25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

UMEME BEI JUU

muhongo

*Ewura yatangazakupandakwa asilimia 8.5

*Profesa Muhongo asema hana taarifa

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

SIKU moja kabla ya mwaka mpya wa 2017 kuanza, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imeridhia ongezeko la bei ya umeme kwa wastani wa asilimia 8.5.

Ewura imepitisha ongezeko hilo linalotajwa kuwa litawaumiza watumiaji wa umeme baada ya kuyafanyia uchambuzi wa kina maombi yaliyowasilishwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Ewura, Felix Ngamlamgosi, alisema katika maombi ya awali yaliyowasilishwa Oktoba 4, mwaka huu, Tanesco ilipendekeza gharama za umeme ziongezeke kwa kiwango cha asilimia 18.19 jambo lililokataliwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Ewura.

“Itakumbukwa kwamba Aprili, mwaka huu baada ya uchambuzi tuliofanya tuliitaka Tanesco kupunguza gharama za umeme na kweli ilishuka kwa asilimia 1.1 na Watanzania tulinufaika na punguzo lile.

“Baada ya uchambuzi ule Oktoba 4, mwaka huu, Tanesco iliwasilisha andiko lingine ambapo iliomba ongezeko la bei kutoka shilingi 242.20 hadi shilingi 286.28 kwa kila uniti moja ya umeme, ongezeko hilo ni kiasi cha asilimia 18.19,” alisema.

Ngamlamgosi alisema ombi hilo liliambatana na ombi lingine ikiwamo kuvunja kundi la T1 ambalo ni la wateja wa nyumbani linalojumuisha biashara ndogo ndogo, maduka madogo madogo, mashine za kusaga, taa za barabarani na minara ya simu.

“Kwamba kuwe na kundi moja la wateja wa nyumbani hasa katika nyumba zetu, biashara ndogo ndogo na bei ya taa za barabarani. Hili ombi la kundi la T1B, lihusishe viwanda vidogo vidogo na minara ya simu ombi hili lina mantiki,” alisema.

Pia alisema baada ya kupokea andiko hilo walitoa wito kwa wadau kutoa maoni na kwamba walipokea maoni kutoka kwa wananchi 150 kwa mdomo na zaidi ya maoni 35 yaliwasilishwa kwa maandishi.

“Makundi mengi yalitaka Tanesco iboreshe utendaji kazi wake, idhibiti upotevu wa umeme yaani iwadhibiti vishoka na miundombinu yake lakini pia iboreshe huduma kwa wateja wake na iangalie upya gharama zake hasa katika uzalishaji, usafirishaji wa umeme na Ewura ichunguze kwa kina uhalali wa gharama ambazo imeziwasilisha, wengi walisema ongezeko hilo ni kubwa linaweza kuleta madhara kwa uchumi kwa ujumla na wananchi mmoja mmoja,” alisema.

Ngamlamgosi aliendelea kusema kuwa Tanesco ilikuwa inaomba kukusanya Sh trilioni 1.9 kwa kiwango kile cha asilimia 18.19, lakini walibaini gharama halali za kwenda kwa mtumiaji ni Sh trilioni 1.6

“Hivyo ni gharama ambayo haikwepeki iwapo tunataka Tanesco itoe huduma kama tunavyotaka. Bei itaongezeka kwa asilimia 8.5 na si asilimia 18.19 kama ilivyopendekeza Tanesco na sababu kuu ni uchambuzi wa bei,” alisema.

 SABABU ZA ONGEZEKO

Alisema Ewura imeridhia ongezeko hilo kwa sababu Tanesco ilitoa mapendekezo kadhaa hasa ya kuboresha miundombinu yake.

“Hivyo tukaona pendekezo hilo ni zuri kwa sababu limelenga kupunguza malalamiko ya wananchi kuhusu ubora wa umeme unaotolewa na Tanesco, tumepitisha gharama ya shilingi bilioni 90 iliyopo katika miradi mitatu.

“Kundi moja la mradi linahusu upanuzi wa mtandao ili kupata wateja wengi zaidi, hapa wanatarajia kutumia si chini ya shilingi bilioni 40. Kuna miradi mipya ya kupanua msongo wa umeme katika maeneo ambayo haukufanyika.

“Tanesco inalenga pia kuboresha na kuimarisha mtandao labda mahali ambapo transfoma imeungua ibadilishe na pia inatarajia kuendelea kuboresha mitandao yake, wametenga tena fedha ili waendelee kuboresha, hivyo wamelenga kuboresha upatikanaji na kuboresha huduma uje umeme wa uhakika, tumeruhusu fedha hizo ziingie katika gharama ili wapate uwezo wa kufanya hayo,” alisema.

MAKUNDI YATAKAYOATHIRIKA

Ngamlamgosi alisema kundi la T1A ambalo linajumuisha wateja wa nyumbani, biashara ndogondogo za nyumbani na taa za barabarani, Tanesco ilipendekeza ongezeko la kutoka Sh 292 hadi Sh 338 sawa na asilimia 15.8.

“Uamuzi uliotolewa hautaongezeka kwa asilimia 15.8 bali asilimia saba, hivyo kutakuwa na ongezeko la shilingi 312 katika kila uniti ya umeme watakayotumia,” alisema.

Pia alisema kundi lingine litakaloathirika na ongezeko hilo ni la TB1 ambalo linajumuisha viwanda vidogovidogo, minara ya simu na mabango ya matangazo na Tanesco iliomba nyongeza ya asilimia 16.4.

“Baada ya uchambuzi, Ewura imepitisha asilimia 8.4 kwa kundi hili la TB1, hivyo katika kila uniti moja kutakuwa na ongezeko la shilingi 317,” alisema na kuongeza:

“Kundi lingine ni la T2 linalojumuisha matumizi ya kawaida ambao wanatumia hadi volti 400, kundi hili linajumuisha wamiliki wa hoteli na biashara nyinginezo kubwa kubwa.

“Tanesco iliomba bei iongezeke kwa asilimia 19 lakini baada ya Ewura kupitia mapendekezo hayo imeridhia ongezeko la asilimia 8.8 tu na kutakuwa na ongezeko la shilingi 213 katika kila uniti moja.”

Alisema kundi lingine litakaloathirika na ongezeko hilo ni la T3 linalojumuisha watumiaji waliounganishwa katika msongo wa kati (medium voltage).

“Hawa ni wale wa viwanda vya kati, ombi la Tanesco walitaka bei ya umeme iongezeke kwa asilimia 19.1 lakini baada ya uchambuzi tumejiridhisha kwamba wanastahili ongezeko la asilimia 8.3, kwa hiyo kutakuwa na ongezeko la shilingi 170 kwa kila uniti,” alisema.

Ngamlamgosi alisema kundi la T3 linalojumuisha watumiaji wakubwa waliounganishwa na msongo mkubwa wa umeme (high voltage) kwa mfano Mgodi wa Bulyanhulu na Kiwanda cha Saruji cha Twiga.

“Ombi la Tanesco ilikuwa ongezeko la asilimia 19.1, hata hivyo Ewura imepitisha ongezeko la asilimia 7.5, hivyo kutakuwa na ongezeko la shilingi 164 katika kila uniti moja ya umeme.

“Kwa muda mrefu pia kumekuwa na malalamiko kutoka kwa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), huyu ni mnunuzi wa jumla anayenunua umeme na kuuza visiwani Zanzibar, alikuwa analalamika kwamba ingawa ananunua umeme katika msongo mkubwa lakini atenganishwe na viwanda na migodi.

“Tumeona ni sawa pamoja na kwamba Tanesco iliomba kuwe na ongezeko la asilimia 19.1 lakini Ewura imeona anastahili ongezeko la asilimia 5.7 na ameundiwa kundi lake maalumu, katika kila uniti moja ya umeme kutakuwa na ongezeko la shilingi 161,” alisema.

VIJIJINI WAPATA AHUENI

Katika kundi la D1 linalojumuisha wananchi wa kipato cha chini hasa wale wa vijijini ambao matumizi yao ni madogo na hayazidi uniti 75 kwa mwezi, alisema Tanesco iliomba iongeze gharama kutoka Sh 100 kwa uniti moja hadi Sh 105 sawa na asilimia tano.

“Lakini kwa hawa wanaotumia chini ya uniti 75, Ewura imekataa ongezeko lililopendekezwa la asilimia 8.5 na hawataguswa kabisa,” alisema.

AGIZO KWA TANESCO

Alisema pamoja na Ewura kuridhia ongezeko hilo, bodi imeitaka pia Tanesco kuhakikisha inawaunganisha moja kwa moja katika kundi la D1 wateja wanaostahili kuwa katika kundi hilo.

“Waboreshe huduma zao, mteja kama anastahili kuwekwa katika kundi la D1 basi awekwe pale anapojiunga na huduma lakini si wamuweke katika kundi lingine halafu baadaye waje kumtoa,” alionya.

 WAZIRI MUHONGO

Ongezeko hilo limetangazwa licha ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kuwahi kunukuliwa mara kadhaa siku za nyuma akisisitiza kwamba gharama za umeme hazitapanda na zitaendelea kuwa nafuu.

Profesa Muhongo alitoa msimamo huo kutokana na uwepo wa nishati nyingine hasa mafuta na gesi. Baada ya Ewura kutangaza ongezeko la bei ya umeme, MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta Profesa Muhongo ili kupata kauli ya Serikali.

Hata hivyo, baada ya kupokea simu yake ya mkononi na kuelezewa jambo hilo, Profesa Muhongo, alisema kwamba bado hajapokea taarifa hiyo.

“Mimi sina taarifa, sina taarifa hiyo,” alisema na kukata simu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles