24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ukamataji senene makazi ya watu wazuiwa Bukoba

Nyemo Malecela-KAGERA

KAMATI ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera imezuia ukamataji senene katika makazi ya binadamu na badala yake shughuli hizo zinatakiwa kuhamishiwa sehemu za wazi zilizotengwa kwa shughuli maalumu.

Tamko hilo limetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawilo.

Alisema ukamataji wa senene unaoendelea sasa unaweza kusababisha mji wa Bukoba kuteketea kwa moto.

“Ukamataji wa senene unaotumika sasa ni wa kutumia moshi wa majani mabichi yanayochomwa moto karibu na jenereta zinazotumia petroli na umeme uliofungwa bila kufuata taratibu za kiusalama,” alisema.

Wakati wa katazo hilo, Mkuu wa Idara ya Mazingira Manispaa ya Bukoba, Tambuko Joseph alisema sheria ya mazingira ya mwaka 2004 sehemu ya nane iliyopo katika tangazo la Serikali kifungu 193, inazuia na kudhibiti uchafuzi wa mazingira.

Pia kifungu 106 kinazungumzia machukizo yote yaliyotajwa kwamba hayaruhusiwi kwenye maeneo ya makazi, wakati huo sheria ya afya ya umma ya mwaka 2009 kifungu cha 54 kinazuia machukizo yaliyotajwa.

Alisema sheria ya udhibiti wa mazingira pia inazungumzia madhara ya kelele ilhali kwa sasa jenereta zimesambazwa katika mitaa na pembeni wanawasha moto ambao unaweza kusababisha mlipuko wa moto.

Tambuko alisema katazo hilo lina lengo zuri la kuinua kipato cha wananchi kwa kufuata sheria za nchi.

“Sheria inasema ni vizuri shughuli hizo za uvunaji senene zikafanywa nje ya maeneo ya mji na zikafanywa kwa maelekezo ya wataalamu ili kuweza kujikusanyia kipato, lakini pia kuhakikisha sheria za nchi zinazingatiwa,” alisema.

Pia alisema taa zinazotumika kukamata senene kitaalamu zina athari kwa jamii kutokana na kuwa na mwanga mkali, wakati jenereta zinasababisha kelele katika makazi na moshi unazalisha hewa ya cabon dioxide ambayo ni sumu kwa jamii na majani mabichi yanayochomwa yanasababisha moshi mzito ambao una madhara kwa binadamu.

Naye Ofisa Mipango Miji wa Manispaa ya Bukoba, Catres Rwegasira alisema Manispaa ya Bukoba imetenga maeneo maalumu kwa makazi na maeneo ya wazi kwa shughuli maalumu ikiwemo uvunaji wa senene.

Watu wanaoishi mjini kati wanatakiwa kuishi na kufanya shughuli zao zinazoruhusiwa kama vile biashara.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Moris Limbe alisema ukamataji wa senene utaathiri ufaulu wa wanafunzi mkoani Kagera.

“Watoto wenye umri kuanzia miaka nane hadi 18 wanakesha wakikamata senene, kuna hatari ya kupata mimba, kushindwa kuendelea na masomo wakati huu wanafunzi wa darasa la nne wakifanya mitihani ya taifa.

“Wanafunzi hao ni miongoni mwa wanaokesha mjini kukamata senene. Hivyo watoto chini ya miaka 18 na wanafunzi hawaruhusiwi kujihusisha na shughuli hizi na asubuhi hawaruhusiwi kuendelea kunyonyoa senene na kushindwa kwenda shule,” alisema Limbe.

Aliongeza kuwa tayari amepokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya walimu kuwa wanafunzi wamekuwa watoro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles