24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Ukitaka kuaminika, epuka kusema kitu usichomaanisha

Christian Bwaya

“NINA mke asiyeniamini kabisa. Hana imani kabisa na mimi.  Juzi kati hapa nimemkuta anachunguza simu yangu. Tuligombana sana.” Haya ni maneno ya kijana mmoja ambaye ndani ya ndoa hawaaminiani na mkewe.

Kijana huyu anaonekana kusumbuliwa na hali ya mke wake kukosa imani na yeye. Kuchunguzwa kwa siri, kwake ilimaanisha kuwa mke wake hamwamini.

Nilimwuliza kwanini anafikiri mke wake hamwamini? Akajibu: “Basi tu ndivyo alivyo. Hata ufanyaje hana imani.”

Hivi ndivyo vijana wengi walivyo, anadhani mke wake ana wajibu wa kumwamini. Hakujua kwamba naye kwa upande wake alikuwa na wajibu wa kuweka mazingira ya kuaminiwa na mkewe.

Sote kama alivyo kijana huyu, tuna hitaji la kuaminiwa. Tunatamani watu wasiwe na shaka juu yetu. Tunatamani watu waamini yale tunayowaambia. Tunaposema jambo, tunatamani watu wengine waliamini. Tunapofanya mambo fulani, tusingependa watu wawe na shaka nasi. Tunajisikia vizuri kuaminiwa.

Hata hivyo, yapo mazingira tunakutana nayo, kama ilivyokuwa kwa kijana huyu, tunajisikia kutokuaminiwa. Pengine nawe umewahi ‘kuwadai’ watu wakuamini. Umekwenda kwa rafiki, mathalani, kumkopa fedha. Rafiki yako anasita. Hakuamini. Unajisikia vibaya kuona rafiki yako hakuamini. Unamwomba akuamini. Tusichojua ni kwamba kuaminiwa si tukio bali matokeo ya yale tunayoyafanya.

Maisha hayaendi bila kuaminiwa. Ndio maana hata mtu muongo, laghai, angependa kuaminiwa. Kazini, wakubwa wa kazi wanapenda mtu anayeaminika. Bila kuaminika, huwezi kupata mafanikio. Usalama wa kazi, kwa kiasi kikubwa unategemea namna gani mwajiri anakuamini. Biashara pia inategemea kiwango cha kuaminika. Mfanyabiashara anapoaminiwa na wateja wake anakuwa kwenye nafasi kubwa ya kupata mafanikio.

Urafiki kati ya watu wawili, hali kadhalika, unategemea kwa kiasi kikubwa namna watu hao wanavyoaminiana. Huwezi kuwa na urafiki mzuri na mtu kama hamuaminiani. Kuaminiwa ni msingi wa uhusiano wowote wa karibu na hata shughuli zinazohusisha watu zaidi ya mmoja.

Kuaminiwa, si tukio la siku moja wala haki inayoweza kudaiwa kwa watu. Mke hawezi kudai ‘aaminiwe’ na mumewe. Mume hali kadhalika. Kuaminika ni zao la tabia zetu. Kuaminiwa ni sawa na miamala ya benki.  Unaweza kuchukua kile ulichokiweka. Huwezi kudai zaidi. Fanya mambo matatu uaminiwe.

Mosi; sema ukweli daima. Fikiria uko mahali na rafiki yako ukamsikia akimdanganya mwenzake kwenye simu. Hata kama aliyedanganywa ni mwingine, kwa vyovyote vile imani yako kwa aliyedanganya inapungua. Uongo unapunguza kuaminika.

Ukitaka kuaminika, jenga tabia ya kusema ukweli. Epuka kusema kitu usichomaanisha kwa lengo tu la kuwafurahisha watu. Usimdanganye mtu hata kama unajua hatagundua. Ukitambulika kama mtu mwenye tabia ya kusema ukweli unawafanya watu wasiwe na wasiwasi na maneno yako. Utaaminika.

Pili; kuwa na tabia ya kutimiza ahadi zako. Ishi unachokisema. Unajua ni rahisi kutoa ahadi hasa kama hujiamini na unatamani kuwaridhisha watu. Hata hivyo, ni vizuri kuelewa kuwa ahadi ni kipimo cha ukomavu wako. Usipotekeleza ahadi zako watu wanakuchukulia kama mtu asiye na ukomavu. Huwezi kuaminika katika mazingira unayoonekana huna ukomavu.

Kuliko kutoa ahadi kwa lengo la kumridhisha mtu, ni bora usiahidi kabisa. Punguza matarajio ya watu kwako, kisha fanya jitihada za kuzidi matarajio hayo. Unapoahidi kufanya kitu, tekeleza. Ukishindwa kutekeleza, kuwa muungwana. Omba msamaha. Kwa namna hii watu watakuamini.

Tatu; heshimu na utaheshimika. Mtu asiyeheshimika ni vigumu kuaminiwa. Wapo watu wanaaminiwa kirahisi kwa sababu tu wamejijengea taswira ya heshima kwa jamii. Heshima ni zaidi ya vitu ulivyonavyo na namna unavyoonekana. Heshima kubwa unayoweza kupewa na watu inategemea vile unavyowaheshimu. Ukitaka kuheshimiwa, heshimu watu.

Unapokuwa na tabia ya kuwadharau watu, kujiona bora kuliko wengine, watu wanakudharau.  Hata wale unaowazidi wanastahili heshima. Hata wanaokukosea na kukutendea mabaya wanastahili heshima. Ukijenga tabia ya kulipa ubaya kwa wema utashangazwa na matokeo.

Jambo la kukumbuka ni kwamba watu wanaweza kupoteza imani na wewe kimya kimya. Si kila mtu anaweza kukutangazia kuwa hana imani na wewe. Linda tunda la uaminifu. Imani ikipotea ni vigumu kuirejesha. Habari njema ni kwamba kadri unavyojiwekea mazingira ya kuaminika, ndivyo utakavyoendelea kuaminika.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya, Simu: 0754 870 815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles