28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ukuta unavyohatarisha maisha ya watu Pangani

mpina 1Na Amina Omari, TANGA

MJI mkongwe wa Pangani ulioko mkoani Tanga umeathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi kutokana na kina cha maji ya bahari kuongezeka kwa kasi.

Hali hiyo ya kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari imesababisha athari katika mji huo baada ya ukuta unaozuia maji ya bahari na makazi ya watu kumeguka na kuanza kutishia uhai wa makazi ya watu wa mji huo.Ukuta huo ulijengwa mwaka 1805 na wakati wa utawala wa kijerumani wakati wakitawala katika eneo hilo.
Kutokana na mji huo kuwa karibu na pwani ndipo walipojenga ukuta huo pamoja na mitaro ya kupitisha maji pale ambapo bahari ilikuwa na bamvua, maji yaliweza kupita kwenye mitaro hiyo hadi mjini na kisha kurudi baharini tena.

Wakati huo hifadhi ya eneo la pwani ilikuwa inatuzwa na uwapo wa mikoko pamoja na matumbawe ambayo yalikuwa yanazuia kasi ya maji ya bahari.
Lakini uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa mikoko umesababisha mawimbi makubwa ya bahari wakati wa bamvua (kujaa na kupwa kwa maji ya bahari) na kuubomoa ukuta huo.

Wakati wa bamvua maji yanasonga mbele zaidi kutokana na kutokuwepo kwa kizuizi chochote katika pwani ya bahari hiyo, na hivyo kusababisha kuharibu nyumba kadhaa za mjini Pangani zilizojengwa karibu na ufukwe.

Aidha athari nyingine iliyopo kwenye mji huo maji ya bahari yameweza kuingia ndani zaidi na kuharibu visima kadhaa ambavyo sasa vina maji ya chumvi yasiyofaa kwa matumizi ya binadamu.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais
Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina, hivi karibuni alitembelea Wilaya ya Pangani
kukagua ukuta huo ambapo alishuhudia namna ulivyoathiriwa na maji ya bahari.

Anasema kubomoka kwa ukuta huo kunadhihirisha namna athari za mabadiliko ya tabia nchi zinavyoweza kuleta madhara makubwa kwa jamii pamoja na viumbe vyake.

“Huu ni ushahidi tosha kuwa kasi ya shughuli za binadamu katika kuharibu mazingira ikiwemo ukataji wa miti ovyo unachangia kuleta madhara ya mabadiliko ya tabia nchi katika maeneo mbalimbali nchini,”anasema Mpina.

Anasema serikali itahakikisha ukuta huo unakarabatiwa kwa haraka iwezekanvyo ili
kunusuru hali ya sasa ilivyo.
Anasema tayari wamepata fedha kutoka nchi za Umoja wa Ulaya Sh bilioni 2.2 kwa ajili ya kuanza ujenzi huo.

Ambapo eneo la ukarabati wa ukuta wenye urefu wa mita 1,600 katika ufukwe unaotenganisha bahari ya Hindi na mji wa Pangani na ujenzi unaanza rasmi mwezi huu.

“Nawahakikishia wakazi wa Pangani kwamba tumeamua kumaliza kabisa changamoto hii iliyowakabili kwa muda mrefu,” anasema.
Vilevile amebainisha kwamba mradi wa kukarabati ukuta huo unahitaji Sh bilioni 3 na kwamba serikali inaangalia uwezekano wa kupata fedha nyingine kutoka kwenye bajeti yake kiasi cha dola 400 sawa na Sh milioni 800 ili kukamilisha ujenzi.

Naibu Waziri huyo pia ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Pangani kufanya tathmini ya haraka ya uharibifu wa fukwe za bahari katika eneo la Pangadeco ili kubaini athari zinazoendelea kujitokeza.
Anasema tathmini hiyo itaiwezesha serikali kujiwekea mipango endelevu ya kuzuia uharibifu wa fukwe kunakochochewa na mabadiliko ya tabianchi.

Anasema tayari serikali imepata Dola 352,000 za Kimarekani kutoka kwa wafadhili mbalimbali ili kutekeleza kazi ya kufanya tathmini katika maeneo mengine ya fukwe za bahari yenye
uharibifu kama ilivyo kwa Pangani.
“Tunapofanya utafiti mapema katika maeneo mapya ya uharibifu wa fukwe inasaidia serikali kujipanga na kutenga bajeti ya kupunguza
madhara bila hata kutegemea misaada ya wafadhili,” anasema Mpina.
Meneja mradi ujenzi wa ukuta huo, Mkongo Twahiru, anasema utafiti kuhusu mradi huo tayari umekamilika na kinachosubiriwa ni mkandarasi aweze kupatikana kuanza ujenzi huo.
Anasema tathimini ya awali ya ukarabati
iliyofanyika mwaka 2009 ilionyesha eneo la ambalo linahitaji ukarabati ni mita 474.

Anasema kuchelewa kuanza kwa ujenzi huo kwa wakati kumesababisha maeneo yaliyoharibika kuongezeka na kufikia mita 600.

Meneja huyo anasema licha ya ujenzi wa ukuta huo wameanza kutekeleza mradi wa upandaji miti ya mikoko pembezoni mwa eneo la fukwe ili kuhifadhi mazingira ya bahari.

“Mradi huu utakapokamilika utasaidia
mji wa Pangani kuepukana na tatizo la kumezwa na maji ya bahari kutokana na
mabadiliko ya tabia nchi,” anasema.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kimang’a, Salum Choba, anasema mara kwa mara bajeti ilikuwa inapangwa lakini fedha zilikuwa

hazipatikani kwa wakati ili kuanza utekelezaji wake.

“Halmashauri imekuwa ikitenga fedha kidogo kwa ajili ya ukarabati hasa katika maeneo yaliyokuwa hatarishi lakini uwezo mdogo wa kifedha umekuwa hautoi matokeo mazuri,”anasema Choba.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Arshie Mntambo ameishukuru serikali kwa kuonyesha nia Ya kutenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles