24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Uchaguzi Marekani 2018: Wapigakura wameanza ‘kumzaba makofi’ Trump

Na MWANDISHI WETU         |            


RAIS wa 45 wa Marekani Donald Trump, yupo kwenye kibarua kigumu baada ya viti vingi vya Baraza la Wawakilishi kunyakuliwa na chama cha upinzani cha Democratic.

Kitendo hicho kinaweza kutafsiriwa kama ‘kumzaba makofi’ Rais huyo na chama chake cha Republicans baada ya kushindwa vibaya kwenye nafasi za Baraza la Wawakilishi (House of Represantative) na Baraza la Seneti.

Licha ya kuwa Rais Trump hakuwapo kwenye karatasi za kupigia kura katika uchaguzi huo wa katikati ya muhula uliofanyika Novemba 6, mwaka huu, hata hivyo matokeo yanabainisha mustakabali wa urais wake.

Ikumbukwe kuwa wananchi wa Marekani wataingia  kwenye Uchaguzi Mkuu katika nafasi ya urais mwaka 2020.

Wakati Rais Trump akiangalia upepo wa kisiasa wa miaka miwili iliyosalia kutimiza miaka minne ya utawala wake tayari taa nyekundu imeanza kuwaka ikionyesha kuwa ana hali mbaya kisiasa, kutokana na kushindwa kwa Warepublican katika uchaguzi huo wa Baraza la Wawakilishi.

Tangu aingie madarakani Rais Trump, wafuasi na wanachama wa Republican walikuwa na imani iliyojaa matumaini kwamba utawala wa chama hicho utafanya mambo makubwa na kuvutia uungaji mkono, jambo ambalo limekwenda kinyume kabisa na matarajio yao.

Katika uchaguzi huo kinachoonekana ni kwamba siasa na Sera za Rais Trump na chama chake zimefeli na kusababisha wapigakura takribani asilimia 55, katika uchaguzi huo kutokipigia kura chama cha Republican.

Hali hiyo ndiyo inakazia msingi wa hoja kuwa Trump atakuwa na kibarua kigumu cha kupambana na wapinzani wake kulinda kitumbua chake kisiingie mchanga.

Bunge la 116 la Marekani linalotarajia kuketi mwanzoni mwa mwaka ujao linaonyesha dalili za Wademocrat kuhodhi kiti cha spika na kuongoza kamati zote za Bunge hilo. Hivyo miaka miwili ijayo Rais Trump atakuwa na kibarua kigumu cha kukabiliana na upinzani katika Baraza la Wawakilishi, ili kuweza kutekeleza mipango na sera zake.

Wachambuzi wa kisiasa za Marekani wanadai kuwa kwa kuwa Baraza la Wawakilishi ndilo litakalohodhi uandaaji na upangaji wa bajeti ya serikali kuu ya Marekani, baraza hilo lina uwezo wa kuuwekea vikwazo utawala wa Trump katika kufanikisha mipango yake, kwa kutumia turufu ya kubadilisha tarakimu za ukubwa wa bajeti yake.

Aidha, kulidhibiti Baraza la Wawakilishi, kunawapa Wademocrat fursa ya kipekee, ya kuweza kuchunguza na kufuatilia kashfa kadhaa zinazomkabili Trump, ikiwemo ya tuhuma za kushirikiana kula njama na Russia, kukwepa kulipa kodi na mahusiano yake ya kingono na wanawake kadhaa.

Kiongozi na mbunge wa Democratic, Nancy Pelosi, anayetarajiwa kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi katika Kongresi ya Marekan amekipandisha chama hicho na kukiweka katika hali nzuri kisiasa.

Mbunge huyo ametaka Wademocrat ambao wameshinda katika uchaguzi huo kuwatumikia vema wananchi wa Marekani badala ya kuonyeshana ubabe na chama tawala.

Ikumbukwe kuwa uchaguzi uliofanyika nchini humo ulikuwa ni kuwachagua wagombea wa nafasi ya useneta (35), magavana (36) wa majimbo na wabunge wote 435 katika Bunge la Wawakilishi, pamoja na maofisa wengine kadhaa wa serikali za majimbo.

Uchaguzi huu wa katikati ya muhula ni muhimu kwani unatumika kuonyesha taswira ya mwelekeo wa kisiasa kati ya vyama vinavyochuana ambavyo ni Democratic na Republicans.

Mchuano mkubwa ni kwa vyama hivyo kuibuka na ushindi kisha kulidhibiti Baraza la Wawakilishi au Baraza la Seneti. Baada ya kutangazwa matokeo. Kama nilivyoeleza awali ni dhahiri kuwa chama cha upinzani cha Democratic kimeshinda pakubwa hivyo kuwanyang’anya udhibiti chama cha Republicans.

Chama cha Republicans kimepoteza wingi katika hali ambayo itaufanya urais wa Trump kupitia katika wakati mgumu zaidi tofauti na hata wakati akiwania kiti hicho miaka miwili iliyopita.

Katika uchaguzi huo Republicans wamepoteza viti  vya ugavana hata hivyo kimefanikiwa kubaki na viti vingi katika Bunge la Seneti.

Ushindi wa Democratic na kulidhibiti Baraza la Wawakilishi ina ujumbe wa kuwadia ukomo wa udhibiti wa chama cha Republicans katika majimbo nchini Marekani.

Chama cha Democratic kimepata viti 223 dhidi ya 197 vya chama cha Republicans. Katika uchaguzi kama huu mwaka 2014 chama Republicans walizoa viti 247 na huku Democratic wakiambulia viti 188.

Ushindi wa Democratic kwenye Bunge la Wawakilishi si jambo zuri hata kidogo kwa Rais Trump, ambapo sasa atakabiliwa na upinzani maradufu katika kutekeleza sera zake kwa miaka miwili iliyobaki kwenye muhula wake wa uongozi.

Upande wa Bunge la Seneti chama cha Republicans wameshinda 51 na Democratic 46. Katika uchaguzi kama huu uliofanyika mwaka 2014, Republicans walishinda viti 54 huku Democratic wakipata viti 46. Mwaka 2014 Republicans walishinda majimbo 37 na Democratic 17.

Uchaguzi huo unatarajia kubaini ikiwa Trump ana uwezo wa kuongoza Marekani katika kipindi cha miaka miwili ijayo au la.

Shauku ya upigaji kura hususani kwa vijana ulikuwa mkubwa zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka 2014.

Ikumbukwe kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2017, asilimia 80 ya wazungu walimpigia kura Trump kwenye urais, ambapo baadhi yao wamekinyima kura chama chake kwenye uchaguzi huu wa wabunge wa Baraza la Wawakilishi na Seneti.

Inaelezwa kwamba licha ya juhudi za Rais Trump kutumia mbinu tofauti kuwasilisha hoja ambazo zinaonekana kuzua hisia mseto katika juhudi ya kuimarisha uungwaji mkono wake, lakini hata hivyo ameshindwa kuwashawishi wapigakura.

Aliyekuwa mtangulizi wake, Barack Obama – amekuwa mstari wa mbele kuendesha kampeni za chama cha Democratic amesema uamuzi wa Wamarekani mara nyingi hufanywa kwenye sanduku la kura.

Wakati wa kampeni zake Trump alikumbusha masuala muhimu yaliyompa ushindi uchaguzi wa mwaka 2016 akisisitiza kuwa chama cha Democratic watasambaratisha uchumi kwa kuruhusu uhamiaji haramu.

Wagombea wa Democratic kwa upande wao walijiepusha na mashambulizi ya moja kwa moja na wapinzani wao, badala yake walizungumzia masuala kama vile ya afya na ukosefu wa usawa katika mambo ya uchumi.

Chama hicho kilitumia fursa ya kuwashawishi  wapiga kura vijana na wale wanaotokea katika makundi ya wachache waliotengwa ambao wanapinga msimamo wa Rais Trump dhidi ya masuala yanayowagusa wao na wenzao moja kwa moja.

Trump amekuwa akikabiliwa na ukosoaji mkubwa kutokana na lugha yake ambayo inadaiwa kuwagawanya watu.

Uchaguzi wa katikati ya muhula utaamua ni nani atakayechukua udhibiti wa mabunge yote mawili ambayo yanatunga sheria nchini humo.

Ikiwa chama cha Republicans kingefanikiwa kuongoza mabunge yote mawili yaani Seneti na uwakilishi, huenda wangeimarisha ajenda za chama chao na zile za Rais Trump. Lakini sasa watategemea Bunge la Seneti pekee, wakati Bunge la Wawakilishi limedhibitiwa na wapinzani wao wa chama cha Democratic.

Katika mahojiano na runinga ya ABC wiki hii, Rais Trump amesema anataka kupunguza makali ya matamshi yake katika kipindi kilichobaki cha uongozi wake.

“Nahisi kwa kiwango fulani, sina chaguo, nadhani nilitakiwa kupunguza makali ya matamshi yangu kuanzia mwanzo.” anasema.

Kwa upande mwingine matokeo ya uchaguzi huu yameonyesha mabadiliko makubwa ya wapigakura ambao walikichagua chama cha Republicans kwenye urais.

Utafiti wa maoni wa baada ya kura kupigwa mwaka 2016 uliofanywa na Edison Research kwa niaba ya kundi kwa jina National Election Pool, ambao ni mkusanyiko wa mashirika makubwa ya habari ABC News, Associated Press, CBS News, CNN, Fox News na NBC News unaonyesha kuwa Trump alinufaisha pakubwa, lakini sasa ameumizwa nao.

Utafiti huo ulioshirikisha wapiga kura zaidi ya 25,000, na hizi ndizo takwimu bora zaidi zinazoweza kupatikana kwa sasa.

Matokeo hayo yanaonyesha asilimia 53 ya wanaume walimpigia kura Trump, na asilimia 41 wakampigia Hillary Clinton. Takwimu hizo ni kinyume kabisa kwa wanawake, ambapo asilimia 53 walimpigia kura Clinton na asilimia 41 walimpigia Trump.

Miongoni mwa wapiga kura wazungu (ambao ni asilimia 70 ya jumla ya wapiga kura), Trump alishinda kwa asilimia 58 naye Clinton alipata 37, huku mgombea huyo wa Democratic akipata uungwaji mkono mkubwa miongoni mwa wapiga kura Weusi kwa asilimia  88, wakati  Trump aliungwa mkono na watu weusi kwa asilimia 8.

Wapiga kura wa asili ya Hispania (Latino/Mexico), asilimia 65 kwa Clinton naye Trump akipata asilimia 29. Ukiangalia sasa wanawake Wazungu, walimpendelea Trump, ambapo asilimia 53 walimuunga mkono wakilinganishwa na asilimia 43 wakimpigia Clinton.

Ingawaje uchaguzi huu haukuhusu urais, lakini umetoa taswira ngumu kwa Republicans. Ndiyo kusema ushawishi wa Trump kwa wapigakura umeshuka kwa mbali sana ukilinganisha na takwimu za kura zilizomchagua yeye, huku chama chake kikitoshwa kwenye seneti na wawakilishi.

Wanawake 100 wavunja rekodi Marekani

Licha ya wapiga kura katika uchaguzi wa katikati ya muhula kuchagua wagombea tofauti, lakini wanawake wameibuka kuwa videdea zaidi. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Habari la CNN zinaonyesha kuwa wanawake 100 wamechaguliwa katika viti vya Bunge la Wawakilishi.

Awali CNN walibashiri wanawake 96 wangechaguliwa katika kinyang’anyiro cha viti vya Bunge la wawakilishi. Katika uchaguzi wa mwaka huu asilimia 52 ya wagombea waliochaguliwa ni wanawake.

Aidha, ifikapo mwaka 2019 itashuhudiwa zaidi ya wanawake 100 wakiingia bungeni.

Uchaguzi wa muhula kwa ujumla ni kama vile kura ya maoni kuelekea uchaguzi wa urais na chama chake kwa ujumla. Hicho ni kiashiri kuwa wagombea wanawake wana uwezekano mkubwa kushinda katika uchaguzi ujao iwapo watateuliwa kugombea katika majimbo ama nafasi ya urais.

Tukitazama kinyang’anyiro hiki kama turufu ya mbio za urais mwaka 2020 ndani ya chama cha Democratic, maana yake wanasiasa wawili ambao wametamba tena kwenye uchaguzi wa muhula, Kirsten Gillibrand (Seneta wa New York) na Ammy Klobuchar (Seneta wa Minnesota) watakuwa na nafasi kubwa ya kuibua upinzani dhidi ya chama cha Republicans.

Duru za kisiasa ndani ya Democratic zinawataja Klobuchar na Gillibrand kama wanasiasa wenye nguvu na ambao wanastahili kupewa madaraka ya urais nchini Marekani. Sifa zao zinalingana, kwamba wanapenda kupambana ana kwa ana na wapinzani wao hususani Rais Trump.

Inaelezwa kuwa litakuwa jambo la kushangaza kama wanasiasa hao hawatagombea urais katika uchaguzi ujao wa mwaka 2020.

Baada ya kushindwa vibaya kwenye uchaguzi wa katikati ya muhula, Rais Trump anatarajiwa kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri ambapo hatua ya kwanza ni kumfukuza kazi mwanasheria mkuu, Jeff Sessions.

Lengo la mabadiliko hayo ni kujaribu kurekebisha hali yake mbaya ya kisiasa kutokana na matokeo ya uchaguzi wa muhula.

Trump ametajwa kupania kuwateua wanasiasa ambao ni watiifu kwake ili wawe mawaziri huku wale wasiomtii kutimuliwa. Hapo ndipo linapoingia jina la Jeff Sessions ambaye amejiuzulu kukwepa shinikizo la Rais. Taarifa za ndani zimesema kuwa Rais Trump amedhamiria pia kuanza kufanya mikutano ya hadhara na amefuta mapumziko. Hilo litakuwa kama nyenzo ya kutafuta uungwaji mkono ili achaguliwe tena kwenye uchaguzi ujao.

“Matokeo ya uchaguzi yamemwangusha Trump, ameshuhudia kwa namna gani alivyoanguka. Kwahiyo anataka kurejesha upendo uliokuwepo kwenye mikutano ya hadhara wakati akigombea urais mwaka juzi,” kimesema chanzo cha ndani ya rais huyo kilipozungumza na CCN.

Hatua nyingine ambayo itachukuliwa na Trump ni marekebisho katika sera za mambo ya nje, eneo ambalo marais waliopita walitumia kama nyenzo ya kujijenga kisiasa.

Hivyo atakutana na viongozi wa Jumuiya ya Ulaya wakati wa kuadhimisha kumbukumkbu ya vita ya kwanza ya dunia pamoja na kukutana na marais, Xi Jinping (China) na Vladimir Putin (Urusi).

Mgogoro na vyombo vya habari

Wakati akiwa katika hali ngumu kisiasa Rais Trump amekuwa na uhusiano mbaya na baadhi ya vyombo vya habari tangu aingie madarakani. Uhusiano mbaya ulichangiwa zaidi wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2016.

Vita yake kuu ilikuwa dhidi ya Kituo cha Televisheni cha CNN.

Chombo hicho wakati wa uchaguzi mkuu huo  kilikuwa kambi ya chama cha Democratic. Vita vya maneno, sera, na propaganda zimewafikisha kwenye mapambano makali hali ambayo imevuka mipaka na kuihuisisha serikali ya sasa. Hadi ameingia madarakani amekuwa na vita ileile.

Kufukuzwa mkutanoni na kufutiwa kibali cha kuingia Ikulu ya White House nchini Marekani kwa mwandishi wa CNN, Jim Acosta kumekumbusha vita iliyokuwepo kipindi cha uchaguzi.

Mwandishi huyo alifukuzwa kwenye mkutano wa  Trump baada ya majibizano ya maneno kati ya Acosta na Rais huyo walipokuwa kwenye mkutano.

Ikumbukwe kuwa Januari mwaka jana, Jim Acosta alinusurika kufukuzwa na maofisa wa Ikulu nchini humo kwa kile kilitajwa uhusiano mbovu kati ya serikali ya Trump na kituo cha runinga cha CNN.

Katika mkutano wake wa kwanza tangu alipochaguliwa kuwa rais, alionyesha ghadhabu ya waziwazi dhidi ya CNN baada ya kumkatalia Jim Acosta nafasi ya kuuliza swali.

Acosta alitaka kufahamu kuwa kwanini Rais huyo amekuwa akikishambulia kituo cha CNN bila kukipatia nafasi ya kujieleza. Hata hivyo Trump alitupilia mbali maombi hayo.

Kwahiyo, katika mkutano wa Rais Trump na vyombo vya habari  wiki hii, Jim Acosta aliiingia matatizoni kwa mara nyingine baada ya kuhoji sera ya wahamiaji haramu kutoka Amerika ya Kati ambao wamepigwa marufuku kuingia nchini Marekani.

Acosta alihoji matamshi ya Rais Trump ambaye aliwaita wahamiaji hao ni wavamizi wenye lengo la kuiharibu Marekani. Lakini Rais Trump alimjibu kifupi, “Tafadhali, naomba uniache niongoze nchi hii, na wewe unaongoza CNN,” alisema Trump.

Mabishano kati ya Trump na Acosta yamezua mjadala mkubwa. Na zaidi baada ya maofisa usalama wa Ikulu ya White House kumtaka arejeshe kitambulisho kinachomwezesha kuingia Ikulu hiyo katika mikutano na kurusha matangazo ya moja kwa moja.

Msemaji wa Ikulu, Sarah Huckabee Sanders, ambaye amekuwa kwenye malumbano ya muda mrefu na mwandishi huyo.

Duru za kisiasa zinasema kwa mara ya kwanza Rais Trump alionyesha hasira zake hadharani dhidi ya CNN akiwa ziarani nchini Uingereza.

Katika ziara hiyo Trump alikataa kujibu swali la mwandishi wa CNN akidai kuwa chombo hicho kipo kwa masilahi ya wapinzani wake Democratic pamoja na kuwa chanzo cha kusambaza habari za uzushi dhidi ya serikali yake.

Ugomvi kati ya Rais Trump na waandishi wa habari haujatendeka kwa Jim Acosta peke yake, bali wapo waandishi wengine waliokutwa na dhahama hiyo kama vile Peter Alexander (NBC), April D. Ryan (American Urban Radio Networks) na Yamiche Alcindor (PBS).

Mantiki inaonyesha kuwa Trump amekuwa kwenye vita dhidi ya vyombo vya habari vyote ambavyo havikumuunga mkono kwenye Uchaguzi Mkuu wa Urais mwaka 2016.

Katika vita yake dhidi ya vyombo vya habari, amewahi kumfokea mwandishi April D. Ryan na kumwamuru akae chini licha ya kulalamikia matamshi ya kibaguzi yaliyotolewa na rais huyo.

Malumbano yaliyodumu kwa miaka miwili sasa kati ya Trump mwandishi huyo wa CNN yameonyesha taswira mbaya na sasa wasaidizi wake wamechukua hatua ya kumwondolea kibali cha kuhudhuria mikutano inayoandaliwa Ikulu.

Wataalamu wa sayasni ya siasa wanasema kisiasa msimamo wa Rais Trump kama mwanasiasa dhidi ya chombo cha habari ni sahihi kwakuwa hakimtendei haki.

Mwenendo huo wa Trump dhidi vyombo vya habari umekuwa mbaya kupindukia jambo hilo linatajwa kuwa linaweza kumwathiri katika uchaguzi ujao wa urais wa mwaka 2020.

Matokeo ya uhusiano wake mbaya dhidi ya vyombo vya habari yanatishia kuathiri kampeni zake za uchaguzi ujao ambao atawania kuchaguliwa katika muhula wa pili.

Je uhusiano wa chama cha Republicans na vyombo vya habari utaathiriwa na matukio ya mwanachama wake Donald Trump? Hili na mengine ni jambo la kusubiri. Muda utaongea zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles