33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

‘Ulaji’ mkoa wa Rukwa waishtua PAC

Amina MwidauPatricia Kimelemeta na Shabani Matutu

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeshindwa kupitisha hesabu za Mkoa wa Rukwa baada ya kubaini kuwapo ufisadi katika baadhi ya matumizi za fedha za Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Amina Mwidau, alisema ufisadi huo umebainika katika hesabu za mwaka 2012/13.
Mwidau alisema Sh 44,394,927 zimetumika kumlipa mzabuni Julius Akilimali kwa ajili ya matengenezo ya gari lenye namba za usajili STK 5508 bila ya kuonyesha vielelezo vya matumizi ya fedha hizo.
Alisema malipo hayo yametumika ndani ya mwaka mmoja, jambo ambalo limewafanya wajumbe wa kamati hiyo kuwa na shaka.
“Tumeshindwa kupitisha hesabu za Mkoa wa Rukwa baada kubaini kuwapo upungufu wa hesabu zao, hatukubaliani na hali hii,” alisema Mwidau.
Alisema licha ya kufanyika kwa malipo hayo, kamati hiyo imebaini magari kumi ya Serikali yaliyotolewa kwa shughuli mbalimbali ndani ya mkoa huo, matatu yameuzwa bila ya kuonyesha viambatanisho.
Mwidau alisema mkoa huo pia umetumia Sh milioni 20, kwa ajili ya kuchapisha vitabu wakati wa maadhimisho ya sherehe za Uhuru mwaka 2012 bila ya kuambatanisha vielelezo vya matumizi ikiwamo risiti.
Alisema kutokana na hali hiyo, kamati imewapa wiki tatu kutafuta nyaraka zote zilizotajwa kwenye kikao hicho na kuziwasilisha Mei 15, mwaka huu mkoani Dodoma ili wajumbe wa kamati waweze kuzipitia.
Hata hivyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Smythies Pangisa alikiri kuwapo udhaifu kwa baadhi ya watendaji, jambo ambalo limesababisha baadhi ya vyaraka kutoonekana.
“Ni kweli kuna tatizo kwa baadhi ya watendaji wetu ambao wameshindwa kuweka kumbukumbu sahihi za matumizi ya Serikali, suala hili nitalishughulikia kabla ya kuwasilisha taarifa hii mjini Dodoma,” alisema Pangisa.
Alisema kutokana na hali hiyo, watendaji ambao watabainika kwenda kinyume watachukuliwa hatua za kinidhamu ili iwe fundisho kwa wengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles