Uchunguzi ajali ya Mv Nyerere waanza

0
1526

TUMELIOPOA: Gari aina ya Canter lililokuwa  ndani ya kivuko cha MV Nyerere kilichopinduka katika Ziwa, likiopolewa jana .PICHA NA PETER FABIAN.

NA PETER FABIAN, UKEREWE.

TUME ya kuchunguza tukio la ajali ya Kivuko cha Mv Nyerere iliyoteuliwa na Rais Dk. John Magufuli jana imeanza kazi yake rasmi wilayani Ukerewe, Mwanza jana kwa muda wa mwezi mmoja.

Akizungumza mjini hapa jana, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, alisema tume hiyo yenye wajumbe saba itakayokuwa chini ya Mwenyekiti wake, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama mstaafu, Jenerali George Waitara, imeshafika Mwanza na kuelekea Ukerewe hadi kisiwani Ukara kulikotokea tukio la ajali Alhamisi wiki iliyopita na kusababisha abiria 228 kupoteza maisha na mali zao huku manusura 41 wakiokolewa wakiwa hai.

Kamwelwe ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Kivuko cha Mv Nyerere alisema tume hiyo imepewa jukumu la kufanya uchunguzi wa kina kisha watawasilisha taarifa kwa Magufuli na baadaye Serikali itatoa taarifa kwa wananchi.

“Wananchi wa Ukerewe, Ukara na Watanzania kwa ujumla mwendelee kuwa watulivu kama mlivyonyesha wakati wote kulipotokea tukio hili, lakini tunaomba muipe tume ushirikiano wa kuwezesha kufanikisha majukumu yao watakapokuwa Ukerewe na kisiwani hapa Ukara watakapohitaji kuongea nanyi,” alisema.

Pia aliyataja majina ya wajumbe wa tume hiyo kuwa ni Selina Magesa (Mtendaji Mkuu mstaafu wa Temesa), Julius Kalolo (Wakili), Queen Mlozi (Katibu wa UWT), Camilius Wambura, Bashir Hussein (Ofisi ya Waziri Mkuu-maafa) na Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi (Chadema).

“Tunaipisha tume ya uchunguzi kuanza kufanya kazi yake kama ilivyoelekezwa na Rais na kila shughuli ya uopoaji vifaa ndani ya maji Ziwa Victoria imefungwa leo (jana) rasmi na kubwa tunawashukuru wadau mbalimbali mlioshirikiana na Serikali katika ajali hii iliyoacha majonzi makubwa,” alisema.

Wakati tume hiyo ikianza kazi, shughuli kuopoa gari aina ya canter ya tani mbili na nusu, pikipiki moja, baiskeli moja na viroba viwili vyenye vifaa vya umeme jua mali ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) vilivyopakiwa katika gari lililoopolewa vikiwa vinapelekwa Ukara kwa ajili ya mradi wa umeme wa jua ulioanza kutekelezwa kisiwani humo.

Kazi ya uopoaji vifaa hivyo ilianza jana saa nne asubuhi chini ya Mkuu wa Jeshi la Wanamaji (Navy Kamanda), Meja Jenerali Rashid Makanzo na kufanya ukaguzi katika Kivuko cha Mv Nyerere ili kujiridhisha endapo kama kuna miili ndani yake lakini haikukutwa pia kuondoa maboya ya kujazwa upepo yaliyotumika kukigeuza na kuinuka kabla ya kuvutwa nchi kavu juzi jioni.

“Tuliahidi kukamilisha kazi hii ya uopoaji vifaa uliofanywa na wazamiaji na askari wa JWTZ wanamaji, nchi kavu, polisi na jeshi la akiba (mgambo) waliofanya kazi hiyo kwa saa nne huku wafanyakazi wa Chama cha Msalaba Mwekundu wakifanya usafi katika kivuko hicho ili kukikabidhi kwa uongozi wa Tamesa,” alisema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, alisema ulinzi katika eneo kilipo kivuko hicho litakuwa chini ya JWTZ lakini litatoa ulinzi kwa tume iliyoteuliwa na Rais ili kuwezesha kukamilisha majukumu yake.

 MICHANGO MFUKO WA MAAFA

Kamwelwe alitoa taarifa ya kupokea michango mbalimbali kabla ya muda uliowekwa na kamati ya maafa kitaifa kufungwa na alikabidhiwa hundi ya Sh milioni 50 kutoka Kampuni ya Songas iliyokabidhiwa na Meneja Rasilimali Watu, Agatha Keenja. Hundi nyingine ya Sh milioni 80 ilikabidhiwa na Richard Ojendo ambaye ni Meneja Jamii Endelevu kutoka Kampuni ya Acacia inayomiliki Mgodi wa North Mara.

Pia alipokea mchango wa Sh milioni 10 kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar iliyokabidhiwa na Mwenyekiti wake, Mwanaasha Hamis Juma huku akitoa taarifa ya michango ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kutoa Sh milioni 86 iliyochangwa na wabunge wakiwamo wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki lililochangia Sh milioni 8.5 na tayari imeishasomeka katika akaunti.

Aliitaja michango mingine na tayari fedha zake imeingizwa katika Akaunti ya Maafa iliyofungulia Benki ya NMB tawi la Kenyatta Road, Mwanza ni Sh milioni tano za Benki ya Azania Tanzania zilizowasilishwa na Bernadetta Makigo ambaye ni Meneja wa benki hiyo tawi la Rock City na Kampuni Rex Energy (Dodoma) imetoa vifaa vya sola vyenye thamani ya Sh milioni 35 ambavyo vitafungwa Kituo cha Afya Bwisya Ukara.

Pia alisema uchangiaji wa fedha hizo umehitimishwa rasmi kupokelewa saa tisa alasiri wakati akitoa taarifa ya mwisho ya michango na kupokea taarifa ya hitimisho la uopowaji vifaa vya umeme, gari, baiskeli na pikipiki ikiwamo ukaguzi wa ndani ya Kivuko cha Mv Nyerere ambalo nalo umehitimishwa rasmi jana.

Pia alihitimisha kwa kutoa taarifa ya kiasi cha fedha zilizomo katika akaunti kuwa ni Sh 725,625,595.

“Mongela tumieni vijana wa Suma JKT kujenga majengo haya na utaratibu wa kufanya ununuzi wa vifaa vya ujenzi kutumia force akaunti kwa umakini na weledi badala ya kusubiria kutangaza zabuni ambapo utaratibu huo utachelewesha,” alisema.

 Kivuko Mv Ukara na Mv Sabasaba

Katika hatua nyingine, alisema tayari wizara imeuelekeza uongozi wa Temesa kukifungia injini Kivuko cha Mv Ukara na kufanyiwa majaribio ikiwamo ukaguzi ili kuanza kutoa huduma ya usafiri kati ya Bugorola Ukerewe.

“Natoa rai kwa wasimamizi na wafanyakazi kwamba Kivuko cha Mv Ukara kinao uwezo wa kubeba abiria 70 tu bila mizigo hivyo mzingatie hilo ili kuepusha majanga kama hili lililotokea Bwisya, lakini tuna kikarabati kwa kukifungia injini na polopela Kivuko cha Mv Sabasaba chenye uwezo wa kubeba abiria 300 na magari ambacho tayari Rais Magufuli ameshatoa maelekezo na fedha ya kununulia injini na polopela ili nacho kije kuungana na MV Ukara kutoa huduma hapa,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here