25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Ulimwengu: ataka Kikwete ashtakiwe

Jakaya Kikwete
Jakaya Kikwete

* Asema ni kwa kuisababishia hasara Serikali pamoja na mawaziri wake

* Kinana awataka watawala kuwanyenyekea, kuwasikiliza wanaowaongoza

JONAS MUSHI NA ELIZABETH HOMBO, DAR ES SALAAM

MWANAHABARI mkongwe na mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, Jenerali Ulimwengu, amesema Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ashtakiwe kama viongozi wengine kwa kuisababishia hasara Serikali.

Mbali na Kikwete, pia ametaka washtakiwe na mawaziri waliohusika pamoja naye katika mchakato wa Katiba Mpya.

Wakati wa mchakato huo, Wizara ya Sheria na Katiba iliongozwa na mawaziri wawili kwa vipindi tofauti ambao ni marehemu Selina Kombani na Dk. Asha-rose Migiro, ambaye kwa sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza.

Mchambuzi huyo alisema kuwa Rais mstaafu Kikwete akiwa madarakani, fedha nyingi zilitumika kwenye mchakato wa kuunda Katiba Mpya ambayo haikupatikana.

Kauli hiyo aliitoa jana alipokuwa akichangia kwenye Tamasha la Nane la Kigoda cha Mwalimu Nyerere lililofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambako mzungumzaji mkuu alikuwa Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

Ulimwengu alisema iwapo mawaziri wa zamani wamechukuliwa hatua na kufikishwa mahakamani kwa kuisababishia hasara Serikali, hivyo na Kikwete apelekwe huko.

“Mchakato ule wa Katiba ulichukua fedha nyingi za wananchi na ukaishia barabarani, wakati mwingine mwiteni Kikwete kwenye mijadala kama hii mwaka ujao ajieleze kwamba fedha za wananchi zilikuwa zina sababu gani za kutumika halafu mchakato ukaishia barabarani.

“Iwapo mawaziri wa zamani wamechukuliwa hatua na wakafikishwa mahakamani kwa kuisababishia hasara Serikali, Kikwete naye apelekwe mahakamani kujibu mashtaka ya kusababisha hasara kubwa na kuzima matumaini ya wananchi, huku akiwaacha wanarandaranda barabarani hawajui wanaelekea wapi,” alisema Ulimwengu huku ukumbi ukilipuka kwa makofi.

Akizungumzia hali ya demokrasia, alisema pamoja na hatua zote nzuri anazozichukua Rais wa sasa, Dk. John Magufuli, lakini taifa limerudi nyuma kama miaka 50 kwa masuala ya kidemokrasia.

Ulimwengu ambaye wakati wote alikuwa akishangiliwa na waliohudhuria tamasha hilo, alisema juhudi hizo za Rais Magufuli hazionekani kwa sababu amefinya uhuru wa kujieleza, hususani kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Pamoja na hatua zote nzuri anazochukua Rais Magufuli, lakini ukiangalia picha kubwa tumerudi nyuma kama miaka 50 kwa masuala ya kidemokrasia kwa kufinya uhuru wa kujieleza, hususani kwa kufinya uhuru wa wawakilishi ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano,” alisema Ulimwengu.

Kutokana na hilo, alisema hakuna fimbo ya uchawi ya kujikwamua na hayo yote isipokuwa moja ambayo ni Katiba Mpya.

Pamoja na mambo mengine, katika kile kilichoonekana akimlenga Mkapa, Ulimwengu alisema ni kwa bahati mbaya amebaini kwamba viongozi wanakuwa na busara baada ya kustaafu.

“Na si hapa nchini tu, mwezi Januari nilikuwa AddisAbaba wakati mheshimiwa Mkapa na marais wengine wastaafu walipokuwa wamekusanyika pale kama kamati ya viongozi wastaafu ambao busara zao sasa zinakusanywa ili zisaidie maendeleo ya Bara la Afrika. Pale alikuwepo Chisano, Moghae.

“Nikamwuliza mmoja wa waandalizi wa mkutano huo kwamba marais wenyewe mliowakusanya hapa, mlifanya tathimini kwa kiasi gani kuhusu kazi zao walizofanya nyumbani kwao kipindi chote walipokuwa viongozi, mkaona mafanikio yao ndipo mkawaleta hapa wachangie kuleta busara zao ili kuendeleza Bara la Afrika?

“Huyo mwandalizi akanijibu kwamba sifa yao kubwa ni kwa kuwa walikaa madarakani na muda wao ulipofika wakaondoka. Hakuna sifa nyingine ndiyo maana Yoweri Museveni hawezi kuitwa hapa kwa sababu muda wake bado,” alisema.

Katika muktadha huo, alisema ili kiongozi aweze kuwa na busara wakati na baada ya kutoka madarakani, anapaswa kuwasikiliza wale anaowaongoza.

“Njia moja ya kuwapa ni mwongozo ambao ni ‘impersonal’ na si wa kwako, ila ni wao wenyewe pamoja na wewe mwenyewe namna ya kuendeleza nchi yao na moja ambayo ni kubwa sana ni Katiba.

“Lakini naona Katiba imekwama na imekwamishwa kwa makusudi kabisa kwa sababu wewe Mkapa ni msomi kuna wakuu wa nchi  ambao ni ‘Law givers’ kwa kuwapa wigo wananchi wa kujieleza na kutenda, lakini hapa kwetu tumeshindwa kuwapata viongozi wa namna hiyo.

“Julius Nyerere sidhani kama angekuwa mkamilifu kama asingechukua msimamo wa mwaka 1991-1995 tulipopata Bunge la kwanza la vyama vingi, CCM hawakupenda baada ya kuwaambia kwamba siasa ya vyama vingi haiepukiki.

“Mimi nilikuwepo Diamond Jubilee siku hiyo, wakati Mwalimu Nyerere anazungumza CCM hawakupenda, walishangilia pale tu aliposema mtoto akichezea wembe umpe umkate… akichezea moto umpe ukimchoma ataacha, walipiga makofi kweli kweli.

“Wengine niliwasikia kwa masikio yangu wakimpinga Mwalimu palepale, wengine wakisema huyu mzee kaharibikiwa uzeeni… huyu mzee kachanganyikiwa sasa, na ndiyo yanayoendelea hadi sasa ya kurudisha nyuma harakati za aina hiyo,” alisema Ulimwengu.

 MKAPA

Akijibu hoja hiyo ya Ulimwengu, Mkapa alisema wakati wa mchakato huo wa katiba yeye hakuwa mshauri wa rais na kwamba hawezi kulijibu suala hilo.

“Sikuwahi kuwa mshauri wa rais wala chama juu ya mchakato wa Katiba, lakini niliombwa kutoa maoni kama wananchi wengine,” alisema.

Awali akijibu maswali aliyoulizwa katika tamasha hilo, Mkapa alisema anajua na anakiri kuwa alikosea wakati wa uongozi wake kwa kuleta sera ya ubinafsishaji bila kuweka chombo cha kuudhibiti.

Mkapa amekuwa akirudia kauli hiyo mara kwa mara pale anapozungumzia masuala ya utawala wake.

Alisema kukosekana kwa mfumo wa udhibiti kumesababisha kuwepo na watu wanaotumia fursa hiyo kwa maendeleo binafsi badala ya taifa.

“Katika uongozi wangu kitu ninachojutia ni kuanzisha ubinafsishaji na kushindwa kuweka mfumo au chombo cha kuudhibiti,” alisema na kuongeza:

“Hicho ndicho kitu naweza kukiri nilikosea na ninachoweza kuwaomba Watanzania msamaha.”

Hata hivyo, Mkapa alisema kukosea huko hakufanyi sera ya ubinafsishaji ionekane kuwa haifai kwani imechangia maendeleo na kuongeza uzalishaji kuliko ilivyokuwa awali.

“Nilifanya kosa, lakini hatuwezi kusema ubinafsishaji haufai kwa sababu ulisaidia kuleta mabadiliko na kuongeza uzalishaji katika mashirika yaliyokuwa yameshindwa kuendeshwa na Serikali.

“Mfano mimi wakati naingia madarakani viwanda vya sukari vya Mtibwa, Kagera na Kilombero vilikuwa vikizalisha tani 120,000 hadi 130,000 lakini wakati naondoka niliacha vinazalisha tani 300,000.

“Mtibwa ilikuwa imeshakufa kabisa, lakini tuliweza kukirudisha na baada ya mimi kuondoka vimeendelea kuzalisha. Lakini inashangaza kuona miaka 17 wameshindwa kuongeza uzalishaji,” alisema Mkapa na kuongeza:

“Tatizo tunaongea sana, lakini hatufanyi kazi kwa bidii… Watanzania wanapenda sana kuwazungumzia watu badala ya kuzungumzia sera na kuziboresha ili ziwe na tija kwa taifa.”

Awali akisoma hotuba yake ya kueleza jinsi anavyomfahamu Rais wa Kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere katika kuleta maendeleo ya watu, Mkapa alisema watu wanaweza kuona kuwa Baba wa Taifa alipinga ubinafsishaji, lakini si kweli.

“Mwalimu alikubali dhana za ujasiriamali, uwekezaji, ushindani, ubunifu, ufanisi na utengenezaji wa faida vitu ambavyo viko sambamba na ubepari.

“Vitu alivyokuwa anavikataa Mwalimu ni baadhi ya mambo mabaya ya ubepari, ikiwemo unyonyaji na mgawanyo wa faida usio sawa na ndiyo maana akaweka Azimio la Arusha akilenga kuwa na jamii ya usawa isiyo na unyonyaji.

“Kama ambavyo ingekuwa kwa mtu mwingine, Mwalimu hakuwa tayari kuona ubinafsishaji wa mashirika aliyoyataifisha na mengine aliyoyaanzisha, lakini pia alitambua kuwa yasingeweza kuendelea yenyewe huku mengine yalikuwa yameshafungwa,” alisema.

Alisema kuwa Nyerere aliona faida za ubinafsishaji na kwamba hata kuhusu Benki ya NBC aliona umuhimu wa kuibinafsisha.

“Kuhusu NBC, Mwalimu si kwamba alikuwa anapinga kuibinafsisha bali ni namna ambavyo inaweza kuwanufaisha wananchi baada ya kuibinafsisha,” alisema Mkapa.

Akizungumzia kuhusu mkwamo wa kupata Katiba Mpya, alisema ni vyema watu wakaacha kuzungumza kuwa watu fulani ndio waliokwamisha na badala yake wachambue masuala ambayo yalikwamisha Katiba.

“Hakuna mtu aliyechambua ni kwanini na kwa namna gani mchakato ulikwama, tumeishia kuwanyooshea mikono watu fulani kuwa ndio waliokwamisha kwa masilahi yao,” alisema Mkapa.

Akizungumzia kuhusu uhuru wa kujieleza, Mkapa alisema licha ya watu kumwona kama rais aliyeongoza kwa mabavu, lakini ndiye aliyepanua wigo wa vyombo vya habari nchini.

“Mimi ndiye niliyemwambia Aga Khan aje awekeze kwenye vyombo vya habari baada ya kuona kuwa tulivyokuwa navyo havitoshi, walikubali na ndio ikaja Kampuni ya Nation na kuanzisha magazeti ya Mwananchi na Citizen,” alisema Mkapa.

Alisema ni vyema watu wakatumia uhuru wa kujieleza kujadili masuala ya msingi badala ya kuutumia kutoa malalamiko kwa Serikali.

Alieleza kushangazwa kwa kitendo cha Watanzania kutumia muda mwingi kulalamika, hususani wabunge vijana ambao ndio wamekuwa wakililia kupewa nafasi za uongozi.

“Kuna umuhimu wa kuwapa watu uhuru wa kujieleza, lakini pale mtu anapoutumia kulalamika tu inabidi tutafakari umuhimu wa kukunyamazisha,” alisema Mkapa.

 KINANA

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, alijikuta anashangiliwa katika tamasha hilo baada ya kutoa hoja ambayo iliwagusa moja kwa moja watawala.

Kinana alisema watawala wamekuwa wakiongoza bila kuwa na unyenyekevu wa kuwasikiliza watu wanaowaongoza na kumtaka Mkapa aeleze umuhimu wa suala hilo.

Pia alisema watawala wengi wamekuwa wanashindwa kukiri pale wanapokosea na kupokea mawazo ya watu wengine.

“Viongozi wamekuwa wakitawala pasipo kuwasikiliza wale wanaowaongoza… naomba uniambie umuhimu wa kiongozi kuwa mnyenyekevu na kuwasikiliza watu anaowaongoza pamoja na kukubali makosa pale anapokosea,” alisema Kinana huku akishangiliwa.

 PROFESA LUANGA

Wakati wa mjadala katika tamasha hilo, Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mathew Luhanga, ndiye aliyeanza kumchokonoa Mkapa kwa kumuuliza maswali kuhusu masuala mbalimbali kipindi cha uongozi wake.

Profesa Luhanga alimuuliza Mkapa ni mambo gani katika utawala wake aliyafanya katika kuhakikisha kuwa anaendeleza yale mazuri yaliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere.

Pia alitaka kujua Mkapa alipata vikwazo gani katika kutekeleza baadhi ya mambo ambayo aliamini ni mazuri yaliyoachwa na Mwalimu.

“Wewe (Mkapa) ulikuwa rais wa nchi hii, ningependa utuambie ulifanya nini kuendeleza mazuri yaliyoanzishwa na Mwalimu Nyerere na ni vikwazo gani ulikumbana navyo katika kuyaendeleza mambo hayo?” alihoji Profesa Luhanga huku akishangiliwa.

Katika kujibu maswali hayo, Mkapa alisema miongoni mwa mambo ya Mwalimu ambayo anaamini aliendeleza ni pamoja na kukifanya chama chake (CCM) kuwa imara na chenye kuwakilisha watu.

“Niliimarisha chama chetu (CCM) nikaendelea kukiweka katika misingi ya umoja na mshikamano, lakini nikahakikisha kinawakilisha watu,” alisema na kuongeza:

“Mimi nilipochaguliwa kuwa rais nilichaguliwa kwa asilimia 60 ya kura zote, lakini aliyenirithi mikoba yangu alishinda kwa zaidi ya asilimia 80 ya kura… hiyo ni ishara tosha kwamba nilikifanya chama kiendelee kukubalika,” alisema Mkapa.

Alisema mafanikio mengine ni kuboresha elimu kwa kuhakikisha kuwa kunakuwa na madarasa, vitabu.

Mafanikio mengine ni katika suala la ardhi ambapo Mkapa alieleza kuwa aliweza kuweka sera nzuri ya ardhi kwa kuhakikisha kuwa inagawanywa kulingana na matumizi.

“Niliendeleza elimu nikahakikisha kunakuwa na madarasa na vitabu, lakini kwenye ardhi nako nilihakikisha tunaigawanya kulingana na matumizi ili kudhibiti matumizi holela,” alisema.

PROFESA SHIVJI

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kavazi la Mwalimu Nyerere, Profesa Isa Shivji, alihoji kuhusu kuibuka kwa nyufa za ukabila, udini na ukanda na kutaka kujua sera za kiuchumi zinazosababisha mipasuko hiyo.

“Mwaka 1994 Mwalimu Nyerere alitutahadharisha juu ya nyufa hizi, lakini wanasiasa wa leo wameendelea kuzikuza. Serikali ni lazima iwe makini kwenye kuingia mikataba ambayo inatunyonya kama wa EPA,” alisema Shivji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles