‘Unafiki kikwazo  katika kumuenzi Nyerere’ 

0
564

Na EVANS MAGEGE-DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Bodi ya Shirika la Posta Tanzania (TPC),  Dk. Harun Kondo amesema baadhi ya wasomi na viongozi mbalimbali wameifikisha nchi sehemu mbaya katika uchumi kwa sababu ya unafiki katika  kumuenzi  Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu   Nyerere.

Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa kongamano la Kumbukizi ya miaka 19 ya Hayati Baba Taifa, Mwalimu Nyerere, lililofanyika katika Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kigamboni  Dar es Salaam.

Dk. Kondo alisema viongozi  na wasomi wamechangia sehemu kubwa ya kuua jitihada za nchi katika kupiga hatua za maendeleo kwa sababu hawataki kuzifuata falsafa za Azimio la Arusha ambalo ndiyo mtazamo madhubuti wa Mwalimu Nyerere katika kujenga uchumi wa kujitegemea kwa taifa hili.

“Kwa bahati mbaya tumekuwa na wasomi na viongozi wanafiki wa kumuenzi Baba wa Taifa, wametufikisha hapa kwa sababu ya unafiki wao.

“Namshukuru Mungu kwa kutuletea Rais Dk. John Magufuli, huyu katika imani naweza kumuita Joshua ambaye atatufikisha Canani,” alisema Dk. Kondo.

Mhadhiri  Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dk. Monranus Milanzi  alisema matamanio ya Mwalimu Nyerere juu ya Azimio la Arusha yalikuwa ni kujenga taifa la kujitegemea.

Alisema  sifa ya Baba wa Taifa siyo mwalimu tu bali ana sifa nyingine 22 ambazo zimeandikwa kwenye vitabu mbalimbali katika  mataifa mengine.

“Mwalimu alipanda na wakati wa kuvuna ni sasa  katika utawala wa Rais Dk. Magufuli,” alisema Dk. Milanzi.

Mkuu wa Idara ya Uchumi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Binto Binto alisema taifa kushindwa kuendelea kulitokana na ubinafsi si tu wa mtu mmoja mmoja bali uhusiano wa kimataifa.

Alisema hali ya ubinafsi ilikuwa chini  kati ya miaka ya 1961 hadi 81 lakini mwaka 1991 hadi 2010 hali hiyo ilipanda kwa kiwango cha juu lakini imeanza kushuka ndani ya utawala wa sasa.

Alisema tatizo jingine lililosababisha kukwama  maendeleo ni tabia ya watu waliosoma kujiona wanajua kila kitu hivyo wa hawakuhitaji kujifunza zaidi ili kuelimika.

Awali Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana  na Rushwa (TAKUKURU), Ekwabi  Mujungu, alisema hali ya Watanzania katika elimu ni kubwa  kwenye kutafuta vyeti kuliko kuelimika, hatua ambayo inasababisha kuvuja   mitihani na wengine kughushi vyeti.

Akiwasilisha   mada yake juu ya nafasi ya elimu katika kukuza viwanda vya ndani, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Dk. Charles Kitima, alisema wazazi wasibweteke na elimu bure, kwa sababu  bado wanao wajibu wa kuhakikisha watoto wao wanaelimika.

Alisema haitoshi mtoto wa shule kuwa na uhakika wa kukalia dawati shuleni na kusoma bure wakati hana vitabu vya kujisomea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here