31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

UN: Maofisa wa Saudia walipanga kumuua Khashoggi

ANKARA, UTURUKI

MJUMBE maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, Agnes Callamard, amesema uchunguzi aliofanya umethibitisha mauaji ya mwandishi wa habari wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi, yalipangwa na kutekelezwa na maofisa wa Saudia.

Callamard ameitoa kauli hiyo juzi baada ya kumaliza ziara yake maalumu nchini Uturuki na anatarajia kuwasilisha ripoti yake katika Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa, Juni, mjini Geneva, Uswisi. Hata hivyo, uchunguzi wa Callamard na timu yake bado unaendelea.

Ameongeza kwa kusema Serikali ya Saudi Arabia ilihujumu juhudi za Uturuki kuchunguza mauaji ya Khashoggi, aliyeuawa Oktoba 2 mwaka jana ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia, mjini Istanbul.

Aidha, ameuita uchunguzi wake kama hatua muhimu kuelekea kwenye ukweli na uwajibikaji. Amesema ushahidi uliokusanywa unaonesha wazi kuwa Khashoggi aliuawa kikatili na maofisa wa Saudia.

Akiwa nchini Uturuki katika uchunguzi huo huru, Callamard alikutana na mwendesha mashtaka mkuu wa nchi hiyo, mkuu wa idara ya usalama pamoja na mawaziri wa mambo ya nje na sheria.

Kwa upande wa Serikali ya Uturuki, imetoa kauli kupitia Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ofisi ya Rais wa nchi hiyo, Fahrettin Altun, amesema kukosekana kwa uwazi kutoka kwa maofisa wa Saudia kunaleta wasiwasi mkubwa na kunaondoa uaminifu kwa maofisa hao.

Altun amesema viongozi wa Saudi Arabia wanapaswa kuwakabidhi nchini Uturuki wauaji wa Khashoggi, kama ushahidi wa kuonesha nia yao ya kuzingatia haki na kuongeza kuwa uchunguzi wa Uturuki katika mauaji hayo, unafanana na ule wa Umoja wa Mataifa.

Wakati huo huo, wabunge wa Marekani wametishia kuchukua hatua kali dhidi ya Saudi Arabia kuhusu mauaji ya Khashoggi, kutokana na taarifa mpya zinazoeleza kuwa mrithi wa kiti cha mfalme wa Saudia, Mohammed bin Salman, aliwahi kusema kuwa atatumia ‘risasi’ dhidi ya Khashoggi, kama hatarejea nyumbani na kuachana na ukosoaji wake kwa Serikali.

Taarifa hiyo imeripotiwa juzi kwenye gazeti la New York Times na kwamba, Bin Salman aliyatoa matamshi hayo mwaka 2017 wakati akizungumza na msaidizi wake.

Gazeti hilo limezinukuu duru kutoka kwa maofisa wa sasa na wa zamani wa Marekani na wale wa mambo ya kigeni ambao wanajua kuhusu taarifa hizo za kijasusi.

Rais wa Marekani, Donald Trump, jana alitarajia kukabiliwa na kizingiti hicho, ikiwa ni siku ya mwisho aliyopewa na Bunge la Marekani kueleza kama Bin Salman aliamuru mauaji ya Khashoggi.

Kamati ya Bunge ya Uhusiano wa Kigeni, iliipa Serikali ya Trump siku 120 kuanzia Oktoba mwaka jana hadi Februari 8 mwaka huu, kueleza iwapo mwanamfalme huyo aliamuru mauaji ya Khashoggi na kumtaka achukue hatua dhidi yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles