30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ujerumani yaipa Tanzania ruzuku ya bilioni 330/-

Benny Mwaipaja -Dar es Salaam

SERIKALI ya Ujerumani kupitia Benki yake ya Maendeleo (KfW), imeipatia Tanzania ruzuku ya Euro milioni 127.7 sawa na Sh bilioni 330 kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji safi na salama mkoani Simiyu kutoka Ziwa Victoria.

Makubaliano ya msaada huo kupitia mikataba miwili yamesainiwa Dar es Salaam juzi na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, kwa niaba ya Serikali na Mkurugenzi wa KfW anayeshughulikia nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ulaya, Dk. Klaus Mueller.

Katika mkataba wa kwanza, kiasi cha Euro milioni 102.7 sawa na Sh bilioni 265 kimetolewa na Mfuko wa Kimataifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund) na mkataba wa pili unahusisha Euro milioni 25 sawa na Sh bilioni 65 zilizotolewa na KfW.

Mbali na mradi wa maji wa Simiyu ambao chanzo chake ni kutoka Ziwa Victoria, miradi mingine itakayonufaika na msaada huo ni kilimo endelevu cha umwagiliaji, usafi wa mazingira, maji na malisho ya mifugo na kuzijengea uwezo taasisi zitakazotekeleza mradi huo, hasa mamlaka za maji katika wilaya tano za Bariadi, Itilima, Meatu, Busega na Maswa zitakazonufaika na mradi huo.

“Kutokana na umuhimu wa mradi huo wa maji, Serikali kwa upande wake itachangia Euro milioni 40.7 sawa na shilingi bilioni 104 na wananchi watakaonufaika na mradi huo watachangia Euro milioni 1.5 sawa na shilingi bilioni 3.8 na kufanya gharama za mradi mzima kufikia zaidi ya Euro milioni 171 sawa na zaidi ya Sh bilioni 446,” alisema James.

Aliishukuru Serikali ya Ujerumani kupitia GCF na KfW kwa kutoa kiasi hicho kikubwa cha fedha kitakachotumika kutekeleza mradi huo utakaochukua miaka mitano hadi kukamilika kwake.

“Katika kipindi cha miaka mitatu, Serikali ya Ujerumani imeipatia Tanzania zaidi ya Euro 202.8 sawa na shilingi bilioni 518.5 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za afya, nishati, uhifadhi wa maliasili, udhibiti wa fedha za umma na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi,” alisema James.

Kwa upande wake, Dk. Klaus alisema hii ni mara ya kwanza kwa mfuko huo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutoa kiasi kikubwa cha fedha cha Euro milioni 102.7 kwa mkupuo katika nchi za Afrika tangu uanzishwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles