25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

UMUHIMU WA KUMFANYIA UCHUNGUZI MAREHEMU NDANI YA SAA 24

Na VERONICA ROMWALD- DAR ES SALAAM


HUDUMA za matibabu nchini zinazidi kukua na kuimarika. Kila kukicha tunashuhudia namna ambavyo serikali inajidhatiti kuboresha huduma katika hospitali zake, kadhalika hospitali binafsi nazo zinazidi kufunguliwa.

Lengo ni kuhakikisha watu wanapata huduma bora za matibabu dhidi ya magonjwa mbalimbali ili wawe na afya njema na waweze kuendelea kujenga uchumi wao binafsi, familia na Taifa kwa ujumla.

Wataalamu wa afya wanajitahidi kuhakikisha wanatoa huduma za matibabu zinazokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Lakini wapo wachache ambao wamekuwa wakilalamikiwa kufanya mambo yasiyoendana na maadili ya kazi zao,
wakilalamikiwa kutoa kauli za kuudhi kwa wagonjwa na wakati mwingine matibabu yasiyo sahihi.

MTANZANIA limezungumza na Wakili wa Mahakama Kuu Tanzania, Maulid Kikondo ambaye anafafanua kwa kina katika makala haya baadhi ya makosa yanayofanywa na wataalamu wa afya ambayo kwa namna moja au nyingine husababisha madhara kwa mgonjwa.

“Wataalamu wa afya kwa asilimia kubwa wanajitahidi kutoa huduma bora za matibabu, lakini kama unavyojua ingawa wapo ambao wanazingatia maadili na weledi katika kazi wapo ambao hukiuka,” anasema.

Anatoa mfano: “Wakati mwingine madhara hutokea kutokana na mazoea mabaya yaliyojengeka kwenye jamii, kwa mfano; mtu anaridhika kuwa na daktari mmoja anayemuhudumia kila wakati anapokuwa anaugua, ni makosa makubwa katika suala la matibabu.

“Ni vizuri kuwa na daktari binafsi ambaye anakuhudumia lakini unapaswa pia kuwa na daktari mwingine ambaye atakuwa mshauri wako kama ambavyo watu wengi mashuhuri hufanya,” anasema.

Kwanini?
“Kwa mfano mgonjwa anakwenda hospitalini anafanyiwa kipimo na kuambiwa haumwi, lakini kumbe ana saratani ipo hatua za awali na daktari hajamfanyia uchunguzi wa kina, anarudi nyumbani akiamini ni mzima.
“Kadiri anavyokaa nyumbani anazidi kuumwa, anaporudi hospitalini anakuta ugonjwa umesambaa kiasi kikubwa, daktari anakuwa amemsababishia madhara… lakini kwa sababu alimuamini anaweza kumtibu
pekee anakuwa amechelewa.

“Mgonjwa wa aina hii angekuwa na daktari mshauri, kwa namna yoyote ile angeweza kuzungumza naye na angemshauri jinsi ya kufanya na pengine angegundulika mapema na kusaidiwa, kabla hajapata madhara
makubwa.

“Au unakuta daktari anaenda kufanya upasuaji akiwa hajaongozana na daktari wa usingizi hasa huko kwenye maeneo ya pembezoni matokeo yake mgonjwa anapata madhara kutokana na uzembe huo,” anasema.
Wakili huyo ambaye amebobea katika upande wa Sheria ya Matibabu anasema wakati mwingine unakuta mgonjwa alihitaji kufanyiwa upasuaji mdogo lakini anafanyiwa upasuaji mkubwa kutibu ugonjwa wake hali
inayoweza kumsababishia madhara.

“Kwa mfano, msichana anakuja anatakiwa kufanyiwa upasuaji mdogo tu kutibu tatizo linalomsumbua lakini wakati wa upasuaji daktari akaenda hadi kugusa kizazi chake na kusababisha kuondolewa, mgonjwa huyo ana
haki ya kushtaki ili apate haki yake,” anasema.

Anaongeza: “Au wakati mwingine unakuta daktari anasahau vitu mbalimbali tumboni mwa mgonjwa kwa mfano gozi, mkasi na vinginevyo ule ni uzembe mkubwa mno ambao ungeweza kuepukika, mgonjwa huishi kwa maumivu
makali.
“Au unakuta mjamzito anaambiwa na daktari mimba yake imeharibika na mtoto amefia tumboni lakini anapofanyiwa upasuaji kumbe mtoto mzima, ana haki ya kushtaki mahakamani.”

Anasema hata hivyo si watu wote ambao wanajua kuwa hilo linawezekana kutokana na elimu duni kuhusu Sheria ya Matibabu ambayo inampa mgonjwa haki ya kumshtaki mahakamani daktari aliyemsababishia madhara.

Ni kesi ngumu
Wakili huyo anasema kesi hizo kwa kawaida huwa si rahisi kuziendesha hasa iwapo mwanasheria au wakili anayeisimamia hana uelewa wa kutosha kuhusu Sheria ya Matibabu.
“Mawakili na wanasheria wengi hawajajikita upande huu wa matibabu sasa ili aweze kusimamia vema kesi za namna hii lazima wakili au mwanasheria awe ana ule uwelewa wa masuala ya kimatibabu.

“Kwa sababu mara nyingi madaktari ndio ambao huja kutoa ushahidi sasa lazima ujue zile ‘terminologies’ ambazo huwa wanazitumia katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku, vinginevyo hata kama mgonjwa ana
haki anaweza kujikuta anashindwa kesi,” anasema.

Mazoea hujenga tabia
Wakili Kikondo anasema mara nyingi mazoea yanayojengeka kwa baadhi ya wataalamu wa afya, kujiamini kwamba wanaweza kufanya kila kitu husababisha madhara kwa wagonjwa.
“Kwa mfano; daktari amebobea katika upasuaji kutibu magonjwa ya wanawake anakwenda kutoa huduma hiyo pasipo kuongozana na daktari wa usingizi ambaye kimsingi anapaswa kuwapo katika chumba cha upasuaji,”
anafafanua.

Wakili huyo anasisitiza: “Kila mtaalamu ana umuhimu wake katika kusimamia upasuaji wa mgonjwa, kwa uzembe wa aina hiyo matokeo yake unakuta yanatokea madhara kwa sababu upasuaji haukuzingatia taratibu
zinazotakiwa.

Daktari rafiki muhimu
“Makosa makubwa ambayo Watanzania wengi tunafanya ni kuwa na daktari mmoja ambaye tunamuamini kwa matibabu yetu, si kosa lakini ni vizuri kuwa na daktari rafiki ambaye atakuwa anakushauri katika mambo fulani
fulani ya kimatibabu,” anasema.
Anaongeza: “Ni mfumo ambao viongozi wengi wanautumia, ingawa ana daktari anayemuhudumia lakini yupo daktari mwingine ambaye huwa anamtumia kwa kumpatia ushauri wa kidaktari, hata inapotokea daktari anayemtibu amekosea huyu mshauri humsaidia na hivyo kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.

Uchunguzi wa marehemu
Anasema inafahamika wazi kwamba kulingana na imani mbalimbali za kidini, inaaminika kila mwanadamu kama ambavyo alizaliwa ipo siku atakufa na kurejea kwa muumba wake.
Anasema kwa kawaida binadamu anapofariki mwili wake huhifadhiwa kwa kufanyiwa maziko maalumu kulingana na imani ya muhusika.

“Kimsingi hakuna anayejua siku yake ya kufa, hiyo ni siri kubwa na ya kipekee ambayo Mwenyezi Mungu pekee ndiye ajuaye siku ya kufa ya kila mmoja.
“Ni kwa mantiki hiyo kila mmoja hufa kwa mtindo wake, wapo ambao huugua maradhi mbalimbali, wengine hufariki ghafla wakiwa usingizi, wapo wanaopata ajali na kadhalika.

“Pamoja na hayo, mwili wa marehemu nao una haki zake, unastahili kupatiwa haki hizo kwa sababu ni binadamu ingawa hawezi kuishi tena kama wale walio hai katika ulimwengu huu,” anasema.

Anasema ili kulinda haki za marehemu, Sheria ya Matibabu huelekeza mambo muhimu ikiwamo ulazima wa kuuchunguza kujua ukweli wa kile kilichosababisha kifo cha muhusika.

“Hiyo huwa haijalishi kwamba amepata ajali au ameugua ghafla, lazima ijulikane kwa undani kile kilichosababisha kifo chake achilia mbali matukio hayo yanayoweza kuonekana au kusekemekana kwa nje,”
anabainisha.

Wakili Kikondo anasema kosa kubwa ambalo watu wengi huwa wanafanya hasa inapotokea mtu amefariki ghafla ni kutaka kuwahi kufanya maziko.

“Kuna umuhimu mkubwa mno wa kuruhusu marehemu achunguzwe, inakuwa ngumu kushinda kesi unapomshitaki daktari ikiwa hamkufanya uchunguzi kujua kilichosababisha kifo cha marehemu kama ambavyo sheria ya matibabu inavyoeleza.

“Wengi wanakwepa lakini ili uweze kumshinda daktari uchunguzi ni muhimu, ni wakati pekee unaweza kubaini nini kimesababisha kifo cha marehemu na huchukua muda mfupi tu,” anabainisha.

Kifo saa 24
Wakili huyo anasema kisheria ni jambo linalohitaji uchunguzi wa kina inapotokea mgonjwa kufariki dunia ndani ya saa 24 tangu alipofikishwa hospitalini jambo ambalo wengi hawajui.

“Inapotokea hali hiyo ni lazima uchunguzi ufanyike, nini kimetokea hadi mgonjwa afariki. Pia inapotokea mgonjwa amefia kwenye meza ya upasuaji wakati wa upasuaji wenyewe, madaktari wanaita kitaalamu ‘death on table (DOT)’ yaani mgonjwa anakuwa amekufa kitandani akifanyiwa upasuaji,” anabainisha.

Anaongeza: “Kwa kuwa watu wengi hawajui kwamba kisheria hilo linahitaji uchunguzi wa kina, basi huwa hawajishughulishi kutaka kujua nini ambacho kimesababisha kifo cha marehemu.

“Ingawa hatuwezi kuzuia kifo, lakini kinapotokea lazima tujiulize nini kimesababisha si kuchukulia kila kifo kwamba kimepangwa na Mwenyezi Mungu, ikiwa marehemu amefariki kwa mfano kwa kulishwa sumu tutayajua
hayo baada ya uchunguzi, kifo chochote kile ni muhimu kufanya uchunguzi,” anasisitiza.

Changamoto
Anasema wakati mwingine huwa kuna shinikizo kutoka kwa ndugu wa marehemu kutaka ndugu yao azikwe mapema ingawa askari wa Jeshi la Polisi hufanya kazi nzuri kuhakikisha marehemu anafanyiwa vipimo,
jamii inapaswa sasa kutambua umuhimu wa suala hilo.

Wakili Kikondo anasema kosa jingine ambalo ndugu wa marehemu hufanya ni kuondoka na mwili wa marehemu kwenda kuuzika pasipo kusubiri taarifa ya daktari.

“Hakikisheni mmechukua pia taarifa ya uchunguzi wa mwili wa ndugu yenu, ingawa ipo pia changamoto kwa baadhi ya ndugu kuogopa kuingia ndani wakati daktari akimfanyia uchunguzi ndugu yao kujua nini ambacho
kimesababisha kifo chake,” anasema.

Anasema kutokana na hali hiyo, ikiwa kifo hicho kimetokana na uzembe wa daktari, basi daktari husika anaweza kutumia mwanya huo kwa kushirikiana na wenzake wasio waaminifu kutengeneza taarifa ya uwongo
kuhusu kifo cha marehemu.
“Ni muhimu ndugu wa marehemu kuhudhuria kipindi cha ‘postmortem’ ili kupata uthibitisho wa kile kilichosababisha kifo cha ndugu yao.

“Nimeshuhudia wengi wanapokuja kuchukua mwili wa marehemu huwa wanahangaika kutafuta tu barua ya kibali cha maziko lakini wanasahau kwamba taarifa ya uchunguzi ni muhimu pia,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles