28.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

UDHIBITI WAHAMIAJI ULIANZISHWA KUKABILI WAAFRIKA KUDAI UHURU

Na LEONARD MANG’OHA



IDARA ya Uhamiaji ni moja ya vyombo vya ulinzi na usalama nchini, yenye majukumu ya kuwezesha na kudhibiti uingiaji, utokaji wa watu na ukaazi wa wageni nchini. Jukumu jingine ni kutoa huduma ya pasipoti, hati nyingine za safari kwa raia wenye sifa na kuratibu mchakato wa maombi ya uraia wa Tanzania kwa wageni wanaoishi nchini.

Udhibiti wahamiaji nchini ulianza rasmi mwaka 1924 baada ya kutungwa sheria ya kwanza iliyoitwa ‘Immigration Ordinance’ 1924; iliyolenga kusimamia masuala ya uhamiaji ndani ya Tanganyika, wakati huo ikiwa chini ya utawala wa Wajerumani na ilianza kutumika rasmi Februari mosi, 1925.
Kuanzia wakati huo hadi mwaka 1948, shughuli za udhibiti wa wahamiaji na utoaji wa pasipoti zilifanywa na kitengo maalumu ndani ya idara ya Polisi.
Idara ya Uhamiaji ilianzishwa rasmi Julai 13, 1949, lakini iliendelea kuwa chini ya Kamishna wa Polisi kutokana na uchache wa watumishi hadi alipoteuliwa rasmi Ofisa Uhamiaji Mkuu kuongoza idara hiyo. Oktoba mwaka 1949 ilibadilishwa jina na kuitwa Idara ya Uhamaiji na Pasipoti.
Kuanzishwa kwa idara hii kulilenga kuimarisha udhibiti wa wageni waliokuwa wakiingia ndani ya koloni la Tanganyika chini ya utawala wa Kiingereza, hususan Wazungu waliokuwa na makoloni mengine ndani ya Afrika pamoja na raia wa mataifa rafiki zao.
Katika kipindi hicho, Waafrika waliruhusiwa kutoka sehemu moja hadi nyingine bila udhibiti kutokana na mahitaji ya wafanyakazi ‘manamba’ kwenye mashamba ya wakoloni.
Pia udhibiti huo ulilenga kukabiliana na kuenea kwa harakati za kudai uhuru katika baadhi ya mataifa ya Afrika katika miaka ya 1950, ambapo baadhi ya makabila kama ya Wakikuyu, Wakamba na Wajaluo kutoka Kenya walidhibitiwa kuingia ndani ya koloni la Tanganyika.
Jukumu la idara hii kabla ya uhuru ilikuwa ni kudhibiti uingiaji na ukaazi wa wageni katika ndani ya Tanganyika pamoja na kutambua raia wa Uingereza. Baada ya uhuru, Desemba 9, 1961, iliendelea kuitwa Idara ya Uhamiaji na Pasipoti huku majukumu yake yakiongezeka na kufanyika mabadiliko ya sheria.
Idara hii iliendelea kufanya majukumu yake yaliyorithiwa na Tanganyika huru, huku baadhi yakiongezeka ambayo ni pamoja na utoaji wa Visa kwa wageni walioomba kuingia Tanganyika kwa shughuli mbalimbali ikiwamo kufanya misako, doria na shughuli nyingine za upelelezi.
Wakati huo idara hiyo ilikuwa ikitekeleza majukumu yake kwa kuongezwa na sheria ya Uraia namba 3 ya mwaka 1961 na Sheria ya Uraia ya Mwaka 1961 ambazo zinafutwa na Sheria namba 6 ya mwaka 1995.
Baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, majukumu ya yake yaliendelea yaleyale, isipokuwa shughuli zilipanuka kijiografia.
Kwa Tanzania Bara, utendaji kazi wa idara kuhusu masuala ya uraia uliendelea kusimamiwa na sheria ya Uraia namba 3 ya Mwaka 1961 na sheria ya Uraia ya Mwaka 1962, Zanzibar, masuala ya Uraia yalisimamiwa na Sheria ya Uraia ya Zanzibar ya 1952 ambayo ilifutwa na Sheria ya Uraia ya mwaka 1964.
Masuala ya uhamiaji na uraia yalifanywa kuwa ya muungano mwaka 1964. Ilipofika mwaka 1995 sheria zilizokuwa zinasimamia majukumu ya uhamiaji Tanzania Bara na Zanzibar zilifutwa na kutungwa sheria mpya ya Uhamiaji namba 7 ya mwaka 1995 na kanuni zake zilizotungwa mwaka 1997 pamoja na kuboresha huduma za pasipoti, ambapo mwaka 2002 ilitungwa sheria ya kusimamia utoaji wa pasipoti na hati za safari na baadaye kanuni zake zilitungwa mwaka 2004.
Kutokana na uchache wa watumishi, shughuli zote zilizohusu masuala ya uhamiaji nje ya Dar es Salaam ziliendelea kufanywa na wakuu wa wilaya na maofisa wa polisi katika vituo vya Tanga, Lindi, Tabora (Airport), Mbeya, Kigoma, Urambo (Airport) na Mikindani.
Pia kwa kutumia utaratibu maalumu uliowekwa kati ya ofisa uhamiaji mkuu na utawala wa majimbo, wakuu wa wilaya au maofisa wa wilaya waliruhusiwa kufanya shughuli za uhamiaji katika vituo vya Pangani, Kilwa, Bagamoyo na Ngara mkoani Kagera.
Baada ya muungano, idara ya uhamiaji ilifanywa kuwa miongoni mwa idara ya muungano, chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Idara idara hii kwa sasa ina ofisi katika mikoa yote ya Tanzania, ofisi za wilaya 36 na vituo 54 vya kuingia na kutoka nchini katika maeneo ya mipaka na nchi jirani ikiwamo Namanga, Lusumo, Sirari na Tunduma.
Mwisho…

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles