27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Ujirani mwema kichocheo uhifadhi Ruaha

SIDI MGUMIA, IRINGA

JAMII inayoishi pembezoni mwa Hifadhi ya wanyama na misitu inatajwa kuwa ndio washiriki wakuu wa matendo mema na mabaya yanayofanyika hifadhini.

Ukweli wa hilo unadhihirishwa na matukio mengi ya ujangili na ukataji wa miti, ambao kwa kiasi kikubwa wahusika ni wakaazi wa maeneo ya jirani kwa kushirikiana na majangili kutoka maeneo ya mbali.

Kwa muktadha huo huo ni wazi jamii hiyo inaweza kuwa kichocheo kikubwa cha kuzilinda hifadhi hizo, pamoja na kuhakikisha wanyama na mimea vinakuwa salama.

Ili kufanikisha ulinzi wa hifadhi, kumekuwa na jitihada kadhaa zinazofanywa na mamlaka zinazohusika moja kwa moja na hifadhi, hasa za wanyamapori.

Miongoni mwa jitihada hizo ni kuanzishwa kwa mtandao wa ujirani mwema, ambao unawahusisha wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi.

Ujirani mwema ni mpango wa kuwafikia wananchi waishio pembezoni mwa hifadhi kutoka ngazi ya kijiji hadi wilaya ili kushirikiana nao katika uhifadhi.

Kwa mujibu wa Mhifadhi wa Ujirani Mwema wa hifadhi ya Taifa  Ruaha, Moronda B. Moronda, mpango huo ulianza kwa majaribio mwaka 1988 kwenye vijiji vitatu vya Oloipiri, Soitsambu na Ololosokwan vilivyopo mashariki mwa hifadhi ya Serengeti.

Hadi kufikia mwaka 1994 mpango ulipanuka kwenye hifadhi zote na kuwa idara kamili.

Kwa upande wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha yenyewe ilianza shughuli za elimu ya uhifadhi mwaka 1991, kisha kushika hatamu kwenye miradi mbalimbali mwaka 1994.

Iliweza kufikia vijiji 14 vya wilaya ya Iringa katika tarafa za Idodi na Pawaga. Mpango huu umefika katika wilaya tano ndani ya mikoa mitatu na jumla ya vijiji 64 vimeweza kufikiwa na kitengo cha ujirani mwema katika huduma mbali mbali za jamii, uhifadhi pamoja na mazingira.

Moronda aliongeza kuwa miradi ya ujirani mwema inalenga kuwezesha jamii inayoishi pembezoni mwa hifadhi kushiriki katika maendeleo.

Lakini pia kusaidia jitihada za jamii katika kuboresha na kuimarisha maisha salama, kuboresha uhusiano katika maeneo ya wanyamapori na maisha ya wananchi, kukuza na kuendeleza miradi rafiki na mazingira.

Kukuza uelewa wa jamii katika athari zitokanazo na mazingira ambapo alisema ipo miradi ya ujirani iliyokwisha fanyika, miongoni mwake ikiwa ni ujenzi wa madarasa, maabara, mabwalo, mabweni, vitabu, samani za ofisi na nyumba za walimu.

Aidha pia kuna ujenzi wa miundombinu, barabara, daraja, gati za boti, uchimbaji wa visima vya maji safi na salama na tenki za maji ya kutega.

Kwa upande wa Afya Moronda alisema miradi iliyopo ni ujenzi wa zahanati, maabara, samani, vituo vya afya na nyumba za watumishi.

Pia kuna miradi ya uzalishaji maji, ufugaji nyuki, mifugo, vitalu vya miche ya miti, ujenzi wa majosho, mabirika ya kunyweshea mifugo na  malambo.

Pamoja na mambo mengine, suala la uhifadhi linakwenda sambamba na kutolewa kwa elimu juu ya namna ya kuwalinda wanyama pori na misitu bila kuyasahau mazingira kwa ujumla wake.

Elimu hiyo ya uhifadhi hutolewa ili kutatua changamoto ya elimu kwa jamii katika uelewa na ufahamu wa maliasili za taifa na mazingira, huku lengo likiwa ni kushirikiana na taasisi za serikali kutoa elimu ya uhifadhi wa maliasili za taifa na mazingira.

Katika kuunga mkono juhudi za utoaji elimu ya masuala ya uhifadhi, Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Marekani USAID chini ya mradi wake wa PROTECT kimeiona haja na umuhimu wa kutoa elimu kwa jamii juu ya masuala ya uhifadhi.

Hivyo wamekuwa wakitoa mafunzo haswa kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo ili wafahamu jinsi ya kuandika masuala yote yanayohusu uihifadhi na hifadhi zenyewe.

Kwa upande wake Afisa Utalii na Masoko wa hifadhi ya Taifa Ruaha, Antipas Mgungusi, alisema ushirikiano wa hifadhi na jamii iliyozunguka hifadhi hiyo, unasaidia kupunguza matukio ya ujangili kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wa kushirikiana na jamii zinazozunguka Hifadhi yaani kwa maana ya ujirani mwema tumekuwa tukishirikiana nao vizuri ambapo vijana wengi ambao tunawatumia hapa kama vibarua wanatoka kijiji cha jirani.

Lakini pia tumekuwa tukitoa michango yetu kwa jamii kwa kushiriki kwenye miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa zahanati, shule kupitia idara ujirani mwema.

Pia Ruaha tuna wahifadhi wakina mama kwahivyo wanapewa nafasi ni kwasababu wana uwezo, swala la jinsia halina ubaguzi kwetu.

Mgungusi alisisitiza kuwa kuhusu changamoto, alisema jamii kubwa haina uelewa wa hifadhi za Taifa na taratibu zake, kwahiyo wapo ambao wakisikia tu utalii wanadhani ni kwa ajili ya wageni kutoka nje, jambo ambalo linawasukuma kutafuta mbinu zaidi za kuielimisha jamii kwa kuwafikia majumbani, shuleni na hata kwenye maeneo ya starehe.

Naye Fredrick Funzila, Mwenyekiti wa Kijiji cha Tungamalenga anasema kwamba uhusiano uliopo kati yao na Hifadhi ya Ruaha ni mzuri na kutoa mfano wa kujengewa madarasa matatu, shule ya msingi na nyumba ya walimu.

Vile vile tunashirikiana vizuri kiulinzi na kwa upande wa tembo wanaosumbua  wananchi kwa kuvamia mashamba na kula mazao, tukiwajulisha wanakuja tunasaidiana kuwafukuza mashambani.

Funzila anaongeza kuwa wamekuwa wakipelekwa mbugani kutalii pamoja na kupewa elimu ya namna ya kuwatunza wanyamapori.

Akizungumzia ujangili, Jamal Khamis (32) ambaye ni mwanakijiji na mkulima katika kijiji cha Idodi amesema kwasasa hivi hilo halipo baada ya kuwa karibu na hifadhi wakishirikiana katika mambo mbalimbali ya kijamii lakini pia kuundwa kwa mpango wa Matumizi Bora ya Malihai Idodi na Pawaga (MBOMIPA), ujangili umepungua sana.

“Wito wangu ni tujitahidi kuwalinda hawa wanyama kwasababu sasa wakipotea ina maana kizazi kijacho hawata waona,” alisisitiza Jamal

MBOMIPA ni jumuiya ya uhifadhi wa wanyamapori ambayo kwa sasa ina jumuiya kama tano hivi na ilianza rasmi mwaka 2002.

Jumuiya hii ambayo ni Mshindi wa Tuzo la Ikweta: 2014  ilianzishwa kwa lengo la kusimamia maliasili ambazo ni wanyamapori, misitu , Maji, mawe, uoto wa asili

 zinazopatikana katika maeneo ya hifadhi kwa lengo la kukuza kipato kwa vijiji wanachama na kuzifanya ziwe endelevu.

Mapato yatokanayo na jumuiya hugawanywa kwa vijiji wanachama kwa lengo la kutumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile kama huduma ya afya, elimu na miundo mbinu.

Pamoja na jukumu la kuhifadhi wanyamapori, vile vile jumuiya inahusika na suala la kuzuia migogoro iliyopo kati ya wanyamapori na binadamu tatizo linaloonekana kukua.

Akitilia mkazo ushiriki wa jamii katika suala la uhifadhi wa wanyamapori nchini Tanzania, Josephat Kisanyage, Katibu wa Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya MBOMIPA mkoa wa Iringa anasema kuwa mapato ni makubwa sana kwa mfano mapato yanayopatikana na uwindaji wa kitalii ni milioni 60 kwa mwaka inaingia Mbomipa na ni mkataba wa miaka mitatu ambapo mwindaji analipa milioni 60 kila mwaka.

Kisanyage anaongeza kuwa, Utalii wa picha unaingiza milioni 10 kwa mwaka huku ujenzi wa mahema ‘Tented Camps’ na Utalii wa picha unaingiza milioni 70.

“Uwindaji wa wenyeji hauingizi mapato kwasababu ya mgogoro wa ukanda wa Nyalulu ambapo wananchi walivamia kwa ajili ya shughuli za kilimo, kwahiyo wastani wa fehda ni kama milioni 200 na Serikali iliandaa kanuni za kusimamia haya maeneo Tanzania nzima na sio Mbomipa tu,” alisema

“Kwahiyo 50% zinaenda kwenye vijiji na 50% nyingine inabaki Mbomipa kwa ajili ya uendeshaji kama vile askari wanaokwenda kulinda hayo maeneo, usafiri, chakula, malazi kwa mwaka mzima.”

“Huu ni mradi mkubwa sana kwa vijiji vyetu kwasababu kuna baadhi ya vijiji vinategemea ushuru wa vilabu vya pombe za kienyeji na bucha za nyama kwahivyo utakuta kwa mwaka mzima wanakusanya mapato ya wastani wa shilingi laki sita au saba lakini Mbomipa inapeleka milioni mbili mpaka milioni mbili na nusu kwa mwaka, ni mradi mkubwa sana ambao unasaidia vijiji.”

Kwa haya mapato yanayopatikana pesa zinazokwenda kwenye vijiji zinagawanya sawa sawa na kila kijiji kinaangalia kipaumbele chake ambapo wengine ni nyumba za walimu, wengine vyoo.

Kwahiyo sisi tunafuatilia kuona kama zile pesa zimefanya kazi.Sisi kama Mbomipa tuliamua kusomesha watoto yatima wapatao 42.

Kwa mujibu wa Kisanyage, kupitia ujirani mwema, TANAPA wamewasaidia sana haswa kwenye suala la doria kwa kuwapatia vifaa kwakuwa wao wanakijiji ndio tunawajua majangili na sio wao walioko hifadhini na ni kwa sabababu  hiyo watu wamekuwa wakitoa taarifa za majangili kwenye ofisi za vijijikwa mafanikio makubwa.

“TANAPA wamekuwa wakitupatia silaha kukabili ujangili lakini pia wanaendesha mafunzo na sinema na kuhamasisha wananchi katika uhifadhi wa Wanyamapori, kwasababu wanyamapori sio wa TANAPA tu ni wa watanzania wote kwahivyo baadhi ya vijiji vimeitikia  mwito na vingine vimeshindikana na ndio maana mpaka leo vitendo vya ujangili vinaendelea, umepungua tu ule ujangili wa tembo lakini ule wa samaki, asali bado unaendelea,”.

Alimalizia kwa kusema kuwa, “Mi naona Operesheni tokomeza Majangili imesaidia sana kupunguza ujangili hasa katika hifadhi za Ruaha na Mbomipa kwani siku hizi hata ukienda mbugani utaona kila kundi la tembo lina vitoto na hii maana yake ni kwamba wanazaliana na ukitaka kujua familia inaongezeka ni watoto.”

Maria Gasper (29), mkulima na mwanakijiji wa kijiji cha Tungamalenga alisema ushirikiano uliopo umewasaidia sana kujiendeleza hasa katika kulima kilimo chenye tija kwao familia zao lakini pia kijiji na Iringa kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles