22.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

UNACHOVUNA KWENYE MUZIKI WEKEZA KWINGINEKO

INAWEZEKANA mfano nitakaoutumia ukatatanisha kwa kulinganisha mbingu na ardhi lakini pia ni mfano ninaoweza kuumithilisha na udongo na ardhi yaani unajisadifisha kwa mashiko mahsusi yanayopaswa kwa kuwa ndivyo wasanii duniani kote wanavyofanya ili kujihakikishia kiwango cha maisha ya ‘Ustaa’ kinadumu kwa mfumo wa kuishi kama walivyokuwa wanang’ara katika zama walizotamba.

Zuwena Mohamed a.k.a Shilole amekaririwa na toleo letu la Jumatano kutamani kuwekeza kwenye biashara nyingine baada ya kufanikiwa katika biashara ya mgahawa, lakini pengine wengi hamfahamu alikotokea kwani katika biashara ya kuuza vinywaji na vyakula ndiko alikoanzia ingawa ni katika hali ya chini wakati akisota waya huko kwao Igunga Tabora.

Ndiyo maana katika ngoma yake iliyomkubalisha kwa mashabiki: ‘Nakomaa Na Jiji’ ameimba: “Wanasema nirudi Igunga maisha yamenishinda….” akipinga kurudi alikotoka kwani anakomaa na Jiji kusaka riziki, ambayo alianza kuisaka kwa taabu kwa kuja jijini baada ya kuwa amekatizwa masomo kwa kuzalishwa mtoto, akalazimika kuuza mikate na maji ya kunywa kwenye stendi ya Igunga ili kujikimu kimaisha, akakutana na dereva wa lori aliyemleta Dar kuanza maisha kitongoji cha Keko lakini alimkataza kufanya kazi wakati Shilole alitamani kujiendeleza ili awe mhudumu hotelini, akawa mtu wa kupewa vipigo kila mara na huyo mumewe.

Lakini alikomaa na kufanya kazi Hoteli ya Peackock alikokutana na Ray Kigosi aliyemsaidia kujitosa kwenye muvi, kutoka huko ndipo alikojitosa kwenye muziki anakokomaa zaidi hata kukumbuka biashara ya makulaji (mikate, sharubati na maji) akafungua mgahawa na sasa mambo yamemnogea anataka kufungua biashara nyinginezo.

Hivyo ndivyo ‘Back’ yake ilivyokuwa na hadi sasa ‘Front’ yake inakompeleka ingawa ningetamani kufanya mambo mawili kwake, kama ningepata nafasi ya kuwa mshauri wake wa uwekezaji katika biashara anazotaka kufanya.

Kwanza ningetamani kumuelezea kwa kina kwenu wasomaji mapito yake hadi kufikia alipo sasa lakini hii si safu ya historia za wasanii bali kutazama walikotoka (Back) kwa kushadadia wanakokwenda (Front), lakini pili inaelekea nyota yake inang’aa kwenye biashara za makulaji.

Kumbuka mikate na sharubati (juisi) ndizo zilimkutanisha na mtu aliyemleta jijini na kuhudumu kwenye Hoteli, ndiko kulikomkutanisha na Ray (Bongo Muvi) na kutoka hapo akachupa kwenye muziki na kufanikiwa zaidi.

Kwa hiyo ‘next level’ kama akijielekeza kwenye ‘Fast Food Parlour’ hakika atang’aa lakini yeye mwenyewe anafahamu anakotaka kuelekea kiuwekezaji. Nikikurudisha ‘Back’ kwa ninayemfananisha naye (Whitney Houston) ambaye kwa sasa hayuko duniani, mwanadada huyo wa Marekani baada ya kufanikiwa kusomba fedha kwenye tasnia ya muziki aliwekeza sana katika biashara kwa njia ya hisa.

Kuna wakati aliwekeza hadi katika hisa za kampuni ya vinywaji baridi ya Marekani katika tawi lake lililokuwa linahudumia bara la Afrika nchini Afrika Kusini. Ukiachilia mengine yaliyomsibu na kumuondoa duniani lakini ‘Front’ yake ilijikita pazuri kwa uwekezaji huo.

Kwa mfano huo Shilole anaanzaje kurudi Igunga wakati maisha hayajamshinda hapa jijini na sasa anatarajia kujikita kwenye mtambuka wa biashara tanzu!? Hivyo ndivyo kinachovunwa kwenye sanaa kinavyopaswa kutumiwa kwa kuwekeza ili baadaye nyota ya muziki itakapofifia maisha yabaki levo ile ile.

Komaa na Jiji Shishi maana baraka za kuwahudumia yatima zimekujia ingawa hufanyi kwa kujitangaza dua zao zinakufungulia milango kwani anayewiwa zaidi hupewa zaidi ili atimize dhima aliyokabidhiwa!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles