24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

UCHUNGUZI WABAINI MAKONDA KUVAMIA CLOUDS

ASHA BANI na MILLE ABDUL (TURDACO) – dar es salaam

RIPOTI ya uchunguzi ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), imegongelea msumari sakata la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuvamia studio za kampuni ya habari ya Clouds Media Group (CMG), ambayo imeonyesha kuwa ni kweli alifanya uvamizi, hivyo aombe radhi.

Jopo lililofanya uchunguzi huo, linajumuisha polisi mstaafu, wakili wa Mahakama Kuu na mwandishi wa habari.

MCT imetoa ripoti hiyo ikiwa ni siku chache tangu Makonda aseme kamwe hatoomba radhi juu ya suala hilo.

Tukio la uvamizi wa Clouds, lililotokea Machi 17, mwaka huu, lilizua mjadala uliofanya aliyekuwa Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye, kuunda kamati ya kuchunguza ambayo nayo ilikuja na matokeo ya kuwa mkuu huyo wa mkoa alivamia studio hizo.

Akisoma ripoti hiyo jana mbele ya waandishi na wadau wa habari, mwandishi mkongwe na Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Juma Thomas, alisema ripoti imebaini ukiukwaji wa uhuru wa vyombo vya habari na uhariri.

“Kuvamia studio za Clouds Media Group akiwa na walinzi wenye silaha, lilikuwa ni tendo lililo kinyume cha haki za binadamu na utawala bora, lilikuwa ni ubabe ambao haukubaliki katika nchi yoyote inayoheshimu na kufuata misingi ya kidemokrasia.

“Uvamizi wa studio za Clouds Media Group, kwa kutumia walinzi wenye silaha, ulikuwa kinyume na vigezo vya utalawa bora. Makonda amedhalilisha Jeshi la Polisi, hivyo ni lazima awaombe radhi Watanzania.

“Makonda lazima akiri kuwa kitendo chake kilikuwa cha ukiukwaji wa haki za msingi za waandishi wa habari na uhuru wa vyombo vya habari,” inasema ripoti hiyo.

Thomas aIisema timu ya uchunguzi ya MCT ilibaini Makonda alikuwa na uhusiano wa kirafiki na wafanyakazi wengi wa CMG kuanzia ngazi za chini hadi juu.

Alisema wamejiridhisha kuwa Makonda alivamia studio hizo saa 4:30 usiku wakati wa kipindi cha Shilawadu kikiwa kwenye mapumziko na hewani yalikuwa yanarushwa matangazo ya biashara.

Thomas alisema mlinzi aliyejitambulisha kwa tume kuwa ni Thomas Mwakipesile, aliwaeleza kwamba hawakuwahi kumwona Makonda akiingia katika studio hiyo na askari, licha ya kuwa alikuwa mara kwa mara anafika hapo.

Alisema timu imethibitisha bila shaka yoyote kwamba walinzi waliofuatana na Mkuu wa Mkoa wakati wa uvamizi wa studio, walikuwa kutoka Jeshi la Polisi.

MAKONDA AIKACHA TIMU YA UCHUNGUZI

Thomas alisema licha ya kumpa Makonda haki ya kusikia upande wake, walifika ofisini kwake mara tatu na wakamwandikia pia barua, lakini hakutoa ushirikiano.

“Kama ilivyokuwa kwa timu ya uchunguzi ya Nape, juhudi za timu ya MCT kukutana na Makonda hazikufanikiwa, timu iliamua kumwandikia barua kiongozi huyo, ikitoa sababu za umuhimu wake kukutana naye, barua haijajibiwa hadi leo na ndio tukaamua kuitoa ripoti hiyo,” alisema Thomas.

 MAHOJIANO NA WAFANYAKAZI WA CLOUDS

Alisema timu hiyo ilitembelea Studio za Clouds Media na kufanya mahojiano na wafanyakazi husika na kubainika kuwa walipigiwa simu na mtu asiyejulikana na kuwaambia kuna mwanamke anayedai kuzaa na Askofu Gwajima na kwamba alizuiwa kuingia ndani kwa askofu huyo huko Mbezi SalaSala.

Wakili Thomas alisema kutokana na hilo, ndipo watangazaji wa kipindi cha Shilawadu walifika kwenye tukio na kufanya mahojiano na mwanamke huyo.

Alisema waandishi hao walisema baada ya mahojiano na mwanamke huyo, waliona si vyema kurusha kipindi bila kutafuta mtuhumiwa apate nafasi ya kujieleza.

Mtangazaji wa kipindi cha Shilawadu, Soudy Brown, aliiambia tume kuwa Makonda alipokuwa ndani ya studio, aliwaambia kama hawataitangaza habari ya mwanamke huyo, basi atawafunga jela miezi sita.

HATUA ZA CLOUDS

Ripoti hiyo inasema baada ya tukio hilo, Mkurugenzi wa Vipindi wa CMG, Ruge Mutahaba, aliieleza tume hiyo kuwa Makonda anatakiwa kuomba radhi, lakini kinyume na matarajio hayo amekataa kufanya hivyo.

Alisema tayari wameripoti tukio hilo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni.

Timu ya MCT imelaani kitendo cha maaofisa wa TCRA, kujitoa katika hilo na kusema kesi hiyo ni ya kipolisi na kwamba haiwahusu wao.

TUME YA HAKI ZA BINADAMU

Alisema kamati hiyo ilifanya mahojiano na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRGG), Bahame Nyanduga, ambaye alisema kitendo cha uvamizi kilichofanywa na Makonda ni kinyume na kipengele cha 18 cha Katiba ya mwaka 1977 kinacholinda uhuru wa maoni na uhuru wa kujieleza.

MAPENDEKEZO

Katika mapendekezo yake, timu hiyo imesema kuwa na uhusiano na wanasiasa na watendaji wengine kunatakiwa umakini.

Pia wamekitaka chumba cha wahariri wa Clouds kiwe maalumu kwa wahariri wenye wajibu nyeti wa kuhariri habari na mahali ambako maamuzi muhimu yanafanyika, hivyo asiruhusiwe mtu mwingine yeyote kuingia.

“Pia utaratibu wa uandishi unaonyesha kwamba habari zinapofika katika dawati la mhariri, hiyo haiwi tena mali ya mtu kama ambavyo amefanya Makonda kuingia na kuhariri vipindi vyake, CMG wawe makini lisijirudie,” ilisema ripoti.

Mbali na Thomas ambaye alisoma ripoti hiyo jana, wengine waliokuwa wakiiunda ni mwanahabari mkongwe, Hawra Shamte, polisi mstaafu mwenye uzoefu wa masuala ya usalama, Maximinus Ubisimbali na Ofisa Programu Mwandamizi wa MCT ambaye pia alikuwa kiongozi wa timu hiyo, Ustus Mkinga.

TEF

Katika hatua nyingine, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limetoa tamko kuelezea mkutano wake mkuu maalumu uliofanyika Agosti 13, mwaka huu na kusema limebaini mkutano wake na Makonda uliofanyika juma lililopita, ulikuwa na kasoro kubwa.

“Baada ya kutafakari na kutathmini mwenendo wa mkutano huo, jukwaa lilibaini kuwepo kwa kasoro kubwa wakati wa mchakato wa kurejesha uhusiano wa kikazi kati ya vyombo vya habari na kiongozi huyo ambaye habari zake zilizuiliwa kuripotiwa kwa takribani miezi mitano.

“Katika mkutano huo (wa Agosti 13), viongozi wa TEF walikiri kosa na kuomba radhi kwa kuitisha mkutano wa waandishi wa habari kabla ya kupata idhini ya mkutano mkuu na hivyo kusababisha kujengeka taswira mbaya ya kiuwajibika kwa jukwaa na vyombo vya habari hususani wahariri,” inasema taarifa hiyo.

Katika maazimio yake, inasema jukwaa hilo limetoa onyo kwa viongozi wa TEF kutorudia kosa hilo la kiuwajibikaji, kikanuni na kitaratibu.

Katika azimio la pili, uongozi umetakiwa kila panapotokea suala kubwa kama hili ambalo lilishafanyiwa uamuzi na mkutano mkuu kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kihabari, lirejeshwe kwa wanachama kabla ya hatua za mwisho kuchukuliwa.

“Jukwa la Wahariri linapenda kuwahakikishia wanahabari na wananchi wote kwa ujumla kwamba litaendelea kutimiza wajibu wake wa kitaaluma na halitasita kuchukua hatua stahiki kwa kiongozi au mtu yeyote atakayeonekana kutishia usalama wa wanahabari, uhuru wa uhariri na wa vyombo vya habari,” linasema tamko hilo lililosainiwa na Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya TEF, Wallace Mauggo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles