24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

UCHU WA MADARAKA JINAMIZI KWA VIONGOZI AFRIKA

Na Balinagwe Mwambungu,

BAADHI ya viongozi wa Kiafrika wamekuwa ving’ang’anizi kama luba. Wakishaingia madarakani hawataki kuondoka, wako tayari kufanya chaguzi kwa gharama kubwa (ili kuwaridhisha wakubwa wa nchi za Magharibi), kwamba wanafuata misingi ya demokrasia huku wakiiba kura ili waendelee kutawala.

Ni nchi chache katika Afrika ambazo zimeweza kuendesha chaguzi za wazi na kufanikisha kubadili uongozi. Ghana inapigiwa mfano, imebadili uongozi wa juu mara tatu kupitia sanduku la kura. Jerry Rawlings alikuwa Rais wa kwanza kuondoka madarakani kwa hiyari. Akafuatiwa na John Mahama ambaye chama chake cha National Democratic Congress kilishindwa kwenye uchaguzi mkuu na kumwachia madaraka Rais wa sasa, Nana Akufo-Addo.

Nigeria ni nchi ya pili kuendesha uchaguzi huru na wa haki baada ya kustaafu Rais Olusegun Obasanjo, alimwachia kiti Goodluk Jonathan ambaye alikubali kushindwa kwenye uchaguzi mkuu na Jenerali Muhammad Buhari.

Nchi nyingine ambazo zimebadilisha utawala kwa njia ya kura ni pamoja na Malawi. Rais wa maisha, Dk. Hastings Kamuzu Banda, alishindwa kwenye uchaguzi wa mfumo wa vyama vingi na Bakili Muluzi ambaye kipindi chake kilipokwisha pia aliachia ngazi.

Tanzania ni nchi pekee ambayo ina marais wastaafu wengi kwa kuwa inafuata Katiba yake kwa dhati. Rais anaruhusiwa kugombea kwa vipindi viwili tu vya miaka mitano akitaka. Lakini Katiba iko kimya kuhusu rais mstaafu kurudi kwenye madaraka baada ya miaka mitano.

Katika nchi nyingine, kwa mfano Senegal, Rais Mstaafu, Abdoulaye Wade (90), ametangaza kuwa atagombea ubunge katika uchaguzi ujao pamoja na kwamba ana umri mkubwa. Viongozi wengine ving’ang’anizi ni Yoweri Museveni (73) wa Uganda na Joseph Kabila (47) wa DR Congo, walidiriki kubadilisha Katiba ili waendelee kutawala.

Museveni sasa anataka Katiba ibadilishwe tena kwa kuondoa kifungu kinachomzuia mtu mwenye miaka zaidi ya 75 kugombea urais.

Museveni ambaye hakuingia madarakani kwa njia halali, alishiriki kumpindua Iddi Amin na Milton Obote kisha kulibadilisha jeshi lake la msituni NRA (National Resistance Army) na kulifanya vuguvugu la kisiasa National Resistance Movement (NRM).

Museveni pamoja na kutangaza mwaka 2001 kwamba hatagombea tena, akagombea mwaka 2006 na anaendelea kutawala.

“Mzee huyu ambaye aliiokoa nchi, kwanini unataka aondoke? Nawezaje kuacha shamba la migomba nililopanda mwenyewe wakati linaanza kuzaa ndizi,” anasema Museveni.

Aliyekuwa Rais wa Marekani, Barrack Obama, aliwahi kuwaambia viongozi wa Kiafrika: “Asiwepo mtu wa kuwa rais wa maisha. Nchi zenu zitakuwa kiuchumi kama mnawaachia uongozi vijana wenye damu mpya na mawazo mapya.

Mimi bado ni kijana, lakini najua fika kwamba mtu mwingine mwenye nguvu na mawazo mapya ataifaidisha nchi yangu.”

Maneno hayo murua hayakuwaingia akina Robert Mugabe (93), ambaye pamoja na kuugua ugonjwa utokanao na umri mkubwa, (senility), bado anasema atagombea urais mwaka 2018!

Marais wa Afrika waige mfano wa Joachim Chisano na Amando Guebuza (Msumbiji), Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, wote wa Tanzania ambao waliheshimu Katiba na kung’atuka.

Kenneth Kaunda (Zambia), Bakili Muluzi (Malawi), Joyce Banda (Malawi), Daniel Arap Moi na Mwai Kibaki (Kenya), walikubali kuachia madaraka muda wao ulipofika kama ilivyokuwa kwa Festus Mogae (Botswana) na Sam Nujoma (Namibia).

Viongozi wasisubiri yawakute yaliyowakuta Hosni Mubarak (Misri), Blaise Compaore (Burkina Faso), El Abidine Ben Ali (Tunisia), Muammar Gadaffy (Libya), Joachim Opango (Congo) na wengineo ambao waliondolewa madarakani kwa nguvu.

Jose Edward dos Santos ameitawala Angola tangu  mwaka1979, amesema hatagombea tena nafasi ya rais katika uchaguzi ujao (2018) kama hataiga mfano mbaya wa Rais Museveni.

King Mohamed II (Morocco), King Muswati III (Lesotho) na King Letsie (Swaziland), ni watawala wa jadi, lakini Abdelaziz Boutefrika (Algeria), Dennis Nguesso (Congo), Isaias Afweki (Eritrea), Omar Al Bashir (Sudan), Idriss Deby (Chad), Paul Biya (Cameroon), Teodor Obiang Nguema (Equatorial Guinea), wamekuwa madarakani kwa muda mrefu na hawana mpango wa kustaafu.

Hawa wanaweza kuitwa ni walevi wa madaraka, maana wataalamu wanasema jinsi kiongozi anavyokaa madarakani kwa muda mrefu, uwezo wake wa kufikiri na kutenda au kuamua mambo mazito ya nchi, unazidi kupungua. Mambo mengine huwa yanampita bila kujua na watu wajanja wanaamua kwa niaba yake na kumficha asiyajue.

Marie Antoinette aliyekuwa Malkia wa Ufaransa, alipoona maandamano makubwa jijini Paris, aliwauliza wasaidizi wake kwanini watu wanaandamana. Akajibiwa kwamba walikuwa hawana mkate. Akashangaa na kuwajibu: “Kwanini wasipewe keki?”

Mtu akiingia Ikulu atafanya yale yaliyokuwa yanamkera au kurekebisha wenzake walipoptoka, lakini jinsi muda unavyokwenda, vipaumbele vyake vinabadilika.

Mifano hai ni ya marais wetu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin William Mkapa na Jakaya Mrisho Kikwete, wote walifanya kazi nzuri katika kipindi cha kwanza lakini kipindi cha pili au cha ‘lala salama’, waliacha bora mambo yaende.

Ndio maana ilikubalika kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ataongoza kwa mihula miwili tu.

Wananchi wanafurahia Rais John Magufuli anavyofanya kazi na kufikiri kwamba akipewa muda mrefu zaidi ataweza kuipeleka nchi mbali zaidi kimaendeleo.

Miaka 10 iliyotamkwa kwenye Katiba inatosha. Rais Magufuli ayafanye makubwa aliyokusudia kuyafanya, ili kujenga msingi mzuri wa uzalendo na uwajibikaji kwa atakayefuata ajengee juu ya msingi huo. Lakini haya yatawezekana tu ikiwa atamalizia pale alipoishia mtangulizi wake Katiba Mpya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles