26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Udongo unaovimba au kusinyaa ni hatari

Nyumba iliyojengwa mlimani.
Nyumba iliyojengwa mlimani.

Na MHANDISI CHARLES OGARE,

WIKi iliyopita tulikuwa tukiangalia athari za kujenga nyumba karibu na miti.

Kabla ya kujenga nyumba au kununua kiwanja unapaswa kuangalia kwa makini eneo hilo ili lisije kukupa shida hapo baadaye.

Wiki hii tutamalizia pale tulipoishia wiki iliyopita na kuangalia athari za kujenga nyumba kwenye udongo usiofaa. Pia tutaangalia eneo zuri linalofaa kwa ujenzi wa nyumba. Sasa endelea…

Kama unajenga karibu na mti au miti iliyokatwa, subiri mpaka unyevunyevu wa ardhi urudie hali yake ya kawaida (muda wa miezi sita hadi miaka miwili) halafu ujenge, au itabidi utumie aina fulani ya ujenzi wa misingi ya majengo yenye uwezo wa kuhimili mabadiliko hayo ya unyevunyevu kwenye ardhi.

Kumbuka

Udongo wa mfinyanzi huongezeka ukubwa (huvimba) unapopata maji na kusinyaa unapokauka. Jengo hunyanyuliwa juu wakati udongo unapovimba na hutitia wakati udongo unaposinyaa. Kuna aina nyingi ya udongo wa mfinyanzi na kila aina inatofautiana na aina nyingine katika kuvimba au kusinyaa kutokana na kiasi cha unyevunyevu kwenye ardhi husika.

Kuondolewa kwa maji kutoka kwenye udongo (hasa wa mfinyanzi) kwa kunyonywa na mizizi ya miti husababisha udongo kuongezeka au kupungua ujazo (kusinyaa) kwa kiasi cha milimita 40 au zaidi kati ya kipindi cha kiangazi na masika.

Udongo (hasa wa mfinyanzi) huvimba wakati miti iliyomo inapokatwa kwa sababu mizizi hukomaa kuchukua maji kwenye ardhi na hivyo kusababisha ongezeko la kiasi cha unyevunyevu kwenye udongo huo.

Kuvimba au kusinyaa huko kwa udongo ni hatari kwa misingi ya nyumba na huweza kusababisha nyufa kwenye nyumba.

Nyumba iliyojengwa kwenye mtelemko.
Nyumba iliyojengwa kwenye mtelemko.

 

Ardhi yenye mtelemko (sloping ground)

Unapojenga nyumba kwa kutumia msingi wa kawaida wa stripu (strip foundation) kwenye ardhi yenye mtelemko mkali jaribu kujenga nyumba kwa kukata mtelemko wa ardhi hiyo (yaani urefu wa nyumba ukate mtelemko). Kama ardhi ni ya udongo wa mfinyanzi ulioinama kwa zaidi au karibu ya 1/10, au kama udongo ulio na mtelemko uko juu ya ardhi yenye mwamba  kwa chini, basi udongo huo ni hatari kwa misingi ya nyumba kutokana na tabia ya udongo kunyinyirika kufuata mtelemko. Hii itafanya sehemu moja ya nyumba kudidimia na kuweza kusababisha nyufa kwenye nyumba. Ni vizuri kama mtelemko wa ardhi ni mkubwa umwone mhandisi mtaalamu wa masuala ya majengo kwa ushauri kabla ya kujenga kwenye ardhi kama hiyo.

Mahali palipokuwa na shimo la takataka au udongo wa tifutifu

Eneo kama hili lina hatari kubwa sana ya udongo kutitia na nyumba kudidimia wakati wa kujenga na baada ya kujengwa. Ni vizuri kumwona mhandisi wa masuala ya majengo kabla ya kuamua kujenga nyumba katika eneo kama hili. Usijenge nyumba wakati nusu ya nyumba ipo kwenye sehemu ngumu ya ardhi au mwamba na nusu nyingine kwenye udongo debwedebwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles