23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Uhuru amweka Ruto kiporo urais 2022

ISIJI DOMINIC

SIASA za kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2022 zinazidi kumchefua Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ambaye amekuwa akisisitiza wanasiasa kuwatumikia wananchi na kuacha kupiga siasa hadi muda wa kampeni utakapofika.

Hata hivyo, ushauri huu wa Rais Uhuru ni kama unapuuzwa na wanasiasa tena wale kutoka chama tawala cha Jubilee ambao wanadai ni vigumu kutenganisha siasa na kuwatumikia wananchi.

Kundi hili ambalo wengi wanamuunga mkono Naibu Rais, William Ruto katika mbio za kuwania urais 2022 wanasema jukumu la kwanza la mwanasiasa ni kupiga siasa kwa kisingizio kuwa unaweza ukasahaulika kama hujihusishi na siasa ukisubiri muda wa kampeni.

Hii ni hoja ambayo wananchi wanapinga na kusisitiza mwanasiasa au kiongozi anayewatumikia waliompigia kura kwa kuhakikisha anasimamia miradi ya maendeleo ndiye atakayepata kura kutokana na kazi yake kuonekana kwa vitendo.

Rais Uhuru ambaye anakerwa na baadhi ya wanasiasa ndani ya Jubilee wanaomshinikiza atamke kumuunga mkono Ruto kama mrithi wake, hivi karibuni alitoa maneno ambayo yanaashiria huenda asimuunge mkono naibu wake 2022.

Akizungumza Ruto katika Kaunti ya Kiambu wakati anafungua kiwanda cha Bidco, Uhuru alisema ni Mungu pekee ambaye ataamua nani atakuwa Rais ajaye hivyo kuwataka viongozi kuacha kuweweseka na badala yake kuwahudumia Wakenya.

“Uchaguzi utakuja na Mungu ndiye hupeana uongozi. Tufanye kazi,” alisema na kauli yake ilitafsiriwa kumlenga Ruto ambaye amekuwa akizunguka maeneo mbalimbali nchini Kenya, ikitajwa ni lengo la kujitambulisha huku wafuasi wake wakisema Rais Uhuru anatakiwa kutimiza ahadi aliyotoa 2013 ambayo ni kumuunga mkono Naibu Rais.

Moja wa wafuasi sugu wa Ruto, Oscar Sudi ambaye ni Mbunge wa Kapseret, alinukuliwa akimtaka Rais Uhuru kujiuzulu akijigamba anaweza kuongoza nchi vizuri endapo Rais atamuachia kwa miezi mitatu tu.

“Ukiona Rais hawezi kukutana na viongozi, magavana na maseneta ambao wanalazimika kuandamana barabarani, ujue iko shida,” alisema Sudi akiwa nyumbani kwake Kapseret, Kaunti ya Uasin Gishu.

Kelele za baadhi ya wanasiasa wa Jubilee zinazolenga kumpigia debe Naibu Rais Ruto hususan baada ya kitendo cha Machi 9 mwaka jana, Rais Uhuru alipokutana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga na kuzika tofauti zao za kisiasa, zimekuwa zikizimwa na Uhuru ambaye amepania kutimiza ajenda nne kuu ikiwemo kupambana na ufisadi.

Kauli ya Rais Uhuru ya hivi karibuni kwamba Mungu ndiye hupeana uongozi ikionekana kukwepa kumpigia debe Ruto inakinzana kwa kiasi fulani na ile aliyowahi kusema mwaka jana akiwa ziarani Nyeri kufungua soko la Karatina.

Rais aliyeonekana kukasirishwa na wabunge wanaoteka eneo lake la ubunge muda mwingi kutumia kujadili siasa za 2022 badala ya kufanya mambo ya msingi yanayogusa wananchi, alisema chaguo la mrithi wake litawashangaza wengi.  

“Wanafikiri kwa sababu Uhuru ataenda nyumbani 2022, hatakuwa na neno la kusema kuhusu nini kitakachotokea. Ninawaambia wakati muda muafaka ukifika, nitakuwa na kitu cha kuzungumza,”alisema Rais Uhuru katika mkutano wa hadhara.

“Wengine wanafikiri nimenyamaza kwasababu siwezi kuongea kuhusu siasa. Mimi bado ni mwanasiasa. Watashangaa chaguo langu muda huo utakapofika, lakini kwa sasa nataka nijihusishe na kutekeleza ahadi nilizotoa kwa Wakenya.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles