30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Ummy Mwalimu- Mfumo huduma za dharura nchini si mzuri

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

HUU ni mfululizo wa ripoti maalumu kuhusu mfumo wa utoaji huduma kwa wagonjwa hasa majeruhi nchini.

Wiki iliyopita Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura Muhimbili, Upendo George alieleza namna huduma hizo zinavyopaswa kutolewa.

Pia mwandishi alizungumza na Profesa Mohamed Janabi ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.

 

Waziri atoa neno

MTANZANIA lilifika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kujua namna gani wamejiandaa kukabiliana na changamoto hiyo.

Katika mahojiano maalum, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anakiri kwamba mfumo wa utoaji huduma za dharura nchini kiujumla si mzuri.
“Hali inaonesha hatupo vizuri, wataalamu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) walifanya tathmini ambayo inaonesha wazi kuwa hali si nzuri,” anasema.

Anaongeza “Tunazungumzia suala la kuhudumia wagonjwa wa dharura hasa majeruhi, utakuta vituo vyetu vya kutolea huduma na hospitali zilizopo maeneo ya barabarani (njiani) hazina miundombinu ya kutosha kuweza kutoa huduma hiyo.

“Vituo na hospitali zetu hazina vifaa vya kutosha kutoa huduma hii lakini pia hazina ‘ambulance’ za kuweza kutoa huduma, ingawa kwa kwa jiji la Dar es Salaam kuna changamoto ya msongamano wa magari katika kumsafirisha mgonjwa kuwahishwa hospitalini.”

Waziri Ummy anasema tathmini iliyofanywa na wataalamu wa Muhimbili inaonesha kutokana na changamoto hizo, wapo wagonjwa ambao hufariki katika geti (mlango) la hospitali.
“Yaani mgonjwa anakuwa amesaidiwa kuanzia huko alipotoka na kuwahishwa hospitalini lakini kabla hajaanza kupatiwa huduma anapoteza maisha, kwa sababu hakuna huduma nzuri ya dharura, hii ni changamoto.
“Kimsingi mgonjwa yeyote wa dharura anaweza kurudishiwa uhai ikiwa mnakuwa na huduma nzuri za dharura, nasema bila kificho kwamba hali si nzuri,” anasisitiza.

Tunatokaje tulipo?
Waziri Ummy anasema hivi sasa serikali inakamilisha mazungumzo na Benki ya Dunia (WB) ambapo inategemea kupatiwa fedha ambazo zitatumika kujenga uwezo wa kutoa huduma za dharura kwa majeruhi wa ajali.

“Tumeainisha kwanza tutanunua ‘ambulance’, vile vile tunakusudia pia kununua helkopta ya kutoa huduma za dharura lengo letu ni kuimarisha mfumo wa utoaji huduma za dharura nchini,” anasema.

Anasema katika njia kuu kuelekea nchini Zambia kuanzia Kibaha mkoani Pwani, Morogoro, Mbeya hadi Tunduma, kuna vituo vya afya vilivyoainishwa ambavyo tutavijengea uwezo ikiwamo kuweka miundombinu, vifaa na wataalamu watakaotoa huduma ya dharura kwa wagonjwa hasa majeruhi.


“Wizara baada ya kupokea hospitali za rufaa za mikoa, kati ya maeneo matatu ambayo tunaanza nayo ni kuziboresha, tunataka kuhakikisha katika kila hospitali ya rufaa ya mkoa tunajenga jengo maalumu la kutolea huduma ya wagonjwa wa dharura.

“Katika kutekeleza hilo, tunawatumia wataalamu wa Muhimbili kwani wao ndiyo waliofanya tathmini na kutuambia kipi kinastahili kuwekwa wapi,” anasema Waziri Ummy.
Anasema pamoja na hayo, wametoa pia maelekezo katika hospitali zote za wilaya kuhakikisha wanaimarisha mfumo wa huduma za dharura, sambamba na hilo, eneo jingine wanalotaka kuliboresha ni huduma za afya ya uzazi.

Kuhusu sheria
MTANZANIA
lilihoji iwapo Serikali ina mpango wa kutunga Sheria ya kumlinda Msamaria Mwema (Good Samaritan Law) kwani kumekuwapo malalamiko ya muda mrefu kwa wanasheria kwamba kuna upungufu.
“Niwe muwazi sijapitia hilo, lakini watuletee ushauri wao tutaliangalia na tutalifanyia kazi, tupo tayari kuandaa muswada na kuwasilisha bungeni,” anasema Ummy.

Mark Buberwa ni Mwanasheria katika Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) anasema miongoni mwa mambo ambayo wanasheria wanayapigania ni kuhakikisha sheria hiyo inapatikana.

“Hatuna sheria tunapigania kuipata kwa sababu watu wengi wanaogopa kusaidia wengine barabarani kwa kuhofia kuingia kwenye matatizo, hakuna sheria inayomlinda msamaria mwema.

Itaendelea…

Mwandishi wa makala haya ni miongoni mwa waandishi waliochaguliwa kushiriki mafunzo ya uandishi wa habari za usalama barabarani yanayotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kushirikiana na Wizara  ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kupitia mradi wa Bloomberg (BIGRS).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles