28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Tundu Lissu azungumzia kurudi nyumbani, mshahara wake

Na MWANDISHI WETU    -DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), amesema Bunge limemlipa madai ya mishahara yake aliyokuwa akidai kuanzia Januari hadi Machi, mwaka huu.

Lissu ambaye yuko nchini Ubelgiji kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi Septemba 7, mwaka 2017, aliyasema hayo jana kupitia waraka mfupi aliouweka kwenye mitandao ya kijamii.

Mbali na mishahara yake, pia katika waraka huo alizungumzia afya yake huku akisema wakati mwafaka ukifika ataeleza tarehe kamili ya kurudi nchini.

“Kwanza naomba nianze kwa kuwatakia kila la kheri katika wakati huu wa wikiendi ya Pasaka.

“Pili naomba niwape mrejesho kuhusu ‘ugomvi’ wangu na Spika wa Bunge, Job Ndugai na watu wake juu ya mshahara wangu. 

“Pamoja na kwamba Spika Ndugai amesikika akisema kuwa mambo ya mshahara ni siri ya Bunge na mbunge husika na yanatakiwa kujadiliwa ‘chumbani’ na si ‘sebuleni’, nadhani ni vizuri tukafunga mjadala huu kama ulivyoanza hadharani.

“Kwa kifupi ni kwamba Spika Ndugai na watu wake wamelipa mshahara wangu wa tangu Januari hadi yaishe ni ujasiri wenu na wa watu wengine wengi, mlioamua kunichangia, si tu gharama za matibabu yangu, bali hata huo mshahara uliozuiliwa kinyume na sheria na kanuni za Bunge.

“Sikukubali kufa kimya kimya na ninyi ndugu zangu hamkukubali. Walipoona sokomoko la mshahara wangu limekuwa kubwa na sasa limebebwa na wananchi wakakubali yaishe. Nawapongezeni sana kwa ushindi huu.

“Hakuna busara yoyote ile katika kukubali kunyongwa kimya kimya na wasio na haki. Christopher Okigbo, mshairi maarufu wa Nigeria ya wakati wa Vita ya Biafra, aliandika: ‘The man died who keeps silent in the face of oppression’,” aliandika Lissu.

Kutokana na taarifa hiyo ya Lissu, MTANZANIA ilimtafuta Spika wa Bunge, Ndugai pamoja na Katibu wa Bunge Dk. Stephen Kagaigai ili kupata kauli ya Bunge kuhusu andiko la Lissu lakini simu zao ziliita muda mrefu bila kupokewa.

AFYA YAKE

Kuhusu maendeleo ya afya yake Lissu alisema; “Na kwenye hili habari ni njema sana. Aprili 2 mwaka huu nilikutana na madaktari wangu kwa ‘appointment’ ya kwanza tangu operesheni za Februari 20, mwaka huu.

“Taarifa yao ni kwamba mfupa wote wa mguu wa kulia umepona vizuri. Sehemu iliyowekewa ‘kiraka’ cha mfupa na kupigwa ‘ribiti’ ya chuma juu kidogo ya goti na sehemu ya kwenye paja iliyotakiwa kuota mfupa mpya, zote ziko vizuri.

“Sasa kazi kubwa iliyobaki ni kukunja goti na kujifunza kutembea tena. Naomba mniamini nikisema kujifunza kutembea tena, baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa kulala kitandani, ni kazi ngumu sana.

 “Nafikiri sina tofauti sana na mtoto mdogo anayejifunza kupiga hatua zake za kwanza. Lakini polepole nitafika inshaallah.”

Mbunge huyo alisema Mei 14, mwaka huu, atapimwa urefu wa miguu ili atengenezewe kiatu au soli maalumu kwa ajili ya mguu wa kulia.

“Kwa sababu ya majeraha makubwa niliyopata, mguu huo ni mfupi kwa sentimita kadhaa. Bila kiatu au soli maalumu nitakuwa ‘langara’ na madaktari wamesema hiyo sio sawa sawa. Sasa nina tarehe ambayo madaktari wangu wamesema nitakuwa ‘fiti’ kurudi nyumbani.

“Msiniambie niiseme kwa wakati huu. Tunahitaji kushauriana na wadau mbalimbali kuhusu tarehe halisi na namna bora zaidi ya kurudi kwangu nyumbani.

 “Kwa hiyo, wakati mwafaka utakapofika, hopefully (natumaini) si mbali sana, nitawaeleza tarehe kamili ya kurudi nyumbani,” alisema Lissu.

KAULI YA NDUGAI

Aprili 6, mwaka huu, akizungumza na gazeti moja la kila siku (si MTANZANIA), Spika Ndugai alisema mhimili huo wa dola umeshamlipa madai yake yote mbunge huyo, huku akisema kama ana jambo lolote ni vema kuwasiliana na mamlaka husika na si kutumia mitandao ya kijamii.

Kauli hiyo ya Ndugai ilitokana na madai ya Lissu akisema alimwandikia barua Katibu wa Bunge, Dk. Kagaigai akimtaka kumlipa mshahara na posho zake za kuanzia Januari hadi Machi vinginevyo angekwenda mahakamani.

Lissu yupo nje ya nchi tangu Septemba 7, 2017 aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana akiwa katika makazi yake Dodoma wakati akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge.

Baada ya kushambuliwa, alipelekwa Hospitali ya Dodoma kwa matibabu na baadaye katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako alikaa hadi Januari 6 mwaka 2018 alipohamishiwa Ubelgiji kwa matibabu zaidi ambayo anaendelea kuyapata hadi sasa.

Kwa siku za karibuni, Lissu alifanya ziara nchini Ujerumani, Uingereza, Marekani na kurejea Ubelgiji ambako alifanyiwa operesheni ya 23.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles