27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ujenzi bomba mafuta Uganda wanukia

Uzoefu utatokana na ule wa Ujenzi wa bomba la gesi Mtwara hadi Dar es Salaam.
Uzoefu utatokana na ule wa Ujenzi wa bomba la gesi Mtwara hadi Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu,  

Siku njema huonekana asubuhi na mwanzo wa ngoma ni lelekwani mvumilivu hula mbivu na hivyo ndio hali halisi kwa Tanzania kuwa mambo yameiva kuanza mwendo mrefu wa kufanya nchi hii kuwa kitovu cha biashara ya mafuta  na nishati katika eneo hili la Afrika Mashariki.

Kama nchi kibindoni ina hazina ya gesi asilia  ya futi za ujazo trilioni 57.2 na imeanza kufanya  maunganisho ya wenye rasilimali kwa kujenga bomba  la gesi toka Mtwara had Dar na mbioni kujenga lile la Uganda la mafuta  ghafi ya nchi hiyo ambapo watu zaidi ya 5000 wataajiriwa kufanya kazi .

Dalili za mvua ni mawingu na hivyo kitendo cha serikali ya Uganda kumilikisha kwa kutoa  leseni za uzalishaji mafuta kwa kampuni tatu za Tullow Oil, Total na China National Oil Company (CNOOC) zimefungua ukurasa mpya wa masuala ya mafuta nchini humo na eneo lote la Afrika Mashariki na kuanzisha mbio  kamili kuelekea kuzalisha mafuta katika eneo hili.

Leseni nane  zilitolewa na Uganda huku ile ya kampuni ya China ilitolewa  awali mwaka 2013 kwani ni kati ya serikali na serikali ili Uganda ipate mkopo wa dola milioni 600 za kujenga kituo cha kuzalisha umeme wa maji kwenye mlango  mmojawapo wa mto Nile

Kwa Tanzania kwa hatua hii ya Uganda maana yake ni kuwa ule mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima hadi bandari ya Tanga utafanyika na kielelezo tosha kuwa iwe tayari kwa hilo.

Kabla ya hayo nchi yetu ilitembeleewa na ujumbe wa Ufaransa  ikiwa ni ule wa serikali  ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na  ule wa kamapuni ya Total toka makao makuu kuja kufanya tathmini ya mambo na hali ya mwenendo wa mradi tarajiwa. Dola bilioni 4 sio rasilimali ndogo kwa nchi yeyote ile.

Itakumbukwa mradi huo wa bomba una umbali wa kilometa 1440 na unakisiwa kugharimu zaidi ya dola bilioni 4na hivyo kufanya kuwa ni mradi mkubwa sana wa nishati katika eneo hili.

 Kwa maelezo ya Waziri wa Nishati na Mafuta wa Uganda Irene Muloni Uganda ilitoa leseni tano kwa Tullow Oil ambayo ni kampuni iliyosajiliwa Uingereza kama tafutaji  mafuta na tatu kwa kampuni ya Total ya Ufaransa wakati  CNOOC ya China leseni moja kuanzia mwaka 2013. Mgawo wake ni kuwa Total imepewa leseni  Exploration Area One (EA1) na Exploration Area Two (EA2) kwa Tullow Oil na hivyo kurasimisha uwepo wao wa kuchimba mafuta  nchini humo na upatakanaji wa mafuta ghafi ambayo yatasafirishwa   kupitia bomba linalojengwa na Tanzania kupitia Tanzania.

Habari hizo zilipokelewa kwa shangwe na bashasha na Waziri wa Madini na Nishati wa Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo ambaye alikaribisha maendeleo hayo na kudiriki kusema kuwa Tanzania sasa itakuwa kitovu cha biashara ya mafuta kwa kule kujitokeza kwa nchi nyingine kutaka nazo kuhusika na ujenzi wa bomba hilo pamoja na kinu chakuchakata mafuta hayo  ya Uganda kwa nchi wanachama wa Afrika Mashariki.

Alisema DR Kongo inataka kushiriki ujenzi wa bomba kwa vile nao wanategemea kupitisha mafuta yao kwenye bomba hilo na vilevile wanahitaji gesi asilia toka Tanzania kwa matumizi ya nyumbani na viwanda kadiri uchumi wanchi hiyo  unavyokua kutokana na kushamiri kwa Demokrasia baada ya miaka mingi ya mapambano ya kisiasa na vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Waziri Irene  wa Uganda anasema kutolewa kwa leseni  hizo  kumekamilisha mazungumzo  makali na magumu na sasa kilichobaki ni utekelezaji  wa makusudio ya kila mmoja ambaye ni mdau wa biashara hiyo; “Na hivyo kuashiria  kuanza kwa kazi madhubuti ya mradi wetu” alisema.

Irene alisema ; “Ninategemea utoaji wa leseni hizo utafuatia na mipango kazi ya kuzalisha mafuta Uganda kwani kila kitu kipo mahali pake kama ilivyopangwa na  wadau.”

Utatu wa Total, Tullow na CNOOC  kwa pamoja  wanamiliki maeneo ya mafuta ya Uganda na leseni hizo zinadumu kwa miaka 25 na  inaweza kuongezwa tena kwa kipindi cha miaka mitano zaidi.

Lakini mambo bado hayajakamilika vilivyo wakati huu wa majaribu ambapo bei ya mafuta bado ikochini na hivyo kupunguza ari  na hamasa ya  kuwekeza kwenye sekta hiyo na hivyo basi Tullow na Total wana miezi 18 ya kufanya uamuzi wa mwisho wa kuwekeza  baada ya kupata leseni na hivyo kumfanya Waziri Irene aseme kuwa kuzalisha  petroli ghafi  kibiashara kutafanyika kuanzia mwaka 2020 ikiwa miaka zaidi ya 12 tokea mafuta yagunduliwe.

Wachunguzi wa mambo ya mafuta wanasema kuwa mafuta  Uganda yaligunduliwa miaka zaidi ya kumi iliyopita lakini uzalishaji wake umetawaliwa na mbinde kwa kucheleweshwa  haswa  na serikali kudai kupata donge nono zaidi kutoka  kwa wawekezaji kuhusu kodi na  mikakati ya uendelezaji  wa maeneo hayo. Mwishowe wamefanikiwa  kwani watu husema mtafutaji hachoki akichoka amepata!

Wakati uzalishaji utakapoanza Waziri huyo wa Uganda anasema kiasi cha mafuta  kitakachopatikana kwa siku kitakuwa  ni mapipa 200,000 hadi 230,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles