24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

ULEVI WA MADARAKA HATARI KULIKO WA POMBE

Na Masyaga Matinyi,

BABA wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kusema mara kadha wa kadha katika hotuba zake kuwa, afadhali ulevi wa pombe kuliko ulevi wa madaraka.

Ulevi wa madaraka ni mbaya sana, kwa sababu unaweza kumfanya mwenye madaraka ajae kiburi, jeuri, dharau, asione, asisikie, asitambue hata mambo madogo yanayotambulika na hata wakati mwingine akaita mlima kichuguu na kichuguu mlima na mbaya zaidi akasahu kwamba kuna kesho.

Kama ilivyobainishwa awali kabisa, Mwalimu Nyerere alikuwa akirudia mara kwa mara kuwaonya viongozi dhidi ya ulevi wa madaraka, kwa sababu ni tofauti kabisa na ulevi wa pombe.

Mlevi wa pombe ni rahisi kujitambua au kutambulika, kwa sababu atayumba au kupepesuka, anaweza kutoa lugha ya kuudhi au wakati mwingine matusi mazito, kupigana, kulala mtaroni, kuvua nguo hadharani, kupiga yowe bila sababu na vituko vingine vingi.

Lakini matukio yatokanayo au yanayoendana na ulevi wa madaraka ni tofauti, mlevi wa madaraka hapepesuki, hapigani, halali mtaroni wala havui nguo hadharani, lakini mara nyingi utamtambua kwa kauli zake na matendo yatokanayo na dhamana ya uongozi aliyopewa.

Lakini kiongozi makini anaweza kuepuka ulevi wa madaraka, kwanza kwa kutambua dhamana aliyopewa, mipaka ya utendaji kazi yake, kuepuka kutoa kauli zinazotokana na mihemko inayoweza kuchochewa na mazingira fulani au vitu vingine ambavyo kabla ya kuvitaja ni vyema ushahidi ukawepo, kwa hiyo tuviache kwa leo.

Kubwa zaidi kwa kiongozi yeyote ni kufahamu walau kwa kusoma tu sheria mbalimbali za nchi, kanuni na taratibu. Baada ya hayo, ni vyema kwa kiongozi kuheshimu viongozi wenzake na kutofautisha vijembe kwenye majukwaa ya siasa na utendaji kazi serikalini.

Mwanzoni mwa Desemba, mwaka jana, Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, alifanya ziara ya kikazi mkoani Arusha, ziara iliyomchukua mpaka Wilaya ya Ngorongoro, wilaya ambayo ina umuhimu wa kipekee katika Sekta ya Uhifadhi nchini.

Moja ya mambo ambayo Waziri Mkuu aliyaona kwa macho yake ni kasi ya uharibifu ndani ya maeneo ya uhifadhi, ambako shughuli za kibinadamu zinashamiri siku hadi siku na kutishia usalama na uhai wa rasilimali ya wanyamapori na uoto wa asili katika maeneo hayo adhimu duniani.

Waziri Mkuu alitangaza hatua kadhaa wa kadhaa zenye lengo la kuyalinda na kuyahifadhi maeneo hayo, moja ya hatua hizo ni agizo la kuyatambua maeneo yote ya uhifadhi na kuyawekea alama za mipaka (beacons), kazi ambayo inaendelea.

Miongoni mwa maeneo ambayo kazi ya utambuzi wa mipaka inaendelea ni pamoja na Pori Tengefu Loliondo (LGCA) na maeneo yanayopakana nalo likiwamo eneo la mpaka na Hifadhi ya Taifa Serengeti.

LGCA linakadiriwa kuwa na ukubwa wa kilometa za mraba 4,000, ambapo kwa sasa limekodishwa na Serikali kwa mwekezaji Kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC), ambayo inajishughulisha na uwindaji wa kitalii.

Pamoja na Loliondo kuwa maarufu kwa uwindaji wa kitalii, shughuli ambayo inaelekea ukingoni kutokana na wingi wa mifugo, ukataji miti, ujenzi wa makazi na uharibifu mwingine wa mazingira, lakini eneo hilo lina umuhimu wa pekee kwa ikolojia ya Serengeti.

Kutokana na uharibifu huo unaoongezeka siku hadi siku, wataalamu wa uhifadhi kutoka asasi kadhaa wa kadhaa za umma wamekuwa wakiishauri Serikali kuligawa eneo hilo, lakini kwa kipindi kirefu Serikali imekuwa ikisuasua kutekeleza ushauri huo.

Kusuasua huko kumesababisha kuwapo mgogoro wa muda mrefu wa matumizi ya ardhi katika eneo hilo, jambo lililomfanya Waziri Mkuu Majaliwa kuagiza wadau wote katika mgogoro huo wakae na kutafuta suluhu ya kudumu.

Katika kulinda wanyamapori na mazingira ya uhifadhi, Tanzania ilipitisha Sheria ya Wanyamapori ya 2009 (Wildlife Management Act, 2009), lakini jambo la kushangaza usimamizi na utekelezaji wa sheria hiyo Loliondo umekwama kabisa.

Wakati akitoa agizo hilo, Waziri Mkuu hakutoa maelekezo yoyote yenye lengo la kumzuia Waziri mwenye dhamana ya Maliasili na Utalii kutimiza majukumu yake katika eneo hilo kwa mujibu wa sheria. LGCA lipo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na si Mkoa wa Arusha.

Katika kufuatilia utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Januari 25, mwaka huu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alifanya ziara katika eneo la mpaka wa Ngorongoro na Loliondo, kwa lengo la kujionea kazi ya uwekaji alama za mipaka inavyoendela pamoja na kufahamu changamoto zilizopo.

Mbali ya kukagua utekelezaji wa agizo hilo, Waziri alipata fursa ya kupita katika baadhi ya maeneo mahususi kwa ajili ya uhifadhi na kushuhudia makundi makubwa ya mifugo ikiwamo inayotoka Kenya, yakifanya uharibifu mkubwa katika vyanzo vya maji.

Mojawapo ya vyanzo muhimu vya maji alivyoshuhudia Waziri kwa kukuta kundi kubwa la mifugo ni kile kilichopo katika eneo la Olomanaa, katika Kijiji cha Piyaya, ambapo wafugaji mbali ya kuingiza mifugo kwa wingi, wamezungusha uzio wa miba, kwa lengo la kuwazuia wanyamapori kunywa maji.

Waziri hakuishia hapo tu, alikwenda kwenye mpaka wa Serengeti na Loliondo unapopita Mto Grumeti, ambao kwa sasa umekauka kutokana na uharibifu wa mazingira pamoja na ukame.

Hapo alikuta mamia ya ng’ombe wakiwa wamewekwa kusubiri giza liingie, ili waswagwe na kuingia ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kinyume cha sheria.

Kutokana na yale aliyoyaona, Waziri alitoa tamko kuwa wakati umefika sasa kwa Serikali kufanya uamuzi mgumu wenye lengo la kuliokoa eneo hilo, kwa kuligawa katika sehemu mbili, kwa ajili ya uhifadhi na matumizi ya wananchi.

Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009, Sehemu ya 16 Vifungu Na. 4, 5 na 6 inampa Waziri mwenye dhamana uwezo wa kupitia upya mapori tengefu na kufanya marekebisho mbalimbali muhimu kwa manufaa ya wananchi bila kuathiri uhifadhi.

Alisema kilometa za mraba 1,500 ziainishwe haraka na kuachwa kwa ajili ya uhifadhi na zinazobaki (2,500) ziachwe kwa ajili ya matumizi ya wananchi, ambapo pia alisema Serikali itapeleka wataalamu kusaidia kupanga matumizi sahihi ya eneo hilo, pamoja na kuhakikisha huduma ya maji inapatikana, huduma ambayo ni changamoto kubwa katika eneo hilo.

Tamko kama hilo la Waziri Maghembe linalolenga kuiokoa LGCA na Serengeti si la kwanza kutolewa na Waziri mwenye dhamana ya Maliasili na Utalii.

Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Machi 19, 2013, baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, alitoa tamko halali la kupunguza ukubwa wa LGCA kutoka kilometa za mraba 4,000 hadi kilometa za mraba 1,500.

Lakini kutokana na udhaifu kiutendaji na kiuamuzi wa Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, Septemba 23, 2013, akiwa katika Kijiji cha Waso, alitengua tamko la Waziri Kagasheki na kuruhusu shughuli za kibinadamu katika eneo lote la Pori Tengefu Loliondo, bila kujali athari dhidi ya uhifadhi, ambapo matokeo hasi ya uamuzi huo yanaonekana dhahiri hivi sasa.

Lakini katika hali ya kushangaza ambayo bila shaka inatokana ni ulevi wa madaraka, Jumatano wiki iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alikejeli tamko la Waziri wa Maliasili na Utalii na kuliita “maoni ya mdau muhimu.”

Pia alisema halitambui tamko hilo, bali anasimamia maelekezo ya Waziri Mkuu yanayoelekeza kuendelea kwa mazungumzo kwa ajili ya kupata suluhu.

Kwa kumbukumbu zilizopo nchini, si jambo la kawaida kwa Mkuu wa Mkoa kutoa tamko kama la Gambo, tena anakejeli tamko halali kisheria la Waziri, huku akijua kabisa LGCA halipo chini ya mamlaka ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Pia ndani ya Serikali kuna utaratibu wa viongozi kuwasiliana au kuwasilisha malalamiko, sidhani kama lile lilikuwa jukwaa sahihi kwa Gambo kusema alichokisema.

Gambo kabla ya kutoa tamko lake alipokutana na wadau wa habari, alipaswa kwanza kutafakari athari za tamko hilo, kwa sababu zinaweza kuchochea ‘uasi’ wa wananchi dhidi ya hatua halali na yenye tija na maslahi mapana kwa Taifa, kwa sababu suala la kuilinda Loliondo na Serengeti si suala la majadiliano, ni wajibu wa kila Mtanzania mwenye akili timamu.

Haijulikani ni kwa kiasi gani Mkuu huyo wa mkoa kijana kabisa anaufahamu vipi mgogoro huo wa matumizi ya ardhi Loliondo, ambao umekuwa ukivuma tangu 2008, kwa sababu ndani ya mgogoro huo kuna siasa nyingi, ubinafsi, usanii, uongo, fitna uzandiki, fedha chafu na mambo mengine mengi ya ovyo.

Pia anapaswa kufahamu kuwa, wajanja wale wale ‘waliocheza’ na akili za Waziri Mkuu mstaafu Pinda hadi akatengua tamko la aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Kagasheki, ndio hao hao ambao wamemzunguka wakimzidishia ulevi uliotajwa awali. Jitafakari upya RC Gambo.

0755530066

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles