27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

UKAGUZI WA CAG SEKTA YA MADINI UWE NA BARAKA ZA WATANZANIA

WAINGEREZA wana msemo wao maarufu unaosema "There's no such thing as a free lunch." Maana yake ni kuwa, hakuna kitu cha bure. Misaada ambayo inatolewa na nchi tajiri kwa nchi masikini kama Tanzania, ni kurudisha sehemu ndogo sana ya utajiri wanaouvuna.

Inawezekana ikawa vigumu kuamini lakini ukweli ni kuwa, nchi masikini zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi tajiri bila zenyewe kufahamu. Hii ni kwa mujibu wa tafiti za kisomi.

Ripoti iliyotolewa Desemba mwaka 2015 na asasi binafsi inayojihusisha na utafiti wa masuala ya fedha duniani yenye makao yake makuu jijini Washington Marekani inayojulikana kama Global Financial Integrity, nchi zinazoendelea zilipoteza dola za Kimarekani trilioni 7.8 kati ya kipindi cha mwaka 2004-2013.

Kiasi hicho kikubwa cha fedha, kilipotea kupitia mwamvuli wa uwekezaji. Makampuni makubwa yanayowekeza katika sekta mbalimbali na hususani madini yamekuwa yakitumia mbinu mbalimbali ikiwamo ukwepaji kodi kutengeneza faida nono.

Taarifa hiyo inaeleza wazi kuwa, kiwango cha fedha kinachotengenezwa na makampuni makubwa ya nchi za magharibi na kuzipeleka kujenga nchi zao, ni kikubwa zaidi ya fedha za misaada pamoja na uwekezaji zinazotoka nchi tajiri kwenda nchi masikini.  Maana yake ni kuwa, nchi masikini zinazisaidia nchi tajiri badala ya nchi tajiri kuzisaidia nchi masikini.

Tanzania ni moja kati ya nchi nyingi barani Afrika ambazo zina rasilimali nyingi yakiwamo madini ya kila aina lakini bado imeendelea kuwa masikini.Takwimu zinaonyesha kuwa, Watanzania walio wengi ni masikini kiasi cha kushindwa kumudu milo mitatu kwa siku.

Wakati wananchi wengi wakiishi katika lindi la umasikini na wakati serikali ikihaha kuomba wafadhili kusaidia bajeti ya kuendesha nchi, makampuni makubwa ya kigeni yanaendelea kunufaika na misamaha ya kodi pamoja na kuwa ni vinara wa kukwepa kodi.

Agizo alilolitoa Rais John Magufuli kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa kina ni jambo la kutia moyo. Rais alisema pamoja na CAG kukagua pia atatuma timu ya wataalamu kwenda kukagua kwa wakati tofauti. Ni wazi kuwa ameona na kuguswa na upotevu mkubwa wa mapato pamoja na ukwepaji kodi.

Serikali zote duniani hutegemea kodi kama chanzo kikuu cha mapato ya kuendeshea nchi. Nchi tajiri duniani zimeweza kufika hapo zilipo kutokana na kuwa na misimamo mikali sana katika masuala ya kodi.

Nchi hizi hazina utani hata kidogo kwenye suala la kulipa kodi, iweje Tanzania nchi masikini iyavumilie? Haya makampuni hayathubutu kufanya yanachokifanya hapa nchini.

Msimamo wa Rais uwape ujumbe kuwa Tanzania si shamba bibi tena.

Inakadiriwa kuwa, Tanzania inapoteza mapato yanayofikia Sh trillion 2 kutokana na ‘ujanja ujanja’ unaofanywa na makampuni makubwa ya kigeni. Ukwepaji kodi nchini hufanywa na makampuni makubwa kwa njia mbalimbali ikiwamo kudanganya thamani ya mali zao, bidhaa, faida, matumizi pamoja na kutoa rushwa ili mamlaka za kodi  ziyatoze kodi ndogo.

Kutokana na hali kama hii, Tanzania imekuwa ikiendelea kutegemea wafadhili kila kukicha. Misaada ya wafadhili mara nyingi imekuwa ikiyumbisha uendeshaji wa nchi kwa kuwa haitabiriki na pia imekuwa ikija na masharti.

Wadau mbalimbali wamekuwa wakiishauri serikali kuyabana zaidi makampuni makubwa ili yaweze kulipa kodi inayostahili lakini inaonekana serikali bado haijazinduka usingizini.

Makampuni makubwa hutumia ujanja kukwepa kodi ikiwamo kuwa na mifumo tata ya kodi (complicated tax structure) ambayo huwapa mwanya wa kukwepa kodi. Pamoja na jitihada inayofanywa na serikali ya awamu ya nne, bado kuna haja ya kuyabana zaidi makampuni haya.

Ukienda sehemu zenye utajiri wa madini unaweza usiamini mcho yako kwa kuwa pamoja na utajiri uliopo, wakazi wanaozunguka migodi ni maskini wa kutupwa.

Wakati wenyeji wakiwa masikini kiasi hicho, wafanyakazi wa kigeni kwenye migodi huishi maisha kama wapo peponi huku mwishoni mwa wiki wakipata fursa ya kwenda kuwasalimu ndugu na jamaa zao kwa ndege za kukodi kwenye nchi kama Afrika ya kusini.

Fedha wanazotumia kwa matumizi ya anasa huingia kwenye matumizi ya kampuni na hivyo kuathiri kiasi cha kodi wanacholipa Serikalini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles