31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa wadai kunasa waraka wa Ikulu

ukawa hawaSHABANI MATUTU NA PATRICIA KIMELEMETA

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umedai kunasa waraka wa Ofisi ya Rais Ikulu unaoonyesha Serikali imetenga Sh bilioni 2.5 kwa ajili ya kampeni ya kuwezesha Katiba inayopendekezwa ipitishwe   kwa kupigiwa kura ya ndiyo katika kura ya maoni.

Katibu Mkuu wa Ukawa ambaye pia ni Katibu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alidai Dar es Salaam jana  kuwa kampeni hiyo itafanywa kupitia vyombo vya habari  kuwahamasisha wananchi waweze kupiga kura ya ndiyo na kuipitisha kwa urahisi Katiba inayopendekezwa.

Waraka huo alidai kwamba unatoka Ikulu kwenda kwa Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo na kuelekeza kazi hiyo inatakiwa kuanza wiki hii zikipatikana Sh milioni 50 za kuanzia.

“Ofisi ya Rais Ikulu imetenga Sh bilioni 2.5 kwa ajili ya kuhamasisha wananchi waweze kuipigia kura ya ndiyo Katiba pendekezwa.

“Lengo ni kutaka kuipitisha Katiba hiyo bila ya kuwaelimisha wananchi jambo ambalo ni kinyume na sheria,” alisema Dk. Slaa.

Alisema suala hilo ni kinyume na sheria kwa sababu  wanaohusika na utangazaji au uhamasishaji wa Katiba mpya ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na siyo Ofisi ya Rais Ikulu.

Alidai ofisi hiyo imeandaa Kamati ya Kudumu ya Habari ya kusimamia mpango wa kuelimisha umma hadi muda wa kura ya maoni.

VYOMBO VYA HABARI

Dk. Slaa alidai baadhi ya vyombo vya habari vimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo zikiwamo redio,   magazeti, mitandao ya jamii na televisheni mbalimbali   kuhakikisha mpango huo unafanikiwa.

Alidai wahariri wa vyombo hivyo wametengewa fedha kuhakikisha wanatumia vyombo vyao kutenga vipindi vya kutoa elimu kwa wananchi juu ya suala hilo.

Dk. Slaa alidai vipindi hivyo vitaongozwa na baadhi ya watu walioandaliwa kufanya kazi hiyo wakiwamo wasomi kutoka vyuo vikuu nchini; baadhi yao ni wale waliokuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.

WASOMI

Dk. Slaa alidai  wasomi hao watalipwa Sh 500,000 kwa kila kipindi watakachoshiriki katika muda wa wiki 22  kuhakikisha suala hilo linafanikiwa.

“Wameamua kuwachukua baadhi ya wasomi kutoka vyuo vikuu, tena baadhi yao walikuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuendesha vipindi hivyo  kwenye media mbalimbali nchini,” alisema.

NGOMA, VIKUNDI VYA UTAMADUNI

Dk. Slaa alidai katika kampeni hiyo pia zitatumiwa    ngoma na vikundi vya utamaduni vya asili wakiwamo   maofisa utamaduni wa maeneo mbalimbalia kwa ajili ya kuvikusanya pamoja vikundi hivyo.

Njia nyingine alizitaja kuwa ni kubandika mabango katika miji mikuu ya mikoa kuongeza uelewa wa Katiba inayopendekezwa ili wananchi waipigie kura ya ndiyo.

Alipotafutwa kwa simu kuzungumzia madai hayo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ofisi ya Rais Ikulu, Salva  Rweyemamu alisema; “nitakupigia baadaye”.

Hata hivyo hakuweza kupiga na alipotafutwa mara kadhaa baadaye simu yake haikupatikana hadi tunakwenda mtamboni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles