31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Umri watoto kupata huduma za VVU bila ridhaa ya wazazi kupunguzwa

NA MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

SERIKALI inatarajia kupeleka bungeni muswada wa sheria wa kushusha umri wa kuridhia vijana kupata huduma za Ukimwi bila ridhaa ya wazazi kutoka miaka 18 hadi 15 ili kupunguza wimbi la maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), hususani kwa vijana.

Hatua hiyo imekuja baada ya Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), kubainisha kuwa kwa siku zaidi ya watu 200 hupata maambukizi mapya ya VVU, huku kati yao 80 wakiwa ni vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24.

Hayo yalibainishwa Dar es Salaam juzi na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile wakati akizindua upandaji wa Mlima Kilimanjaro (Kilimanjaro Challenge 2019), na kuendesha harambee ya kuchangisha fedha kwa mwaka 2019 kwa ajili ya afua za Ukimwi nchini.

Kilimanjaro Challenge ni mfuko muhimu unaoratibiwa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na Tacaids kwa kushirikisha taasisi za nje na ndani ya nchi katika kuendeleza mapambano dhidi ya VVU/ Ukimwi.

Alisema tatizo la ugonjwa wa Ukimwi linabadilika kila mara hivyo kuchangia zaidi ya asilimia 40 ya vijana kuathiriwa huku asilimia 80 ya vijana hao wakiwa ni vijana wa kike.

“Serikali tumeanza kuliona hilo na kuchukua hatua, hatua ya kwanza ni kushusha umri wa kuridhia kwani ni kweli vijana wanaanza kujamiiana wakiwa umri wadogo, takwimu zinaonesha kuanzia  wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 19, asilimia 27 ni wajawazito au wana watoto.

“Kwa hali hii ya maambukizi tumeamua kupeleka muswada bungeni kushusha umri wa ridhaa hadi miaka 15. Ili sasa iweze kuruhusu kijana kuweza kupata huduma, kwa sababu kwa sasa inabidi apate ridhaa ya mzazi au mlezi,” alisema Dk. Ndugulile.

Aidha, alisema wizara hiyo italeta mpango wa kuruhusu watu kujipima wenyewe ili kutoa motisha kwa akina baba kupima VVU.

“Kama ilivyo kwa wanawake wanavyojipima ujauzito na kina baba watahamasika kujipima na naamini litawapa motisha,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, Dk. Leonard Maboko alisema muswada huo ukipitishwa na kuwa sheria utasaidia vijana kupata huduma za Ukimwi kwa haraka bila ridhaa ya mzazi au mlezi kama ilivyo sasa.

Alisema hadi sasa Tanzania inao watu milioni 1.5 wenye VVU ambao ni sawa na asilimia 4.7.
“Lakini maambukizo mapya yamepungua kutoka 80,000 miaka mine iliyopita hadi 72,000.

“Katika kundi hili Watanzania 6000 wanapata maambukizo mpaya kwa mwezi na kwa siku ni 200,” alisema.
Aidha, alisema sababu za vijana kupata maambukizo zaidi ni kutoka kwenye utoto kwenda kwenye ujana.
“Hawajapata elimu sawasawa hivyo inakuwa rahisi kwake kufanya maamuzi ambayo hana taarifa za kutosha. Lakini pia vijana wa kike kutaka kupata vitu kwa haraka.
“Ndiyo maana tuna miradi ambayo inagusa kaya maskini kwa kuwasaidia kupata elimu ya ujasiriamali katika mikoa mitatu,” alisema.
Kutokana na tatizo hilo Makamu wa Rais miradi endelevu wa Kampuni ya AngloGold Ashanti, GGM, Simon Shayo alisema kwa mwaka huu katika kampeni hiyo ya kuchangia afua za Ukimwi wamelenga kukusanya Sh bilioni mbili.
Hata hivyo, alisema hadi sasa tayari wamekusanya zaidi ya Sh bilioni 1.5 sawa na asilimia 67 ya lengo la kampeni hiyo ya mwaka huu ambayo sasa inatimiza miaka 17 tangu kuanzishwa kwake.

Alisema tangu kuanzishwa kwa Kilimanjaro Challenge, zimekusanywa zaidi ya Sh bilioni 13 ambazo zimenufaisha asasi na taasisi mbalimbali 50 zinazoshughulikia masuala ya Ukimwi.
“Lengo kuhakikisha maambukizi mapya yanatokomea na kufikia lile lengo la sifuri tatu,” alisema.
Alisema tangu kampeni hiyo ianzishwe watu zaidi ya 800 wamepanda Mlima Kilimanjaro, na mwaka huu wanategemea zaidi ya  watu 80 wakiwamo waendesha baiskeli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles