24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

UCSAF YAPEWA SIKU 14 KUREKEBISHA HALI YA MAWASILIANO PEMBA


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye ameupa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) wiki mbili kwenda Pemba kukagua hali ya mawasiliano ya simu za mkononi na kuwasilisha taarifa hiyo kwake.

Nditiye ameyasema hayo akiwa kwenye ziara Zanzibar kukagua hali ya mawasiliano kisiwani humo na kutembelea taasisi za mawasiliano zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambapo suala la mawasiliano ni la muungano.

Nditiye amesema kuwa amepokea taarifa kutoka kwa wabunge wa Kisiwa cha Zanzibar kuwa hali ya mawasiliano kwenye kisiwa hicho si nzuri na sehemu nyingine hakuna mawasiliano licha ya kuwa kuna minara ambayo inatoa huduma za mawasiliano ila kutokana na jiografia ya Pemba ambapo kuna milima na mabonde mawasiliano si ya uhakika.

“Nawaagiza muende Pemba mkaainishe maeneo yote ambayo hayana mawasiliano na muwasilishe taarifa hiyo ofisini kwangu baada ya wiki mbili,” amesema Nditiye.

Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Ofisi ya Zanzibar, Esuvatie-Aisa Masinga akiwasilisha taarifa yake amesema majukumu ya ofisi yake ya usimamimizi na udhibiti wa mawasiliano na posta, amekiri kuwa yapo baadhi ya maeneo Pemba na Unguja ambapo hali ya mawasiliano  hairidhishi.

“Pemba kuna maeneo ambayo hakuna mtoa huduma na pale ambapo mawasiliano yapo bado ubora wa huduma si nzuri, na baadhi ya maeneo kama yanayoathirika na huduma hiyo ni Kengeja na Chokochoko na kwa upande wa Micheweni ni Konde na Gando.

“Ili kufanya mawasiliano yawe mazuri kwa Pemba, ni muhimu ‘site’ zikaongezwa hasa ukizingatia hali ya kijiografia ya kisiwa hicho,” amesema Masinga.

Naye mwakilishi wa UCSAF, John Munkondya amesema Mfuko huo utakwenda Pemba kukagua hali ya mawasiliano na kuwasilisha ripoti ofisini kwake ili wananchi wa maeneo hayo wapate mawasiliano ya uhakika.

“Sisi kama UCSAF tumechukua taarifa hii ya maeneo ambayo hayana mawasiliano, tutakwenda Pemba kukagua na maeneo hayo yataingizwa kwenye utaratibu wa kanda maalumu ili tuweze kufikisha mawasiliano,” amesema Munkondya.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles