo kuliko kujilaumu kwa makosa ambayo huna namna ya kuyabadili.

Chukulia makosa yako kazini yamechangia ‘kutumbuliwa’.  Wakubwa wako wanafikiri kukuondoa kukuadhibu kwa kile ulichokifanya. Katika mazingira haya, kujilaumu kwa makosa haya, hakuwezi kukusaidia. Kutafuta mtu wa kubeba makosa yako hakuwezi kukusaidia.

Lakini utakapoamua kukabiliana na kuachishwa kazi bila kujali vile utakavyojisikia, ukafikiria namna ya kuishi nje ya kazi uliyoizoea bila kujilaumu, utajiepusha na msongo wa mawazo usio na sababu.

Kadhalika, pengine makosa yako yamemfanya mtu umpendaye asite kuendelea na wewe. Amepoteza imani na wewe kiasi cha kuamua kuvunja uhusiano wenu. Pamoja na hayo, unajua ukweli kuwa umefanya makosa hata kama hupendi matokeo yake. Huwezi kukwepa matokeo ya makosa yako kwa kujifanya kuwa hukukosea.

Pamoja na gharama kubwa unayolazimika kuilipa kwa makosa uliyoyafanya, bado unaweza kuwa na furaha. Furaha yako kwenye kipindi hiki kigumu haitategemea namna gani unajitetea na makosa unayojua umeyafanya. Hapana. Furaha yako itategemea namna unavyokuwa tayari kulipa gharama ya makosa yako kwa moyo mkunjufu. Kuwajibikia makosa yako ndio kujitambua.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles