28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa: Bajeti ya Serikali hewa

bajeti hewa* Wasema trilioni saba zilizowasilishwa hazipo

* Wanusa harufu ya ufisadi ununuzi wa ndege, BRN

* Wahoji ujenzi wa kiwanja cha ndege nyumbani kwa Magufuli

Na Khamis Mkotya, Dodoma

KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni imeibuka na kudai kuwa Bajeti Kuu iliyotangazwa juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango ni hewa.

Akisoma maoni ya kambi hiyo jana, pasipo uwepo wa wabunge wenzake wa Kambi ya Upinzani, ambao wanaendelea na mgomo wa kumsusia Naibu Spika wa Bunge, Naibu Waziri Kivuli wa Wizara ya Fedha na Mipango, David Silinde alikosoa lakini pia alihoji baadhi ya mambo aliyodai yamepenyezwa kwenye kwenye bajeti hiyo.

Silinde ambaye wakati anaitwa kwa ajili ya kuwasilisha bungeni maoni ya kambi hiyo kuhusu hali ya uchumi wa Taifa, Mpango wa Maendeleo ya Taifa na Makadario ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 alitokea moja kwa moja lilipo lango kuu la kutokea nje ya Ukumbi wa Bunge, alisema serikali ya ‘hapa Kazi tu’ imepeleka bajeti bungeni yenye jumla ya shilingi trilioni 29 huku kati ya hizo trilioni 7 zikiwa hazijulikani zilikotoka.

Katika hilo, Silinde aliishutumu moja kwa moja serikali kwa kukiuka ibara ya 137(1) inayomtaka Rais kutoa maagizo kwa wahusika kutengeneza mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha unaofuata, jambo ambalo halikufanyika.

Silinde katika kuthibitisha kauli hiyo kwamba serikali imepeleka bajeti hewa bungeni alitoa sababu sita;

“1. Kwa mujibu wa Kitabu cha Mapato ya serikali katika mwaka huu wa fedha volume 1 ‘Financial Statements and Revenue estimates’ for the year 1st July ,2016 to 30th June 2017 kilicholetwa hapa Bungeni kinaonyesha kuwa mapato yote ya serikali yaani mapato ya kodi, yasiyokuwa ya kodi , mikopo na misaada ya kibajeti itakuwa jumla ya shilingi trilioni 22.063.

Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa mapato hayo ni kama ifuatavyo;

  1. Mapato yatokanayo na kodi na tozo mbalimbali ni shilingi Trilioni 17.797

 

Mapato yasiyokuwa ya kodi ni shilingi Bilioni 665.664

 

iii. Mikopo na misaada ya kibajeti ni shilingi Trilioni 3.600” alisema Silinde

Katika kuthibitisha hoja yake hiyo Silinde ambaye alisema ni muhimu wabunge wakatambua kuwa serikali hii haijaonyesha chanzo kingine kipya cha mapato ambacho hakijathibitishwa au kupitishwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba aliitaja sababu nyingine inayothibitisha u-hewa wa bajeti hiyo akisema tayari Bunge limeshaidhinisha matumizi ya jumla ya shilingi Trilioni 23.847

 

“ Kwa mujibu wa kitabu cha matumizi ya kawaida ,volume II Estimates of Public Expenditure Consolidated Fund Services for the year 1st July ,2016 to 30th June, 2017 na kitabu cha Maendeleo, Volume IV Public Expenditure Estimates Development Votes (part A) …mchanganuo wa fedha hizo ni kama ifuatavyo:

  1. Fedha za Matumizi ya Kawaida (Volume II) shilingi 13,336,042,030,510
  2. Fedha kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo (Volume IV) shilingi 10,511,945,288,575

 

Katika kuthibitisha hilo alisema ukichukua kitabu cha Mapato ya Serikali (Revenue Book Volume I) utaona kuwa jumla ya mapato yote ya serikali ni shilingi Trilioni 22.063, ila serikali imepanga kutumia kiasi cha shilingi Trilioni 23.847 kiasi ambacho ni tofauti na Mapato iliyopanga kukusanya.

Alisema tofauti yake ni kuwa kuna nakisi ya shilingi Trilioni 1.783 jambo alililotaja kuwa linaifanya bajeti hii kukosa uhalali kwani nakisi hiyo ni kubwa sana.

 

“Kwa mujibu wa maelezo ya waziri wa fedha ‘Mapendekezo ya kiwango na ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/17 kwenye mkutano wa wabunge wote katika ukumbi wa JNICC’  Aprili 6, 2016 pamoja na maelezo ya hotuba yake aliyoyatoa hapa Bungeni uk. 91 ameendelea kulidanganya Bunge na Dunia kuwa katika mwaka huu wa fedha serikali ina bajeti ya kiasi cha shilingi Trilioni 29.539,” alisema.

 

Silinde alikwenda mbali akinukuu hotuba ya Waziri wa Fedha, katika ukurasa wa 92 kipengele kinachohusu ‘Mfumo wa Bajeti wa Mwaka 2016/17’  ambacho kinaonyesha kuwa kiasi cha shilingi trilioni 7.475 ni mikopo ya ndani yenye masharti ya kibiashara.

Katika hilo alisema fedha hizo kwenye kitabu cha mapato hazipo na pia hazionekani zitakopwa kutoka Benki gani kama ambavyo mikopo ya nje yote imeonyeshwa kwenye kitabu cha mapato.

“Hata kwenye kitabu cha miradi ya maendeleo hazionekani kwenye kutekeleza mradi wowote ule na hivyo ni sahihi kusema kuwa ni fedha hewa , maana hazina hata kasma yake na Bunge hili tunapitisha kasma” alisema Silinde.

Silinde pia alihoji mantiki ya serikali kutangaza katika bajeti ya 2016/17 na si mwaka 2020 kusudio lake la kukata kodi ya asilimia 5 kwenye kiinua mgongo cha wabunge kinacholipwa kila mwisho wa muhula wa miaka mitano.

Pamoja na kwamba Kambi Rasmi ya Upinzani  ilisema haina tatizo na pendekezo hilo, zaidi iliitaka serikali kwenda mbali kwa kuifanyia marekebisho sheria ya mafao ya viongozi wa kisiasa ambayo kwa sasa imewapa misamaha ya kodi ya viinua mgongo viongozi wakuu wa kisiasa kama Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, Spika, Naibu Spika, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ili na wao waweze kulipa kodi.

 

“Bunge linapitisha takwimu zipi hasa? Kitabu cha hotuba ya waziri au ni vitabu vya mapato na matumizi pamoja na kile cha miradi ya maendeleo?

“Fedha ambazo waziri ameeleza kwenye hotuba yake kuwa ni mikopo ya ndani ya masharti ya kibiashara zinakopwa ili kugharimia miradi ipi? Kwani tayari kitabu cha miradi ya maendeleo – Volume IV – kimeshataja miradi yote na kiasi cha fedha ambazo kila mradi utatumia.

“Waziri wa Fedha anaposema kuwa fedha za matumizi ya kawaida ni Sh. Trilioni 17.719 na hapo hapo anasema kuwa tunakwenda kulipa deni la taifa Sh. Trilioni 8, mbona hizi fedha hazipo kwenye kitabu ambacho kinapitishwa na Bunge? (kitabu cha matumizi ya kawaida volume IV).

“Kwa kuwa CAG anakagua kasma zilizopo kwenye vitabu yaani Volume IV na Volume II, katika bajeti hii atakagua kasma ipi? Maana fedha za kulipia deni la taifa hazipo kwenye kitabu cha Volume II.

“Kuingiza malipo ya kiunua mgongo cha wabunge ambacho kitaanza kulipwa 2020 kwa mujibu wa sheria na kuwa chanzo cha mapato katika mwaka huu wa fedha 2016/2017 hiki si chanzo hewa?,” alihoji Silinde.

Silinde iliitaka Serikali kuwasilisha vitabu vyenye kumbukumbu na takwimu sahihi ili wabunge waamue kuipitisha au kuikataa, vinginevyo Bunge litakua halitimizi wajibu wake.

 

HARUFU YA UFISADI ATCL

Akizungumzia mwenendo wa uendeshaji wa Shirika la Ndege (ATCL), Silinde alisema mpango wa serikali wa kutaka kununua ndege tatu mpya kwa ajili shirika hilo una harufu ya ufisadi, kutokana na kiwango kikubwa cha fedha kilichotengwa kinyume na bei halali.

“Waziri wa Fedha alipokuwa akiwasilisha mpango wa maendeleo hapa bungeni alisema serikali imeamua kununua ndege mbili aina ya Q400 na CS300 moja. Ndege aina ya Q400 mwaka jana ilikuwa Dola za Marekani milioni 31.3 na ndege aina ya CS300 ilikua Dola za Marekani milioni 82.0.

“Hivyo kimahesabu ndege hizo tatu jumla yake ni Sh. Bilioni 318.120 na hivyo kufanya Sh. Bilioni 181.880 kusalia. Kambi rasmi ya upinzani inataka kujua ni kwanini serikali ilitenga Sh. Bilioni 500 wakati bei halisi za ndege zinajulikana?

“Hizi fedha ambazo zitabaki baada ya kununua ndege zitatumika kufanya shughuli gani? Je kuna wakala katika ununuzi huu wa ndege ambaye atapata kamisheni na kama yupo ni kiasi gani?,” alihoji Silinde.

Mbali na hilo Kambi hiyo ya Upinzani pia ilihoji kitendo cha serikali kukiuka makubaliano ya ujenzi wa awamu ya pili ya uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwl.Julius Nyerere ambayo waliingia na Kampuni ya Ujenzi ya BAM International ya Uholanzi.

Katika hilo alisema ujenzi huyo upo katika hatihati ya kusimama kutokana na wizara ya fedha kukiuka masharti ya mkataba.

Pia kambi hiyo ilihoji hatua ya serikali kwenda kutafuta Mkopo Mpya mbali na ule wa HSBC nje ya makubaliano ya mkataba baina ya BAM na TAA wa Octoba 2015.

 

UJENZI WA KIWANJA CHA NDEGE CHATO

Kambi hiyo ya Upinzani pia ilihoji ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege cha Chato ambako ni nyumbani kwa Rais John Magufuli.

Kambi hiyo ilihoji kama kuna utafiti wa kina uliofanya juu ya ujenzi wa kiwanja hicho na majibu kuonyesha kuwa ujenzi wake ni kipaumbele cha Taifa kwa sasa?

Pamoja na hilo Kambi hiyo ilishauri fedha kiasi cha shilingi bilioni mbili zilizotengwa kwa ajili ya kuanza kufanyika upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja hicho zisiongezwe kwenye kuimarisha viwanja vilivyopo kwa sasa na hasa ikizingatiwa kuwa serikali ndio kwanza inawaza kununua ndege tatu za ATCL.

BRN YAMINYWA

Silinde aliishangaa serikali kuamua kukivunja kimya kimya Kitengo cha Ofisi ya Rais cha Kufuatilia Ufanisi wa Utekelezaji wa Miradi (BRN).

Alisema katika fungu hilo serikali imetenga Sh. Bilioni 27 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya matokeo makubwa sasa, huku ikiacha kutenga fedha kwa ajili ya mishahara ya watumishi wake.

“Itakumbukwa kuwa wakati kitengo hiki kinaanzishwa tulipinga uanzishwaji wake kwani kilikuwa ni kwa ajili ya ulaji tu. Serikali mwaka huu imeamua kukivunja kitengo hiki kwa kutotenga hata senti moja kwa ajili ya mishahara ya wafanyakazi wake zaidi ya Sh. Milioni 397 zilizotengwa kwa ajili ya kulipia pango.

“Kambi rasmi ya upinzani inataka kujua waliokuwa watumishi wa kitengo hiki wamefukuzwa au wamesimamishwa kazi? Mbona hakuna fedha za mishahara katika kitengo hiki?

“Ni sababu gani zimefanya kitengo hiki kutopatiwa fedha. Ni nani ataenda kusimamia fedha za maendeleo Sh. Bilioni 27 ambazo zimetengwa kama kitengo hiki hakina wafanyakazi?,” alihoji Silinde.

Aidha, Silinde alihoji sababu ya kodi ya pango ya kitengo hicho kupungua kwa asilimia 48, ikilinganishwa na mwaka 2015/2016 ambapo kitengo hicho kilitengewa Sh. Milioni 602.800.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles