27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI MKUU KENYA 2017: NI KENYATTA AU RAILA ODINGA

Na Dorine Otinga, Nairobi

IMESALIA miezi miwili kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa wawakilishi wa mitaa, magavana, seneta wa kaunti, wabunge na urais baadaye mwaka huu.

Hadi sasa kumekuwa na hekaheka za hapa na pale kati ya wagombea 18 wa nafasi ya urais humu nchini, huku kila mmoja akijitapa kuibuka mshindi.

Je, hatima ya Kenya katika uchaguzi wa 2017 ni ipi? Hili ni swali sugu ambalo kila Mkenya anasubiri jibu lake kwa hamu. Uchaguzi wa urais ndio uti wa mgongo wa maendeleo ya nchi yoyote. Ni ndoto ya kila mmoja kuishi katika maeneo yenye haki, usawa na amani. Kenya inapitia hatua muhimu inapojiandaa katika uchaguzi wa urais wa 2017.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC)

Hii ni tume ambayo hujihusisha na shughuli za kuhesabu kura katika uchaguzi nchini Kenya. Kumekuwa na ghasia za mara kwa mara ambapo nyingine zilisababisha vifo vya watu watatu.

Maandamano hayo yalisababishwa na wafuasi wa chama cha CORD ambacho kinara wake ni Raila Odinga. Sababu kuu ya maandamano hayo ni kwamba walitaka Serikali ifanye mabadiliko katika tume hii ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

IEBC ilidaiwa kuunga mkono chama tawala cha Jubilee na kupanga kukisaidia kwa kutumia ulaghai kwenye uchaguzi mkuu hapo Agosti 8 mwaka huu. Kufuatia hayo, IEBC ilitakiwa kujiuzulu na viongozi wa upinzani wa CORD (pamoja na Muungano wa wapinzani  NASA). Upinzani ulihisi kwamba, makamishna wa IEBC walihusika na udanganyifu wa kura za urais mwaka 2013.

Hatimaye, makamishna wa Tume huru ya Uchaguzi Kenya, walisema wako tayari kujiuzulu. Makamishna hao tisa wakiongozwa na mwenyekiti wao, Isaac Hassan, waliafiki uamuzi huo mbele ya kamati ya pamoja katika Bunge la Taifa na Seneti, iliyobuniwa kupokea shutuma dhidi yao na pia mapendekezo ya jinsi ya kuimarisha shughuli za uchaguzi nchini Kenya.

Makamishna wapya wa IEBC

Tayari Kenya imepata makamishna wapya wa IEBC ambao watakuwa wasimamizi wakuu katika uchaguzi wa mwaka huu. Makamishna hao walitafutwa kutoka maeneo mbalimbali kwa lengo la kutimiza majukumu ya IEBC

Oktoba 21, mwaka jana Mwenyekiti aliyechaguliwa kusimamia zoezi la kuwapata makamishna wa IEBC, Bernadette Musundi, alisema jopo hilo litachapisha taarifa kwa wanaotaka nafasi hiyo.

Jopo hilo lilikamilisha zoezi hilo Novemba mwaka jana na siku hiyo pia watamkabidhi Rais Uhuru Kenyatta orodha ya makamishna wa IEBC ambao walipewa siku 14 za kuomba kazi hiyo.

Maandalizi ya Jubilee

Rais Uhuru ana mpango upi ili apate ushindi katika uchaguzi wa urais wa 2017? Chama cha Jubilee ni mojawapo ya vyama vinavyovuma nchini Kenya kisiasa. Kinara wa Jubilee ni Rais Kenyatta na Willaim Ruto, wanajiita UhuRuto.

Mojawapo ya mbinu walizopata kushinda uchaguzi mwaka huu ni kufungua ofisi  zao katika kaunti 47. Rais Kenyatta ana kibarua kikubwa katika kukipigia debe chama chake katika kaunti hizi.

Kuna mpango tayari wa kuhakikisha kwamba vyama vidogo vinavyounda Jubilee vinakubaliana kuhusu maofisa wa chama hicho kote nchini.

Kenyatta pamoja na Naibu wake, William Rutto, wamekuwa wakizuru viwanja vya Kasarani mjini Nairobi na kukutana na wafuasi wao.

Katika eneo la Magharibi mwa Kenya, litakuwa jukumu la vyama kama vile New Ford Kenya (NFK) na United Democratic Front (UDF), kuafikiana kuhusu watakaoteuliwa kuwa maofisa wa chama cha Jubilee.

Mbali na hayo, wenyeviti kutoka matawi 47 wametengeneza baraza kuu la Jubilee Party, ambalo linaendesha shughuli za kila siku za chama. Wanasiasa wawili kutoka maeneo yote nane wanafanya kazi pamoja na Rais Kenyatta na Naibu wake Rutto ili kutengeneza kamati kuu tekelezi ya chama.

Kulingana na ripoti iliyochapishwa katika mtandao wa habari wa Star, Rais Kenyatta na Naibu wake watazuru kaunti 47 ili kukutana na viongozi wa vyama na kukiuza chama hicho kabla ya uchaguzi wa 2017. Ziara hizo za kaunti zitaanza mwishoni mwa mwaka huu.

Raila Odinga amejiandaa vipi?

Kinara wa muungano wa upinzani, NASA, Raila Odinga, kwa muda mrefu amekuwa akitoa upinzani kwa chama tawala. Ilikuwa bahati mbaya sana kwake, kwani kila mara amekuwa akishindwa kutimiza ndoto yake ya kuingia Ikulu.

Inapendeza sana jinsi bingwa huyu wa siasa hafi moyo kisiasa, kwani anaonekana kila mara akiinyooshea Serikali mkono wa lawama iwapo kumetokea sakata lolote la wizi au utenda kazi hafifu.

Katika muungano wa NASA, kulikuwa na mvutano kuhusu nani anastahili kupeperusha bendera ya muungano huo kati ya Kalonzo Musyoka na Raila Odinga dhidi ya muungano wa Jubilee.

Licha ya Odinga  kuwa tayari kumuunga mkono yeyote atakayesimamia kiti cha ugombea urais katika chama cha NASA, wafuasi wake na wanasiasa mbalimbali hawakuafiki yeye kutopewa nafasi nyingine.

Ndiyo kusema NASA iliwaona wawili hao, Raila na Kalonzo  kuwa wagombea wenye sifa ya kupambana na Kenyatta na Ruto

Kiujumla Rais Kenyatta amejaribu kila awezavyo kuwa kiongozi bora. Hata hivyo, Serikali yake imekumbwa na changamoto nyingi sana, mojawapo ikiwa ni ufisadi, ugaidi na mengine mengi. Wakenya wengi wanamtazama kwa jicho la karibu sana kulingana na namna anavyojaribu kukabiliana na changamoto hizo.

Viongozi wa fedha wa mataifa mbalimbali ulimwenguni wamempongeza Rais Kenyatta kwa mtazamo na uongozi bora ambao wanasema ni muhimu katika ukuaji wa bara la Afrika.

Kiongozi wa Benki ya Dunia na African Development Bank (AFDB), alisema sera za Kenya zilizoanzishwa na Rais Kenyatta zimeweka mazingira mazuri ambayo yamechangia uwekezaji na biashara kati ya mataifa ya Afrika.

Maoni: +254 716 955356

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles