24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

UBUNGE AFRIKA MASHARIKI PATASHIKA

WABUNGE

NA EVANS MAGEGE,

VIKUMBO ambavyo vimeambatana na mikakati ya chini kwa chini ya kuwania ubunge wa Afrika Mashariki (EALA), vimeanza miongoni mwa wanasiasa kutoka vyama mbalimbali nchini.

Mazingira hayo yameanza kujipambanua kwa kasi ndani ya kipindi ambacho imesalia miezi mitano kuelekea kwenye ukomo wa Bunge la sasa ambalo limehudumu kwa miaka mitano kwa mujibu wa sheria za Bunge la EALA.

Tayari majina mapya ya vigogo kama  Balozi Khamis Kagasheki, Steven Wassira, Habib Mnyaa, Ezekia Wenje, John Shibuda na Profesa Kitila Mkumbo yanatajwa kuingia kwenye mkumbo huo wa mikakati ya chini kwa chini ya kuwania nafasi hiyo.

Wengine wanaotajwa katika kinyang’anyiro hicho ni makada wa CCM, Sebastian Ndege, aliyewahi kuwa Miss Tanzania, Basila Mwanukuzi na Abudlkarim Shah.

Wamo pia wanasiasa wa upinzani ambao ni Julius Mtatiro wa CUF na John Mrema wa Chadema.

Gazeti hili lilitaka uthibitisho wa wanasiasa hao ambapo lilimtafuta kila mmoja kwa wakati wake, Wassira ndiye aliyeweka wazi msimamo wake juu ya hilo kwa kusema kwamba hana mpango wa kuwania ubunge wa EALA.

Profesa Kitila ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)  na mshauri wa siasa wa Chama cha ACT- Wazalendo, alipoulizwa na gazeti hili alikiri wazi kuwa na nia ya kuwania ubunge wa EALA, lakini bado anafanya utafiti kama mpango wake utakuwa sahihi au la.

Gazeti moja hapa nchini ambalo linachapwa mara moja kwa wiki limewahi kumuuliza Wenje kama ana mpango wa kuwania ubunge wa EALA.

Katika maelezo yake, Wenje alisema  yeye ni mwanasiasa kijana na mwenye uwezo wa kutumikia chama chake popote atakapoonekana anafaa.

“Nimewahi kuwa mbunge na hivyo nina uzoefu wa kuwa mbunge. Halafu nilikuwa nashughulika na mambo ya uhusiano wa kimataifa kichama na hivyo nafahamu kuhusu EALA kwa undani. Wakati ukifika na chama kikiona ninafaa sitasita kuchukua fomu,” alinukuliwa Wenje.

Kwa upande wa wanasiasa kama Shibuda na Mnyaa, kauli yao juu ya mkakati huo haikupatikana kutokana na simu zao kuzimwa ila kwa upande wa Balozi Kagasheki yeye hakupokea simu kila alipopigiwa.

Wakati majina hayo yakihusishwa kwa ukaribu na vikumbo vya kuwania ubunge wa EALA, kwa upande wa wabunge wanane kati ya tisa wanaoiwakilisha nchi ndani ya Bunge hilo wameonyesha nia ya kutetea nafasi zao.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Wabunge wa Tanzania ndani ya Bunge la EALA, Makongoro Nyerere, aliweka bayana kwamba taarifa alizonazo kwa sasa wabunge wenzake wameonyesha nia ya kutetea nafasi zao kwa sababu taratibu bado zinawaruhusu kufanya hivyo.

Alisema timu nzima ya wabunge wanaoiwakilisha nchi ndani ya Bunge la EALA (ambao ni wabunge tisa) ni Abdullah Mwinyi pekee ndiye hataweza kutetea nafasi yake katika uchaguzi wa mwaka huu kwa sababu atakuwa amemaliza vipindi viwili vya kutumikia ubunge kama taratibu zinavyoelekeza.

Kwa mantiki ya maelezo ya Makongoro, wabunge ambao watatetea nafasi zao katika bunge hilo ni yeye mwenyewe, Adam Kimbisa, Mariam Usi Yahaya, Angella Kizigha, Benard Murunya, Shy-Rose Bhanji (CCM), Nderakindo Kessy (NCCR-Mageuzi) na Twaha Taslima (CUF).

Kwa upande mwingine duru za siasa zinautazama mwelekeo wa kinyang’anyiro cha kuwania viti vya ubunge wa EALA kuwa kikali zaidi ya chaguzi nyingine zilizowahi kufanyika siku za nyuma.

Mazingira hayo yanajengwa kwa hoja kwamba kinyang’anyiro hicho kitakuwa kigumu zaidi kwa watia nia kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Inaelezwa kwamba, ndani ya CCM ndiko kuna joto kali la ushindani wa kupita kwenye mchujo, hali ambayo ni tofauti sana na kwenye vyama vingine vya upinzani.

Kwamba hata baada ya nafasi ya mchujo wagombea wa CCM watakaosonga mbele watakabiliwa na mtihani mwingine wa kutafuta ushawishi wa kupigiwa kura za kutosha kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wa wagombea kutoka vyama vya upinzani hususani Chadema na CUF inayoungwa mkono na Maalim Seif Sharif Hamad, inaelezwa kuwa wanaweza kupata urahisi kupita katika nafasi ya mchujo ndani ya vyama vyao  kutokana na uhalisia wa ushindani hafifu lakini mtihani mgumu utakaowakabili ni kuungwa mkono na wabunge wa Jamhuri ya Muungano ambao wengi wao wanatoka CCM.

Kwamba ili mjumbe kutoka vyama vya upinzani ashinde nafasi ya ubunge wa EALA, itamlazimu aungwe mkono kwa kiasi kikubwa na wabunge wa CCM.

Mazingira hayo yapo vile vile kwa wagombea kutoka upande wa CCM kwamba nafasi yao ya kushinda itategemea uungwaji mkono kutoka ndani ya CCM na upande wa vyama vya upinzani.

Ugumu ndani ya upinzani

Mgogoro wa CUF nao una changamoto zake na tayari baadhi ya wachambuzi wanasema huenda athari za mgogoro unaofukuta ndani ya chama hicho zikaonekana katika uchaguzi huu.

Kwa mfano, Taslima ni mwana CUF ambaye yuko katika kundi la Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif, lakini Mnyaa ambaye alipata kuwa mbunge wa Jimbo la Mkanyageni, Pemba, yuko katika kundi linaloongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba, wachambuzi wanasema wote wanaweza kujikuta katika wakati mgumu wa kuungwa mkono kupita katika kinyang’anyiro hicho ndani ya Bunge.

Kwa upande wa wabunge wa Chadema hasa wale waliokosa ubunge katika Bunge hili mfano Wenje, chama kinaonekana kuwahitaji waendelee na maisha ya kisiasa kwa kupata majukwaa ya kuzungumzia masuala ya kitaifa.

Katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2012, Chadema haikupata mbunge, ingawa chenyewe ndicho kilikuwa chama kikuu cha upinzani na ndicho kilichokuwa kimeunda Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Itakumbukwa aliyekuwa mgombea wa Chadema, Antony Komu, alikosa fursa hiyo kwa sababu wabunge wa CCM walitumia wingi wao kumnyima kura na hivyo kukimbilia mahakamani kupinga matokeo hayo.

Katika kesi iliyofunguliwa katika Mahakama ya Afrika Mashariki mwaka 2012, pamoja na mambo mengine, Komu alihoji utaratibu unaotumika kupata wabunge wa EALA nchini, ambao ni kinyume na utaratibu unaotumiwa na nchi nyingine.

Kwa mfano, Komu alisema ibara ya 50 ya Katiba ya EALA inataka nafasi za ubunge zigawanywe kutokana na uwiano wa nguvu za vyama katika mabunge ya nchi wanachama, lakini hali ni tofauti Tanzania.

Komu pia alihoji kama ni halali kwa chama kinachounda kambi rasmi ya upinzani bungeni kutokuwa na mbunge kwenye EALA na badala yake chama kidogo kupewa nafasi hiyo.

Ingawa Komu alishinda katika kesi hiyo, Mahakama hiyo ilisema kwamba kesi hiyo haikupaswa kufunguliwa na mtu binafsi bali taasisi; na hadi leo marekebisho aliyokuwa akiyalilia mbunge huyo wa sasa wa Moshi Vijijini bado hayajafanyiwa kazi.

Kuhusu Ukawa

Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) itabidi uamue kuhusu nani ataenda EALA, kwa kutazama uwakilishi wa vyama, suala la Zanzibar na nguvu na ushawishi wa wabunge wanaotakiwa kuwakilisha nchi kwenye Bunge hilo.

Katiba ya EALA inataka wabunge wake wawe wanatokana katika vyama vilivyo bungeni jambo ambalo linatoa mwanya kwa Chama cha ACT-Wazalendo ambacho kina mwakilishi mmoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles