28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ulanzi unavyokuza kipato, kuchochea Ukimwi Iringa

MWANDISHI WETU

ULANZI ni pombe inayotengenezwa kwa kutumia utomvu wa mianzi midogo aina ya Oxytenanthera abyssinica ambayo haijakomaa.

Mianzi inayoanza kukua hukatwa vilele wakati wa majira ya mvua. Utomvu hukusanywa katika chombo, kisha kiowevu hiki huanza kuchachuka mara moja.

Ulanzi unapogemwa kwa mara ya kwanza huwa mtamu kama mtobe au juisi, lakini unapomaliza muda, huwa mchachu.

Kwa kawaida huwa haudumu kwa muda mrefu.

Pombe hii hutegemewa zaidi na wananchi wengi wa mikoa ya nyanda za juu kusini ikiwamo Njombe, kwa ajili ya kuwapatia kipato.

Nchi za Kiafrika zimekuwa zikihangaika kukuza na kuboresha chumi zao, kwa kujiwekea na kupanga mikakati mbalimbali kufikia lengo hilo.

Licha ya wakazi wake kuwa na ndoto hiyo, Tanzania inapania kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Mikoa ya nyanda za juu kusini ambako mianzi hupatikana kwa wingi, wajasiriamali mbalimbali wameamua kutumia rasilimali hiyo kuanzisha viwanda vya usindikaji, ikiwamo vya pombe ya ulanzi.

ukitembelea mkoani Iringa, utashuhudia namna ambavyo pombe ya kienyeji ya wenyeji wa mkoa huo, ulanzi inavyogeuzwa moja kwa moja kuwa pombe ya viwandani.

Katika Kijiji cha Mlandege, wakulima wa ulanzi wanaelezea faida na hasara ya zao hilo la ulanzi.

”Tunasomesha watoto kwa sababu ya biashara hii ya ulanzi na mambo ya kilimo. Hiki ni kinywaji ambacho watu wengi wanakifurahia, lakini kwa upande mwingine ukizidisha kinakuwa na madhara hivyo, tunawaasa watu kunywa kwa kipimo,” anasema mmoja wa wanakijiji.

Hata hivyo, anasema viongozi huwashauri kuhusu unywaji wa kileo hicho kupindukia.

Diwani wa Kata ya Mseke mkoani Iringa, Robert Lawa, anasema wananchi katika eneo lake wamekuwa wakipata kipato kutokana na ulanzi huku akieleza pia madhara ya kinywaji hicho iwapo mnywaji atazidisha.

Anasema watu wengi wameweza kujipatia kipato, kulipia watoto ada na baadhi ya wanavijiji kujikwamua kiuchumi kupitia kinywaji hicho.

”Wakati wa ulanzi mwingi, watu hufanya ngono zembe, kupata mimba zisizotarajiwa na wengine inawapa uvivu wa kutofanya kazi kabisa,” anasema Lana.

Anasema kuwa kuna baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiwanywesha watoto wao pombe hiyo ya kienyeji hivyo, yeye na maafisa wake wamekuwa wakiwaelimisha juu ya madhara wanayoweza kuyapata.

Awali ilielezwa kuwa katika maeneo yanayogema pombe ya ulanzi mkoani Iringa kuwa na unywaji uliopitiliza hali iliyosababisha ongezeko la utapiamlo na lishe duni kwa watoto.

Mratibu Msaidizi wa Afya ya Uzazi na Mtoto Manispaa ya Iringa, Afra Mtuya, anazungumzia madhara ya watoto wadogo kupewa ulanzi hali inayomsababishia udumavu.

Anasema kina mama huwapatia watoto wao pombe ya ulanzi kwa sababu ina ladha tamu kiasi cha kwamba huwavutia, hali inayomfanya kunywa hadi analewa na kulala.

”Mtoto kama huyo wakati mwingi hali kwa wakati unaofaa na mzazi asipotilia maanani tatizo hilo, mtoto ni lazima atapata utapiamlo, udumavu wa mwili na akili,” anasema.

Ili kuepukana na madhara ya unywaji wa pombe hiyo kiholela na bila vipimo, juhudi zinahitajia kufanya kinywaji hicho kuwa cha kisasa na kuhimiza ujenzi wa viwanda nchini hususan vidogo na vya kati.

Kuna baadhi ya watu wameamua kutumia fursa hiyo baada ya viwanda vingi vidogo na vya kati kuanzishwa katika sehemu hiyo.

”Tuliamua kufanya hivyo baada ya kuona kwamba ulanzi hauna soko la kutosha, halafu wagemaji wenyewe hawagemi kwa usafi, tukaona wacha tuboereshe zaidi,” anasema Mwanzilishi wa kiwanda hicho, Sophia Msola.

Mjasiriamali huyo anasema alipata msukumo zaidi wa kuendeleza biashara hiyo kutokana na tamko la Rais Dk. John Magufuli, wakati alipotembelea Iringa na kutangaza kuwa Tanzania inaelekea kuwa ya kiviwanda.

”Nilijua hapa nitapata msaada wa kujiendeleza, nikaanza kusindika taratibu. Lakini changamoto tunayopata ya kufanya kinywaji hiki kuwa cha kisasa ni kwamba kikiwekwa kwenye chupa, basi huvunjika. Ulanzi huwezi kuusindika kwenye plasiki,” anasema mjasiriamali huyo aliyeajiri wafanyakazi watatu na vibarua wawili.

Anasema ana uwezo wa kuuza kinywaji hicho hadi kreti tano kwa siku, lakini hawezi kufanya hivyo kwa sababu ulanzi hauwezi kuwekwa kwenye chupa.

Msola anasema laiti kama angepata vifungashio na mtaji wa kutosha, angeweza kujisaidia yeye binafsi na jamii inayomzunguka.

ILIVYOGUNDULIWA

Pombe ya ulanzi iligunduliwa wakati wa utawala wa machifu wa kabila la Wabena katika Wilaya ya Njombe wakati huo, baada ya mti mchanga wa mwanzi kukatika na kuanza kutoa maji matamu.

Tangu wakati huo, pombe hiyo imekuwa ikithaminiwa na wakazi wa Mkoa wa Iringa na tayari imesambaa na kufika katika maeneo mengine mengi hasa kusini mwa Tanzania.

KICHOCHEO CHA UKIMWI

Wanywaji wengi wa ulanzi wanasema bila shaka kwamba pombe hiyo inachangia kasi ya Ukimwi.
“Msimu wa ulanzi huwa unauzwa bei rahisi ambayo hakuna inayemshinda, ndio maana watu wengi hulewa hivyo kuwa rahisi kwao kufanya ngono bila kujiandaa kwani wanawake wengi wakishanunuliwa kinywaji hicho huwa wepesi kukubali,” anasema Richard Michael.
Anasema pombe hiyo ndiyo kichocheo kikubwa cha ngono zembe hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa maambukizi ya Ukimwi.
“Ulevi hasa wa pombe ya ulanzi unachangia kuongeza hamu ya kufanya ngono zembe, wengi wamejikuta wakipata maambukizi kutoka na pombe hii ambayo inaheshimiwa na wenyeji,” anasema.
Ulanzi siyo kichocheo pekee, suala la mila na desturi potofu ambazo jamii nyingi mkoani humo bado inaziendeleza pia huchagia maambukizi. Miongoni mwao ni kukosekana kwa usawa kijinsia, kutakasa wajane na wasichana, kuoa wake wengi, imani za kishirikina na kutotahiri.
Nyingine ni umaskini wa kipato, ambapo maisha ya wananchi wengi yanaonekana kuwa duni.
Anasema kutobadili tabia licha ya elimu ya Ukimwi kuwafikia wananchi na wengine kuathiriwa kwa njia moja au nyingine na ugonjwa huo, ni miongoni mwa sababu za kuenea kwake.
Anataja sababu nyingine kuwa ni mwingiliano mkubwa wa watu kutokana na shughuli nyingi za biashara na ongezeko la taasisi mbalimbali mkoani humo.

POMBE YA KIENYEJI BURKINA FASO

Tokea kipindi cha hapo awali, kila jamii ilikuwa ikisindika mazao yanayotokana na vyakula vya asili ili kuyaweka katika hali ya usalama kwa matumizi ya familia kula na kunywa. Mazao mengine yaliyosindikwa yalikuwa ni kwa ajili ya kuuza.

Hivyo ndivyo ilivyo kwa nafaka huko Burkina Faso, Nchi iliyo katikati ya Afrika magharibi. Nchini Burkina Faso, nafaka hasa ulezi mwekundu na mweupe, husindikwa kuwa dolo, au pombe ya kienyeji. Dolo huwa na kileo inaposindikwa na huwa haina kileo inapokuwa haijasindikwa.

Ieleweke kwamba, huko Burkina Faso na baadhi ya nchi zingine zinazotumia lugha ya kifaransa, pombe hii ya kienyeji inasemekana kutengenezwa kwa kutumia mtama, japokuwa kiuhalisia hutengenezwa kwa ulezi mwekundu au mweupe. Hii huitwa pombe ya ulezi au Dolo.

Mara nyingi pombe hii ya kienyeji huandaliwa maalumu kwa ajili ya matukio maalumu kama vile sherehe za kijadi, mazishi na sherehe za siku ya uhuru, lakini leo hii ni kinywaji maarufu cha kibiashara ambacho ni salama kwa kunywa na ina kiasi kidogo cha kileo, pia huweza kupatikana katika masoko yote ya mijini na vijijini kote nchini. Utengenezaji wa pombe ya ulezi ni shughuli ya kuongeza kipato inayowaweka wanawake wengi katika hali ya kujishughulisha katika ‘nchi ya watu waaminifu.’ Hii ndio maana ya Burkina Faso katika lugha ya Kiswahili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles