23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa kimeeleweka

0D6A5036Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam

HATIMAYE Manispaa ya Ilala imekiruhusu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutumia viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam kuzindua kampeni zake.

Wakati hayo yakijiri, mgombea wa chama hicho chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, jana alikutana na wanawake kutoka vyama vinavyounda umoja huo na kuwaambia wana CCM bado wana nafasi ya kujiunga naye.

KURUHUSIWA JANGWANI

Jana, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngurumi, alisema viwanja vya Jangwani viliombwa na CCM, kwa ajili ya kufanyia bonanza pamoja na shughuli nyingine za wabunge na madiwani wao.

Alisema hata hivyo tayari wamewaandikia barua ya kuwaruhusu Ukawa kuendelea na mkutano wao kesho.

“Hatujawakatalia wala kuwazuia Ukawa kufanya mkutano katika viwanja hivyo, bali walipoomba tuliwaeleza kuwa viwanja hivyo kuna mtu ambaye tayari ameshalipia.

“Utaratibu umekwishafanyika na tayari tumeandaa barua ya kuwafahamisha Ukawa kutumia viwanja vya Jangwani kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni zao Jumamosi,” alisema.

Manispaa imesema gharama ya kukodi viwanja hivyo ni Sh 75,000 kwa siku na CCM ilikodi kwa siku nne kuanzia Agosti 28 hadi 31, lakini katika kibali chao inaonyesha wameruhusiwa kwa siku mbili tu, Agosti 28 na 29 kwa gharama ya Sh 150,000 badala ya Sh 300,000 kwa siku nne kama ilivyoainishwa na manispaa hiyo.

Kibali hicho chenye namba 00012339 na risiti namba 380835 iliyotolewa Agosti 26, mwaka huu, kinaonyesha waliokodi viwanja hivyo kuanzia kesho ni Bendi ya Tanzania One Theatre (TOT) inayomilikiwa na CCM.

 

CCM WATAKA UKAWA WAWAANGUKIE

Hata hivyo, pamoja na hatua ya Manispaa ya Ilala, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba, alisema watawaruhusu Ukawa kufanya mkutano wao wa uzinduzi wa kampeni kesho endapo wataenda kwa viongozi wa CCM pamoja na Manispaa ya Ilala kuomba.

Alisema CCM hawana tatizo, wameridhia kutoa viwanja hivyo, lakini viongozi wa Ukawa wakaonane na viongozi hao ili kibali kilichotolewa na Manispaa ya Ilala kibadilishwe.

“Hata sisi mwanzoni tuliomba kufanya uzinduzi wetu katika Uwanja wa Taifa kutokana na kwamba viwanja vya Jangwani vilikuwa havifai kutokana na uchafu uliokuwepo, lakini tulikataliwa.

“Tulifanya utafiti katika viwanja vya Biafra Kinondoni, Mbagala na Tanganyika Parkers tukaona kuwa viwanja hivyo havikidhi kutokana na wingi wa watu.

“Kama chama tuliamua kufanya usafi katika viwanja vya Jangwani kwa gharama zetu hatimaye tulifanikiwa na tulifuata taratibu zilizowekwa na manispaa na kulipia viwanja hivyo kwa ajili ya kufanyia shughuli zetu za burudani, sanaa na kufanya kampeni kwa wabunge na madiwani wetu,” alisema.

Simba alisema waliomba kibali kihalali katika Manispaa ya Ilala Agosti 21 na kulipia Agosti 26 mwaka huu kiasi cha Sh 150,000, kwa ajili ya kuutumia Agosti 28 hadi 31 mwaka huu.

“Uchaguzi una utaratibu na sheria zake, tunawashangaa Ukawa wanakurupuka na kutaka kufanya mkutano wao Jangwani wakati hawajaomba uwanja huo, ni vyema kila chama kinapohitaji kufanya shughuli mbalimbali za kampeni ziandae maeneo yao mapema ili vyama mbalimbali visije vikakutana na kusabaisha vurugu na uvunjifu wa amani.

“Ukawa wanalalamika ili waonewe huruma, lakini huruma haipo, kilichopo ni kufuata utaratibu wa sheria ili kuweza kufanikisha malengo yao,” alisema.

 

NEC YANENA

Kwa upande wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema Chadema kwenye rasimu yao ya ratiba waliyowasilisha tume, haikusema kuwa itazindulia kampeni zake kwenye uwanja gani.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima,  alisema: “Hilo suala wanapaswa waongee wenyewe wayamalize, nina ratiba hapa ya kampeni nchi nzima, lakini katika Chadema wameandika watazindua kampeni Agosti 29 kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa 12 jioni.”

Wakati Kailima akisema hayo, jana gazeti hili pia lilifanikiwa kuona barua ya NEC kwenda halmashauri za jiji, manispaa, miji na wilaya, ikitaka ratiba za uchaguzi zilizoandaliwa na tume zizingatiwe na kuheshimiwa.

“Pale ambapo mgombea urais, makamu wa rais, akihitaji kutumia kiwanja katika halmashauri apewe kipaumbele, katika kutumia kiwanja hicho, kwa ajili ya mikutano ya kampeni bila kujali chama anachotoka mgombea huyo.

“Wagombea wote wahudumiwe kwa usawa bila upendeleo. Mikutamo ya wagombea ubunge na udiwani isizuie mikutano ya wagombea urais na umakamu wa rais kufanyika katika viwanja husika,” ilisema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Kailima.

 

HELKOPTA PALEPALE

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi, alisema hawatakubaliana na ukandamizaji wa aina yoyote inayowafanya wakose haki yao katika kipindi hiki cha uchaguzi.

“Vijana hatutakubaliana na udhalilishaji wowote katika kipindi hiki cha uchaguzi. Tutatumia usafiri wa helkopta kwa sababu hakuna sheria ambayo inatuzuia, tutatumia kwa kufuata utaratibu wa sheria.

“Pia kuhusu uwanja wa Jangwani hakuna zuio lolote la maandishi tulilolipata, na kwa vyovyote vile tutatumia ule uwanja kuzindua mkutano wetu,” alisema Katambi.

Mwenyekiti huyo wa Bavicha aliwataka vijana wa vyama vya Ukawa kujiandaa kufanya maandamano nchi nzima endapo haki haitatendeka.

Katambi ambaye anagombea ubunge katika Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia Chadema, alikumbushia siku alivyotekwa na kuchaniwa fomu zake ambapo pamoja na kumbaini askari mmoja, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

“Tunachoomba hivi sasa Serikali ituambie kama na yenyewe ni sehemu ya uchaguzi kwa kupendelea CCM na kukandamiza upinzani…vijana hatutakubali kufanyika uonevu wa aina yoyote,” alisema.

 Habari hii imeandaliwa na Asifiwe George, Aziza Masoud na Elizabeth Hombo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles