23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI UBUNGE KUFANYIKA LEO BILA UKAWA

Na AGATHA CHARLES-DAR ES SALAAM

UCHAGUZI wa marudio katika majimbo ya Singida Kaskazini, Longido na Songea Mjini na kata sita za Tanzania Bara, unafanyika leo bila upinzani baada ya vyama sita vya siasa kugoma kushiriki.

Vyama hivyo ni Chadema, CUF, ACT- Wazalendo, NCCR-Mageuzi, NLD na Chaumma ambavyo vilijiengua kutokana na madai kuwa mazingira ya ushindani hayakuwa sawa.

Hatua ya vyama hivyo kujitoa ilitokana na kulalamikia changamoto zilizojitokeza wakati wa uchaguzi mdogo uliopita wa udiwani katika kata 43 na kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuzishughulikia ili kuleta imani kwa vyama hivyo.

Kupitia mkutano uliovihusisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) uliofanyika Desemba, mwaka jana, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, alisema kutokana na kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi wa kata hizo 43, vyama hivyo, NEC na Serikali vilipaswa kukaa meza ya majadiliano ili kujadili na kutathmini changamoto zilizojitokeza kabla ya kuendelea kushiriki uchaguzi mwingine.

Licha ya hoja za Ukawa, NEC kupitia Mwenyekiti wake, Jaji Semistocles Kaijage, alivitaka vyama vya siasa kutumia utaratibu uliopo wa kisheria na kikanuni kuwasilisha malalamiko juu ya mambo yanayojitokeza wakati wa uchaguzi badala ya kuwataka wao wayashughulikie kwa kuwa hawana mamlaka nayo.

Jaji Kaijage alitoa kauli hiyo alipokuwa akifungua mkutano wa NEC na viongozi wa vyama vya siasa uliofanyika Dar es Salaam, ingawa vyama vilivyojiengua havikushiriki.

“NEC inashauri kwa mara nyingine kuwa ni vyema vyama vya siasa kwa kadiri inavyowezekana, vitumie utaratibu uliopo wa kisheria na kikanuni kuwasilisha malalamiko yanapojitokeza wakati wa kampeni, kabla na baada ya kuhesabu kura na baada ya matokeo ya kura kutangazwa,” alisema.

Pia katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Ramadhani, alisema maandalizi ya uchaguzi huo yalikamilika kwa asilimia kubwa huku vifaa vyote vinavyohitajika vimeshasafirishwa katika halmashauri zote zinazoshiriki uchaguzi huo zikiwamo karatasi za kura.

Kailima alisema wapiga kura 278,137 wanatarajiwa kupiga kura katika uchaguzi huo wa ubunge katika majimbo hayo na 324,435 katika uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata sita.

Uchaguzi huo unafanyika huku ukiwa hauna mvuto wala hamasa za kampeni kutoka kwa vyama mbalimbali kama ilivyozoeleka ambapo CCM na Chadema vilishindana kwa hoja majukwaani.

Pamoja na CCM kushinda kata 42 kati ya 43, lakini kitendo cha vyama vya upinzani kushiriki uchaguzi huo ilileta hamasa.

Kampeni za uchaguzi wa majimbo hayo matatu na kata sita zilianza tangu Desemba 19 na 21, mwaka jana na kumalizika jana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles