31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

UHURU WA KUJIELEZA SHAKANI-LHRC

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimesema haki ya uhuru wa kujieleza na kukusanyika iko shakani, kutokana na kuwapo kwa udhaifu katika sheria mbalimbali.

Hapa nchini uhuru wa kujieleza unalindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 18 na mikataba ya kimataifa na kikanda ambayo taifa limeridhia.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kulinda Uhuru wa Kujieleza na Kukusanyika, Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Ana Henga, alisema uhuru wa kujieleza ni muhimu kwani unaweza kulitoa taifa kutoka hapa lilipo na kuliwezesha kusonga mbele.

Kampeni hiyo imeandaliwa na kituo hicho kupitia mradi wa uhakiki kwa kushirikiana na wadau washirika ambao ni Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Baraza la Habari (MCT), Policy Forum, Twaweza, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

“Watu wengi wanaogopa kujieleza, vyombo vya habari vinafungiwa kwa ujumla hali si nzuri, uhuru wa kujieleza na kukusanyika uko katika hatihati.

“Baada ya Serikali kukataza mikutano ya kisiasa mpaka mwaka 2020 utaratibu wa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kabla ya kukusanyika umegeuzwa na kuwa si taarifa tena bali ni kuomba idhini au kibali jambo ambalo linapingana na katiba ya nchi,” alisema Henga.

Alisema wameamua kuendesha kampeni hiyo baada ya kubaini changamoto kadhaa zinazofifisha uhuru wa kukusanyika nchini ambazo ni uzuiaji holela wa mikusanyiko.

Nyingine ni mkanganyiko wa sheria, matumizi holela ya nguvu katika kutawanya mikusanyiko, kukosekana kwa utaratibu maalumu katika matumizi ya maeneo ya wazi na kukataliwa kukusanyika.

Naye Mwakilishi kutoka MCT, Paul Malimbo, alizitaja sheria kinzani kuwa ni Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya mwaka 2015 na kupendekeza zifanyiwe marekebisho kuendana na Katiba na mikataba ya kimataifa na kikanda ambayo taifa limeridhia.

Kwa mujibu wa Malimbo, sheria ya takwimu inazuia mjadala juu ya usahihi wa takwimu, inazuia watu na taasisi kuchapisha taarifa zao wenyewe na kuyumbisha uhuru wa kujieleza kwa kuwaisha watu adhabu ya kifungo na kulipa faini.

Naye Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga, alisema uhuru wa kujieleza na kukusanyika ni muhimu hasa kwa waandishi wa habari kwani huwarahishia kupata habari.

“Tunashiriki kwenye kampeni hii ili kuwafanya watu wajieleze tupate habari na kuandika, vyombo vya habari tunatakiwa tupate habari kwa serikali na watu wote sasa wasipozungumza tutakosa cha kuandika na matokeo yake tutashindwa kufanya kazi.

“Mfumo wa vyama vingi tumeukubali wenyewe kama jamii hivyo, haiwezekani baada ya miaka 25 tafiti zionyeshe serikali inabinya upinzani, si sifa nzuri kwa nchi ni lazima tuuruhusu uzungumze,” alisema Makunga.

Kampeni hiyo iliyobeba kaulimbiu ya ‘Bila uhuru wa kujieleza na kukusanyika hatuwezi kuendelea’ni ya nchi nzima na inatarajiwa kuhitimishwa Novemba mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles