31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI MKUU KENYA LEO

NAIROBI, Kenya

WAKENYA milioni 19 leo wanatarajiwa kujitokeza kupiga kura kuuchagua uongozi wao mpya katika uchaguzi ghali na wenye ushindani mkali zaidi katika historia ya Kenya.

Ni uchaguzi ulioshuhudia wagombea wakuu wawili wa   urais, Rais Uhuru Kenyatta wa Chama cha Jubilee na mpinzani wake mkuu wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA), Raila Odinga, wakiendesha kampeni kali.

Wawili hao watakabiliana tena ambako kila mmoja amekwisha kuuleza matumaini makubwa ya kuibuka mshindi  matokeo yatakapotangazwa ndani ya siku saba baada ya upigaji kura.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2013, Rais Kenyatta alipata kura milioni 6.1 dhidi ya Odinga  aliyepata milioni 5.3.

GHARAMA KUBWA

Ni uchaguzi ambao unaelezwa kuwa ghali zaidi, ambao gharama yake haijawahi kushuhudiwa si tu nchini humo bali pia katika Bara Afrika.

Na inaaminika kuwa miongoni mwa uchaguzi ghali  duniani, ukikadiriwa kugharimu dola  za Marekani bilioni moja (Sh  trilioni 2.2 za Tanzania).

Kwa takwimu hizo, kwa wapiga kura  zaidi ya milioni 19   waliojiandikisha, kila mmoja ataugharimia   dola za Marekani 25 ( Sh 56,000 za Tanzania).

Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka 2015, nchi ambayo ina idadi kubwa ya watu kuliko nchi nyingine yoyoie  Afrika Mashariki, ulimgharimu kila mpiga kura dola tano za Marekani.

NYADHIFA ZILIZOKIMBILIWA ZAIDI

Mbali ya urais, nyadhifa nyingine zinazogombewa ni ugavana wa kaunti, useneta, ubunge na udiwani wa mabaraza ya kaunti (MCA).

Katika uchaguzi mkuu wa 2013 ambao ndiyo ulikuwa wa kwanza   kwanza katika mwavuli wa Katiba mpya  iliyokuwa na muundo mpya unaozipa kaunti  madaraka, vigogo wengi walijitosa kugombea useneta.

Wengi waliamini kiti hicho kina hadhi zaidi kama ilivyo Marekani ikilinganishwa na nyadhifa nyingine. Walisaka si tu hadhi na heshima bali pia maslahi ya  fedha. Ilikuwa kana kwamba ni raha ilioje ukijulikana kama ‘Seneta fulani bin fulan’

Lakini safari hii maseneta wengi wamevitosa viti vyao badala yake kukimbilia kugombea ugavana na udiwani baada ya kubaini useneta hauna maslahi ya  fedha ikilinganishwa na ugavana na udiwani, ambako kuna mambo mengie ya kupata fedha za ufisadi.

Mfano ni Seneta wa Nairobi, Mike Sonko, ambaye amekitosa kiti hicho  uwania ugavana wa Nairobi na akishinda inamaanisha atakuwa akisimamia fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya jiji hilo, kitu ambacho hakipo kwa useneta unaoonekana kama pambo tu.

Magavana wa kipindi kilichopita kutokana na mamlaka zao za kusimamia fedha za miradi mbalimbali za kaunti kama ilivyo kwa wawakilishi wa mabaraza, waliweza kupata fedha nyingi, ambazo pia zimewezesha kuanzisha vyama vyao vya siasa.

Mmoja wao ni Gavana wa Machakos, Alfred Mutua. Anadaiwa kutumia fedha za ugavana kuanzisha Chama cha Maendeleo Chapchap, Mwingine ni Gavana wa Bomet, Isaac Ruto ambaye ametumia fursa hiyo kuanzisha Chama cha Maendeleo  Mashinani (CCM)

KAMPENI

Rais Kenyatta ambaye alifanya mkutano wake wa mwisho wa kampeni katika Kaunti ya Nakuru Jumamosi, alipita  katika maeneo 504 katika   siku 70 za kampeni katika kaunti 47.

Takwimu za upande wa  Nasa hazikuweza kupatikana mara moja lakini hazitofautiani   na Jubilee hasa katika  wiki mbili za mwisho  ambazo kilishuhudia baadhi ya maeneo yenye ushindani mkali yakirudiwa na timu hizo.

WAGENI

Watu zaidi ya 9,000 wa kigeni na ndani wamepewa jukumu la kuwa waangalizi wa uchaguzi huo.

Waandishi wa kigeni 300 wako nchini humo kuifahamisha dunia habari za  uchaguzi huo.

USHINDI NA HOFU YA MACHAFUKO

Katika Bustani ya Uhuru mjini Nairobi Jumamosi, Odinga alianza kuzungumza wakati ule ule alioanza Rais Kenyatta huko Nakuru.

Kampeni za Jumamosi zilidhirisha  kufungwa kwa kampeni moto katika kile kilichoonekana kuwa mchuano mkali   baina ya watu wawili, ambao baba zao walifanya kazi pamoja miaka 54 iliyopita, kabla hawajafarakana.

Wakati Rais Kenyatta anatafuta kurudia historia ya ushindi wa 2013 dhidi ya Odinga akiamini itakuwa hivyo, Raila naye    amesema ana uhakika wa kumshinda mpinzani wake huyo.

Wote wawili wameeleza watakubali tu kushindwa iwapo uchaguzi utakuwa huru na wa haki, kitu ambacho kimetia hofu ya kutokea machafuko. Tayari Wakenya wengi si tu wanaikimbia miji kama ya Nairobi kwenda maeneo wanakotoka bali pia wengi wanakimbilia nchi jirani.

Mbali ya Wakenya, wengine ni wageni wakiwamo kutoka Ulaya ambao wameshuhudiwa kwa wingi katika mipaka ya Kenya na Tanzania.

WIZI WA KURA

Miongoni mwa  mikakati ya Odinga wakati huu ilikuwa kuhakikisha  unakuwapo mfumo bora wa kutambua wapiga kura, kusambaza na kujumuisha kura   kupunguza mwingilio wa binadamu  ambaye anaweza kuihujumu ikiwamo kupenyeza kura bandia.

Mara kwa mara, Nasa ilikuwa ikidai kuna mpango wa wizi wa kura unaohusisha pia kuhujumu mfumo, ikidai unafanywa na Jubilee ikishirikiana na vyombo vya serikali likiwamo jeshi, madai ambayo serikali imekuwa ikiyakanusha, ikieleza Raila anatafuta kisingizio cha kushindwa.

 

KURA ZA MAONI

Miongoni mwa viashiria kuwa uchaguzi kuwa na upinzani mkali ni kura za maoni.

Awali, Rais Kenyatta alikuwa akimuacha Odinga kwa   asilimia zaidi ya 10 kabla ya kuundwa   muungano wa Nasa, kitu ambacho kwa sasa kiongozi huyo wa Chama cha ODM amekipunguza na hata kumpiku Kenyatta.

Wiki iliyopita kampuni ya utafiti ya Ipsos ilimpa Odinga asilimia 43 ya kura na Kenyatta asilimia 47.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Infotrak, Odinga alikuwa akiongoza kwa asilimia 47 dhidi ya asilimia 46 za Kenyatta.

Kupanda haraka kwa Odinga kumechangiwa na   vyama vipya vipya viwili kujiunga na  NASA; Amani National Congress (ANC) cha Musalia Mudavadi na CCM cha Gavana Ruto.

Ndiyo maana Nasa ilitangaza kwamba iko katika mkakati wa kujipatia kura milioni 10 kati ya milioni 19 wakati Jubilee ilitangaza kulenga kura asilimia 70.

JAMII YA WAMASAI

Kutokana na kura katika ngome zao kukaribiana, wagombea hao wakuu wa urais waliwekeza nguvu katika maeneo yaitwayo kanda za mapambano, kaunti ambazo kuna wapiga kura ambao hawajaamua.

Hilo lilishuhudiwa huko Suswa, Narok Alhamisi na Ijumaa iliyopita.

Likiwa kati ya Mlima Suswa na Mlima Longonot na kuwa katika mpaka wa kaunti tatu, Suswa linahesabiwa kama mahali patakatifu kwa Jamii ya Wamasai.

Alhamisi iliyopita Raila na vinara wake wa NASA walipokea baraka kutoka kundi la wazee wa Kimasai.

Siku iliyofuata, Rais Kenyatta na Ruto wakawa eneo hilo hilo  ambako pia walipokea baraka kutoka kwa koo za Wamasai mbele ya Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania , Edward Lowassa, ambaye anahesabiwa kama kiongozi wa juu  wa jamii hiyo ukanda huo.

KUHUSIKA KWA TANZANIA

Kwa miaka mingi   wakati wa uchaguzi mkuu  wa Kenya, ni  Rais Yoweri Museveni wa Uganda ndiye amekuwa akilaumiwa kuingilia siasa za nchi hiyo.

Alimuunga mkono    Mwai Kibaki wakati wa machafuko ya Uchaguzi Mkuu wa 2007, ambao ulishuhudia watu 1,300 wakiuawa huku serikali ya Kenya zikimuunga mkono Museveni dhidi ya wapinzani wake wakati wa uchaguzi.

Museveni alishutumiwa na upinzani ulioongozwa na  Raila kwa kuingilia siasa za taifa hilo na hilo lilijirudia wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2013.

Lakini safari hii haikuwa   Uganda bali Tanzania na hilo lilianzia katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 wa Tanzania  uliohesabiwa kuwa ulikuwa na mchuano mkali zaidi katika historia ya nchi hiyo.

Ni kipindi ambacho kwa mara ya kwanza Wakenya walionekana kuvutwa na siasa za Tanzania. Hilo lilizidi   Chama tawala cha CCM kilipompitisha   John   Magufuli kuwa mgombea wake wa urais kinyume na matarajio ya wengi.

Vyombo vya habari vya Kenya viliripoti kuwa Serikali ya Jubilee ilikuwa ikifuatilia kwa karibu mchakato wa uteuzi wa wagombea urais wa CCM na haikufurahishwa na uteuzi wa  Magufuli kwa kufahamu ukaribu wake na hasimu wao wa siasa, Raila Odinga.

Magufuli amewahi kusimama katika majukwaa ya upinzani akiwataka Wakenya wamuunge mkono Odinga mwaka 2013.

Katika uchaguzi wa mwaka huu  i Kenya, Tanzania ilishutumiwa kuisaidia NASA ikiwamo kuiruhusu kuweka kituo cha kukusanya matokeo, madai ambayo yalikanushwa na serikali ya Tanzania.

Lakini pia Lowassa naye amekuwa gumzo baada ya kumuunga mkono hadharani Uhuru akiitaka jamii ya Wamasai kumpigia kura, akimueleza ni mpenda Jumuiya ya Afrika Mashariki na mwanademokrasia akilinganishwa na Odinga.

Kwa kitendo hicho, Lowassa ameshutumiwa na wapinzani nchini Kenya   kwa kuingilia siasa nchi hiyo.

 

MAENEO YALIYOTEMBELEWA ZAIDI

Narok ilikuwa moja ya maeneo yaliyotembelewa zaidi na wagombea hao wawili.

Takwimu zinaonyesha eneo hilo pamoja na Pwani, Magharibi, Kajiado, Kisii na Baringo yalitembelewa zaidi na wawili hao ikiwamo mara tatu hadi sita.

MAUAJI

Kifo cha Meneja wa Teknohama wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Chris Msando ni miongoni mwa matukio yaliyotikisa kampeni. Msando aliyekuwa akiufahamu kama kiganja chake cha mkono mfumo wa elektroniki wa uchaguzi alikutwa amekufa Jumatatu iliyopita ,siku tatu baada ya kutoweka.

Hadi sasa vyombo vya uchunguzi vinadai   kukihusisha kifo chake na suala la  mapenzi kuliko siasa.

Mbali ya tukio hilo, kulishuhudiwa kuvamiwa   Kituo cha Kuhesabu kura cha NASA  ingawa polisi wanakana kuwapo  tukio hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles