33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Ukosefu wa shule ulivyoharibu ndoto za watoto Bagamoyo

*Dk. Kawambwa aomba wadau wa maendeleo kujitokeza

AVELINE KITOMARY 

NI ukweli usiopingika kuwa elimu ni msingi wa ustawi mzuri wa kutambua, kuelewa na kufanya vitu mbalimbali katika kila jamii yoyote ile inayohitaji kusonga mbele kimaendeleo. 

Katika jamii yetu, zamani ilikuwa ikitolewa elimu ya mila,utamaduni na desturi mbalimbali ambapo wazee au wazazi walijihusisha kuwapatia elimu watoto na vijana.

Lakini kwa ulimwengu wa sasa wa ushindani ili nchi au sehemu yoyote iweze kufanikiwa kiuchumi,kisiasa, kilimo, ufugaji na mengine kuna haja ya kupitia darasani kupata elimu.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kipindi chake cha uongozi alipata kuwataja maadui watatu wa maendeleo kuwa ni ujinga,maradhi na umasikini. 

Muonekano wa kijiji cha Fuyosi, kitongoji cha Kalimeni, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani

Kutokana na hilo, Rais wa awamu ya tano, John Magufuli amefanikiwa kwa kiwango kikubwa kupambana na maadui hao.

Pamoja na mafanikio hayo, lakini kwa baadhi ya sehemu kumekuwa na changamoto kubwa ya elimu,afya na umasikini. 

Mwandishi wa makala hii ataelezea jinsi ukosefu wa huduma za kijamii kama elimu unavyoangamiza ndoto za watoto wengi katika Kijiji cha Fuyosi iliyopo Kitongoji cha Kalimeni wilayani Bagamoyo katika Mkoa wa Pwani.

Kitongoji hicho cha Kalimeni kina jumla ya kaya 268 ambapo kati yao kuna wanaume 144 na wanawake 124 takwimu hizo ni za mwaka 2017 lakini bado kunaongezeko la watu.

Shughuli kubwa inayofanywa katika kitongoji hicho ni kilimo cha mahindi na mihogo, hata hivyo wanakijiji hao bado wako katika umasikini uliokithiri.

Asilimia kubwa ya wanakijiji hawajui kusoma wala kuandika, kuanzia wakubwa mpaka wadogo, naweza kusema hawaendani kabisa na dunia ya sasa ni kama watu waliosahaulika gizani. 

Umasikini na ukosefu wa huduma za shule, afya,maji, migogoro ya wakulima na wafugaji na barabara, umekuwa ukizunguka kingo za Kitongoji hicho tangu nchi ipate uhuru.

Kizazi hadi kizazi wamekuwa hawana desturi ya kupata elimu, watoto wengi sasa wako kijijini bila hatima yao kujulikana.

Kutokana na kukosekana kwa huduma ya elimu kwa watoto katika kijiji hicho, hali hiyo imesababisha watoto wengi kujiingiza katika vitendo visivyoendana na wao kama ndoa za utoto,mimba katika umri mdogo na wizi kwa watoto wa kiume.

Sababu kubwa ya watoto wengi waliofikisha umri wa kwenda shule kutokwenda ni umbali wa shule iliyopo katika kijiji mama cha Fukayosi. 

Ni takribani kilometa 12 huduma ya elimu inapatikana hivyo kusababisha watoto kushindwa kwenda shule na kubaki nyumbani na wazazi wao. 

Watoto wengi walijaribu kwenda shule lakini wameishia njiani kutokana na changamoto za umbali wa kilometa hizo nyingi, huku wazazi wakiwa hawana uwezo wa kuwalipa gharama za usafiri wa kwenda shule kila siku.

MADHARA YA BAADAYE YA KUKOSA ELIMU

Subira Fikiri ni mtoto mwenye umri wa miaka 15, anasema aliwahi kusoma shule ya awali kwa miaka minne baada ya kupona akaamua kuacha na kubaki nyumbani na mama yake,hakuweza kwenda shule ya msingi kwa sababu ya umbali. 

“Nimebaki na mama yangu,baba alishafariki nilipelekwa kusoma chekechea kwa miaka minne 20012-2015, kwani hii ndio ipo hapa kijijini kwetu baada ya miaka yote nikaamua kuacha na sasa nakaa tu nyumbani.

“Sijui kusoma wala kuandika kwani  nilishindwa kusoma shule ya msingi kwasababu ya umbali wa shule, hata hivyo mama yangu hana uwezo wa kugharamia nauli hata uwezo wakunipangishia chumba hana,”alisema Subira.

Subira ambaye tayari ana mtoto aliyetimiza mwezi mmoja na siku 20, anasema amekata tamaa kabisa ya kupata elimu kutokana na hali yake ya sasa.

“Baada ya kukaa nyumbani muda mrefu sikuwa na la kufanya niliingia katika vishawishi vya kingono baada ya hapo nikapata mimba na sasa nina mtoto mmoja katika umri huu mdogo sijui hata nifanyeje,”anasimulia kwa masikitiko.

Kuhusu ndoto ya kupata elimu, Subira anasema alitamani siku moja awe daktari ili aweze kuisaidia jamii ya Kitanzania. 

“Ndoto yangu kielimu nilikuwa nataka nisome ili niwe daktari nitibu watu hasa jamii yangu lakini sasa niko tu hapa kijijini ndoto zangu, zimeishia njiani sasa nina mtoto ananitegemea, mama yangu kama unvyomuona hana uwezo,nyumba yenyewe ndio hii inakaribia kuanguka,”anaelezea Subira.

Subira anasema hata sasa anatamani kusoma ili atimize malengo yake endapo kama atapata mtu wa kumsomesha.

“Natamani hata sasa ningesoma,napenda kupata elimu, nikipata nafasi ya kusoma naamini nitafanya vizuri na ninaweza kutimiza ndoto yangu,”anasema.

Mtoto mwingine, Salum Kindamba mwenye umri wa miaka 14, licha ya umri wake wa kusoma kufika lakini bado hajaanza hata darasa la kwanza na hajui kusoma wala kuandika. 

“Wazazi wangu hawana uwezo wa kumlipia nauli ya pikipiki ili niende shule hapa nina wadogo zangu watano wote waliofikia umri wa kwenda shule hawaendi pia,naomba Serikali itujengee shule,”anasema Kindamba.

Mmoja wa watoto anayesoma akitokea kijijini hapo, Husen Saleh mwenye umri wa miaka 12 anasema anasoma darasa la pili lakini kutokana na kuchelewa kufika shule imesababisha afanye vibaya katika mitihani.

“Tuko wawili tu tunaokwenda shule, tunapata shida ya usafiri wakati mwingine huwa tunaenda kwa miguu,wakati mwingine tunavizia lift na wakati mwingine hatuendi kabisa shule.

“Tunaweza kufika darasani saa nne au tano tukifika mwalimu ameshafundisha tunachukua madaftari ya wenzetu tunaandika,mwalimu yeye hatuchapi kwasababu anajua tunatoka mbali lakini darasani hatufanyi vizuri na hatusomi vizuri,”anaelezea Husen.

UMASKINI UNACHELEWESHA UJENZI

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kalimeni, Amos Rungwa anasema usaili walioufanya Novemba mwaka jana watoto 120 wanatakiwa waende shule.

Kwa mujibu wa Rungwa, eneo la ujenzi wa shule tayari limeshatengwa na kupimwa hivyo kilichobaki ni ujenzi wa madarasa kuanza.

“Takwimu za mwaka jana tulivyoanza kupata kibali cha kuanzisha shule, tuna watoto wako mtaani 120 ambao wamefikisha umri wa kwenda shule ni miaka mitano sasa tangu kijiji kimetenga eneo kwaajili ya ujenzi wa shule lakini mpaka sasa bado hatujafanikisha.

“Tangu tumefanya takwimu wengine wameshazaliwa na wengine muda wao wa kuanza shule umeshapita, mfano mtoto wa miaka 7 anatakiwa aende shule sasa tunapobaki naye mpaka anafika miaka 14 hata akipelekwa darasa la kwanza wenzake watamshangaa,”anasema Rungwa.

Anaeleza kuwa watoto wengi mpaka sasa hawasomi na wako kijijini, huku wengine walioanza kusoma wakiishia katikati kwa sasabu ya umbali wa shule kwani gharama za kupeleka mtoto shule nauli ya pikipiki kila siku ni Sh 10,000.

“Wengi wako mitaani wengine wameshaoa wengine wamepewa mimba wakiwa watoto,vijana wengine wamekuwa wezi hata juzi tunatoka kuwafunga wawili miaka mitano mitano kwaajili ya wizi hali hii inasikitisha,usafiri ni pikipiki ambapo gharama zake ni Sh 5000 kwenda na Sh 5000 kurudi wazazi maisha duni hawamudu. 

Anasema hali ya umasikni uliokithiri katika kijiji hicho, unakwamisha kuanza ujenzi wa shule hiyo wanaendelea kuwahamasisha wanakijiji waendelee kuchanga.

“Kama unavyoona ndugu mwandishi hali ya hapa ni mbaya hata nyumba zetu unaziona hapa, wote masikini na darasa moja linagharimu Sh milioni 15 huo uwezo wa kufikia hizo fedha ni ngumu ingawa nitaendelea kuwahamasisha wanakijiji kuchanga na tumepanga kila kaya katika kijiji watoe Sh 5000. 

“Hivi karibuni tulipata barua kutoka Ofisi ya Mratibu Elimu wa Kata ya Fukayosi ya kuanza kujenga shule kuanzia la kwanza mpaka darasa la saba lakini bado hatujafanikisha zoezi la uchangishaji.

Anawaomba wadau mbalimbali wa maendeleo na Serikali,kujitokeza kuungana na wao katika kukamilisha ujenzi wa shule hiyo ili watoto wapate elimu.

“Tunaomba wadau mbalimbali, taasisi za kidini na Serikali waungane pamoja na sisi kuchangia gharama za ujenzi wa shule ili watoto wetu wasiendelee kukaa mtaani na wao wanapata elimu kama watoto wengine.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Fukayosi, Salum Mkecha anasema changamoto ya elimu ipo kwa vitongoji vyake hasa Kalimeni ambayo ndio iko mbali zaidi kuliko vitongoji vingine.

“Vitongoji vinaumbali mrefu kutoka kijiji mama cha Fukayosi tunaendelea kufanya juhudi ili shule hiyo ijengwe,tunaendelea kuchangisha wanakijiji japo wana hali mbaya, tutajitahidi kupita vitongoji vyote tisa kwaajili ya kupata mchango wa Sh 5000,”anaelezea Mkecha. 

HALI YA HUDUMA ZINGINE 

Mwenyekiti huyo nasema hata huduma zingine za afya,maji na barabara bado ni changamoto kwao. 

Anasema katika kipindi cha mwaka 2008 na 2017 akina mama takribani sita walijifungulia barabarani, huku watu watatu wakipoteza maisha kutokana na kukosa huduma ya uzazi.

“Ukiacha elimu hata huduma zingine bado zinachangamoto kama huduma ya afya hatuna, hapa akinamama wakati mwingine wanajifungulia njiani hata ukisema utakodisha gari barabara haipitiki. 

“Hali hii imesababisha akinamama kujifungulia barabarani kwamfano tangu mwaka 2008 hadi 2017, akinamama kama sita wamejifungulia barabarani na pia watu watatu wamepoteza maisha mwaka 2017 mama na mtoto wote walipoteza maisha mwaka 2012 mtoto alipoteza maisha kwasababu ya kukosa huduma,”anaelezea Rungwa.

Kwa mujibu wa Rungwa hata upatikanaji wa maji katika kitongoji hicho ni changamoto kubwa.

Anasema maji yanaletwa kutoka sehemu nyingine na wanalazimika kununua kwa dumu Sh 1500 hadi 2000 kwa dumu moja.

“Tulikuwa tumeshaanza kuletewa huduma ya maji kwa mradi wa maji Wami Makurange tangu mwaka juzi, mipira imechimbwa chini bomba ipo na tanki la maji lipo lakini hayatoi maji.

“Sisi tunategemea kuletewa dumu ni Sh 1500 mpaka 2000 na sio watu wote wanamudu kununua maji kwa gharama hiyo kubwa tunaomba Serikali pia iingilie hili maana hata mkandarasi wa mradi huu wa maji hatumwelewi,”anabainisha Rungwa. 

MBUNGE AAHIDI KUTOA MATOFALI 

Mbunge wa Bagamoyo, Dk.Shukuru Kawambwa anakiri kuwepo kwa changamoto ya huduma za jamii katika kitongoji hicho ikiwemo ile ya kupata elimu.

Anasema kutokana na hali ya umasikini ya wananchi wake amechangia matofali 5,000, hivyo anaahidi kuwa atafuatilia suala la ujenzi hadi utakapokamilika. 

“Yote hayo nayajua na tunahangaikia na tayari nimeshawachangia matofali,wananchi wangu ni masikini lakini nawaomba waunge mkono juhudi za ujenzi wa shule.

“Nitaenda Kalimeni wiki ijayo nijue wamefikia wapi na katika kikao changu nahamasisha sana hilo ni kweli watoto kule hawasomi na sio jambo zuri pia naelewa umbali wa shule ni mrefu nalifuatilia kwa ukaribu,”anaeleza Dk Kawambwa.

Dk. Kawambwa aliyepata kuwa Waziri wa Elimu wakati wa Serikali ya awamu ya nne, anawaomba wadau wa maendeleo waweze kuwasaidia ili kufanikisha huduma za jamii katika eneo hilo.

“Tunaomba wadau wa maendeleo wajitokeze, ndugu mwandishi hata mimi nahangaika kuzungumza na wadau wengine ili kufanikisha suala hilo la ujenzi wa shule,”anabainisha Dk. Kawambwa.

Kuhusu maji anasema yako katika hatua ya kufika huko na muda sio mrefu watapata huduma hiyo na tayari mradi umeshaanza.

Anasema pia atahakikisha barabara inayoelekea katika kitongoji hicho itachongwa ili kurahisisha usafiri.

“Kuna mradi wa maji imeshaanza kule hivyo wananchi wangu wasijali watapata maji na pia barabara inayoelekea huko itachongwa ili iweze kupitika,”anaahidi Dk. Kawambwa. 

UTARATIBU WA SERIKALI

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa anasema kwa utaratibu wa Serikali wananchi wanatakiwa waanze kujenga baada ya hapo ndio wanaweza kupata msaada wa halmshauri. 

Anasema hata hivyo baada ya kusikia hali ya elimu atalifikisha suala hilo halmashauri. 

“Kwa utaratibu wananchi wanatakiwa kuanza wao wenyewe halafu halmashauri itawasaidi lakini kwasasabu umeniambia nitalifikisaha suala hilo halmashauri,”anasema Kawawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles