27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Tushirikiane kuwalinda mabinti wa taifa hili

TAARIFA kwamba kundi la vijana wa kike kati ya umri wa miaka 15 na 24 ndilo linaongoza kwa maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi, siyo za kutia moyo. 

Kwamba kiasi cha wasichana 300 wanaambukizwa Virusi vya Ukimwi (VVU) kila wiki ni idadi kubwa ambayo hakika inaonyesha kwamba kazi ya kupambana na kuenea kwa VVU na Ukimwi bado ni nzito.

Hali hiyo ya maambukizi iliwekwa wazi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ukimwi (Unaids) wiki iliyopita wakati wa maadhimisho ya siku ya kupambana na ubaguzi na unyanyapaa dhidi ya wanawake na wasichana wanaoishi na VVU, huku ikielezwa kwamba wavulana nao wanaambukizwa nusu ya idadi ya wasichana kwa wiki.

Takwimu hizi kwa vyovyote zinavyoangaliwa ni mbaya kwa ustawi wa taifa, lakini zaidi katika mapambano dhidi ya Ukimwi. 

Kundi hili linaloandamwa na maambukizi haya ndilo linalotegemewa kama nguvu kazi ya taifa ya sasa na ijayo. 

Ni jambo la kusikitisha kwamba wasichana hawa wanajikuta katika madhila haya kutokana na watu wazima wenye uwezo wa fedha kutumia udhaifu wa watoto hawa na kuwaghilibu kiasi cha kuwatumbukiza kwenye maambukizi.

 Ni bahati mbaya kwamba badala ya jamii kusaidia kuwalinda wasichana hawa ambao wako katika umri wa kuwa shuleni – sekondari na vyuo, wanaandamwa na watu wazima, wengine wakiwa na umri sawa na wazazi wao kwa nia ya kuwataka kimapenzi, matokeo yake wanawaharibia maisha kwa kuwa wanashindwa kufuatilia masomo yao vema, lakini kubwa zaidi wanawatumbukiza katika janga la ugonjwa wa Ukimwi.

Katika miaka ya hivi karibuni kumeibuka kundi la watu wanaoona kuwa ugonjwa wa Ukimwi kama wa kawaida kabisa. Sababu kubwa ya kuuona hivyo ni kutokana na kuwapo kwa unafuu wa matumizi ya dawa za kufubaza makali ya virusi vya ugonjwa huo. Wapo waliokwenda mbali zaidi wakiamini kwamba kutokana na nafuu ya dawa hizo wana uwezekano mkubwa wa kuishi maisha marefu hata kama wataambukizwa sasa, hivyo tahadhari dhidi ya ugonjwa huo kwao si kitu cha kutiliwa maanani tena.

Kundi jingine la waharibifu ni lile linaloamini kuwa wasichana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 ni salama, kwamba kutembea nao hata bila kinga hakuna shida kwa sababu ya imani potofu kuwa wako salama dhidi ya virusi vya Ukimwi. Matokeo yake watu wenye mawazo kama hawa wamejikuta wakisababisha maafa makubwa kwa kundi hili.

Sisi tunaamini kwamba jamii ina wajibu wa kupiga kelele, kuhimiza ulinzi wa wasichana na kuomba juhudi zaidi zielekezwe kwenye hamasa ya ulinzi wa wasichana dhidi ya mafataki wanaoamini kwamba ukware wao unakuwa salama  kwa kuwa tu wanatembea na mabinti wadogo. Kama taifa tunao wajibu wa kutoa elimu ili wasichana hawa wajitambue pia.

Sisi kama taifa sasa tuseme hapana kwa mafataki wanaowaandama mabinti hawa wadogo, na kwa kweli sheria za kuwalinda watoto dhidi ya tamaa za mwili wa wanaume wenye uchu wa ngono zichukue mkondo wake. Tushirikiane kuwalinda mabinti wa taifa hili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles