26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa: Magufuli ajiandae kwa lolote

Pg 2NA WAANDISHI WETU

SIKU moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kupiga marufuku vyama vya siasa kufanya ushindani wa kisiasa hadi baada ya miaka mitano, wanasiasa na wanazuoni wameibuka tena na kuendelea kumpinga.

Akitoa tamko la wabunge wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema Magufuli anapaswa kujua kuwa siasa si starehe bali ni kazi kama zilivyo nyingine na kwamba si tukio la uchaguzi bali ni maisha pia ni mfumo unaogusa maisha yao ya kila siku.

Pia alimshutumu Magufuli kuwa hata uamuzi wake wa kuzuia matangazo ya Bunge kuonyeshwa moja kwa moja (live) na vituo vya televisheni ilikuwa ni mkakati wake wa kupora haki za raia kupata taarifa.

“Walianza kwa kulidhibiti Bunge na wabunge wa upinzani kwa kujaza askari bungeni kama vile ni uwanja wa vita; wakadhibiti haki ya msingi ya wananchi kufuatilia mijadala ya Bunge kupitia matangazo ya live kisha wakazuia uhuru wa vyombo vya habari katika kuhoji na kuchambua kwa uhuru habari mbalimbali zisizowapendeza na hatimaye wanataka kugeuza nchi ya utawala wa mabavu ya kutumia dola,” alisema Mbowe.

Pia alisema hatua ya Magufuli kutoa kauli Ikulu jijini Dar es Salaam juzi wakati akipokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana iliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kutaka kuwafunga midomo kwa kuwazuia kufanya mikutano na shughuli zote za siasa ni kinyume cha Katiba na sheria za nchi zilizounda uwapo wa vyama vingi vya siasa.

Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, alisema uhalali wa kazi za siasa unatolewa na Katiba ambayo Magufuli aliapa kuilinda na kukaziwa na sheria namba 5 ya mwaka 1992 pamoja na marekebisho yake.

Alisema haki ya kufanya siasa haiwezi kuwa miliki ya Serikali, wabunge na madiwani pekee kama anavyoagiza Magufuli huku akisisitiza kuwa Uchaguzi Mkuu si tukio pekee la kisiasa kwa sababu kuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa, uchaguzi mdogo wa marudio na mambo mengine mengi.

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema mwenendo wa Magufuli kuwa mkali katika kusimamia uwajibikaji na utendaji wa Serikali ni jambo jema, lakini linapoteza maana kama ukali huo unatumika kuvunja Katiba na sheria pamoja na kuziba watu midomo na alisisitiza kuwa suala hilo watalipigania na kulitetea kwa gharama yoyote.

“Tumepokea kwa mshtuko mkubwa kauli na maagizo ya Magufuli kuhusiana na haki ya kufanya shughuli za kisiasa ikiwamo mikutano ya hadhara, makongamano na hata maandamano kwa vyama vya siasa.

“Tumetafakari kwa kina kama kweli Magufuli anafahamu vyema sheria zinazotawala na kuongoza siasa katika nchi anayoiongoza ingawa bado tunaendelea kudadisi maana ya demokrasia na tafsiri ya nini ni siasa kwa uelewa wa rais wetu.

“Rais anapaswa kutambua kuwa fursa za wananchi ni kusema, leo hii wananchi hawana sukari, watoto wao wamefukuzwa shule, leo hii hakuna mtendaji wa Serikali anayeweza kumwambia rais ukweli, sisi tutasema, leo rais anaingilia Bunge, anaamua kumleta spika ili aibebe Serikali.

“Hatutasita kumkosoa rais, hatutakubali kuzibwa midomo, rais atambue fursa ya kuzungumza kwa wananchi ni jambo la afya kwa kuwa ukiwalazimisha wasiseme, watasema kwa vitendo jambo linaloweza kusababisha vitendo vya kigaidi, eti anajifanya mkali, huwezi kuwa mkali kwa kuvunja sheria za nchi,” alisema Mbowe.

Kwa upande wake, Mbobezi wa Sayansi ya Siasa na Uhusiano, Profesa Mwesiga Baregu, alisema kitendo cha Magufuli kusema haiwezekani kila siku iwe ni kufanya shughuli za siasa na badala yake watazame wajibu waliopewa na wananchi watakaowapima kama wametekeleza yale waliyoahidi katika kampeni za mwaka jana maana yake ni sawa na kumziba binadamu pumzi na alimtaka ajiandae kwa lolote.

Profesa Baregu ambaye pia aliwahi kuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na gazeti hili, alisema binadamu lazima ajitetee pale unapomzuia kufanya siasa.

“Binadamu anaitwa formal political (kiumbe cha siasa) kabla hajakuwa kiumbe cha uchumi, kauli hii iliwahi kutolewa na mwanafalsafa wa Ugiriki, Aristotle. Sijui kama hata rais amewahi kumsoma huyu mtu maana asingeongea haya maneno, ukimwambia binadamu asifanye siasa  kama unamziba pumzi, rais anawaziba pumzi Watanzania anataka wafe?

“Unaweza ukamnyonga kuku ukasalimika lakini si binadamu, lazima ajitetee hata kidogo na katika kujitetea anaweza akashinda au akashindwa na kukubali kufa, katika hili rais inabidi ajiandae na awe tayari kwa lolote,” alisema Profesa Baregu.

Pia alisema kauli ya Magufuli inaonyesha  ameanzisha vita ya kuishambulia Katiba ya nchi pamoja na sheria ya vyama vya siasa.

“Bado nipo katika mshtuko, hii inaitwa ufashisti yaani zaidi ya udikteta kama kweli bwana mkubwa ameamua kufanya hivi, siamini kama nchi yetu imefikia hapo, mtu yeyote anaweza kusema maneno hata yakiwa kinyume na Katiba.

“Naona Magufuli ameamua kupambana na Watanzania, demokrasia pamoja na Katiba ya nchi, hapa hajashambulia vyama bali ameishambulia Katiba na sheria ya vyama vya siasa, hiyo haitawezekana, anataka sijui atufuge wote kama kondoo,” alisema Profesa Baregu.

Alisema kauli ya Magufuli kwamba hatokubali watu wamkwamishe katika kazi zake maana yake anapanga kuwadhibiti watu wanaomkosoa kiutendaji na kuminya uhuru wa kujieleza.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema yeye haoni kama kauli ya Magufuli imepiga marufuku shughuli za kisiasa bali inapaswa ijadiliwe kwa upana ili ieleweke vizuri.

“Sioni kama amekataza lakini watu wanaikuza tu hiyo kauli, nadhani yeye ametumia kwa muktadha wa Watanzania tungekuwa na busara tungeacha kufanya siasa kipindi hiki, nadhani kasema angekuwa yeye asingejihusisha na siasa lakini hajapiga marufuku,” alisema Dk. Bana.

Alisema kama kuna kiongozi anatoa kauli za kukataza wananchi kufanya siasa si nzuri kwa kuwa kikatiba hakuna mtu anayeweza kumkataza mtu kufanya siasa.

Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha United Democratic (UDP), Goodluck ole Medeye, alisema hakubaliani na msimamo wa Magufuli kwa sababu unatishia kuua vyama vya siasa.

Medeye aliyejiunga UDP hivi karibuni, alisema chama chao kimepanga kukutana na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP),  Ernest Mangu, ili kulizungumzia suasa hilo na kama ikishindikana wataomba kuonana naye.

“Sisi hatukubaliani na msimamo huo wa Magufuli, hata kama ameruhusu kwa wabunge na madiwani kufanya siasa katika maeneo yao, inakuaje kwa vyama kama vyetu ambavyo havina wabunge, anataka tufanye nini au tufe?

Hata kama mazungumzo yetu na Jaji Mutungi na IGP Mangu yatakwama, tutaomba tukutane naye maana tunajua mamlaka makubwa aliyonayo kwa nchi hii, yaani akitoka Mungu ni yeye, hivyo kabla hatujakwenda kwa Mungu tutamuomba kuonana naye na kumwambia kuwa msimamo huo si sahihi kwetu,” alisema Ole Medeye.

Wakati wanasiasa na wanazuoni wakimpinga Magufuli, Jaji Mutungi ameviasa vyama vya siasa kuwa wavumilivu, kuchambua mambo kwa mapana kabla ya kutoa matamko.

Jaji Mutungi alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu ya mkononi na alisema kauli ya Magufuli ilitafsiriwa kulingana na uelewa wa kila mmoja alivyojisikia lakini alikuwa akimaanisha wanasiasa waachane na siasa zisizo na tija kwa Taifa.

“Wanatakiwa kufanya siasa zenye kuleta maendeleo, wanasiasa wajitafakari kubadili mfumo wa siasa, maana uliopo sasa hauleti tija katika mustakabali wa maendeleo ya Taifa,” alisema Jaji Mutungi.

Alisema wanasiasa wanatakiwa kujipa muda wa kutafakari kwa kina hotuba kama ya hiyo ili waweze kutoa matamko.

“Nawasihi wanasiasa wawe watulivu, wajipe muda wa kuchambua jambo kwa mapana, watu wametoa tafsiri tofauti, rais angekuwa anataka kuua demokrasia asingewaambia anataka kushirikiana nao katika maendeleo.

“Watu wawe wa kweli, tusidai demokrasia kwa ngazi ya kitaifa wakati ndani ya vyama vya siasa hakuna demokrasia,” alisema Jaji Mutungi.

Habari hii imeandikwa na Aziza Masoud na Evans Magege (Dar es Salaam), Kulwa Mzee na Arodia Peter (Dodoma)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles