24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Tundu Lissu avuliwa ubunge rasmi

Waandishi wetu

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, ametangaza kumvua ubunge, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu huku akitoa sababu mbili zilizofanya kufikiwa uamuzi huo kuwa ni kutoonekana bungeni bila Spika kuwa na taarifa ya maandishi na kutojaza fomu ya tamko la mali na madeni.

Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni miezi sita tangu Januari ambapo Lissu kupitia mitandao ya kijamii, alisema amepata taarifa za mpango wa kumvua Ubunge.

Jana Ndugai alitangaza uamuzi wa Lissu kuvuliwa ubunge  muda mfupi baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuahirisha Mkutano wa 15 wa Bunge la Bajeti.

Lissu amevuliwa ubunge akiwa nje ya nchi tangu Septemba 7 mwaka 2017 aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu ambao hadi hawajajulikana.

Kutokana risasi alizopigwa akiwa mjini Dodoma akihudhuria vikao vya Bunge, Lissu ambae amekuwa Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki tangu mwaka 2010, amefanyiwa oparesheni 19 hadi sasa.

Wakati uamuzi huo ukitolewa jana, hivi karibuni Chadema ilitangaza mapokezi makubwa ya kumpokea Lissu Septemba ikiwa ni mipango pia ya kushiriki kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Akitoa uamuzi huo, Ndugai pamoja na mambo mengine, alisema Lissu hajaonekana bungeni kwa muda mwaka mmoja sasa.

 “ Septemba, 2017 kwa sababu ambazo zinafahamika kwa kila mtu, Mbunge wa Singida Mashariki aliondoka hapa nchini kwa ajili ya matibabu nchini Kenya.

“Kufanya hadithi iwe fupi mtakumbuka zaidi ya mwaka mmoja amekuwa akionekana kwenye vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa  akifanya mihadhara mbalimbali.

“Lakini kwa muda wote huo hajafika bungeni na hajawahi kuleta taarifa yeyote ile kwa Spika kuhusu mahali alipo  na anaendeleaje wala hajawahi kuleta taarifa kupitia kwa uongozi wake wa kambi au uongozi wa Bunge,”  Ndugai aliliambia Bunge.

Alisema Katiba ya nchi ipo wazi katika mambo ya aina hiyo  na kwamba baadhi ya wabunge  wameshapata matatizo kutokana na utoro kama huo wa Lissu.

“Wa (utoro) kushindwa hata kuwambia Spika niko mahala fulani naendelea na jambo fulani hivi hakuna chochote, yaani kama kum dis-regard Spika kama hakuna chochote,” alisema Ndugai

Alisema jambo la pili wabunge wanatakiwa kujaza taarifa zenye maelezo ya mali na madeni kama Katiba inavyotaka.

“Tunatakiwa tujaze fomu mbili na nakala inabaki kwa Spika, baada ya kuona kwenye kumbukumbu zangu hakuna fomu za Lissu, nilichukua jukumu la kupata uhakika wa jambo hili kwa Kamishna wa Tume ya Maadili na nilijibiwa kwa barua kwamba Lissu hajawasilisha na hawana taarifa zozote,” alisema .

Katika hilo Ndugai alisema kwa maana hiyo Lissu hakuwa amejaa fomu na kwamba katika mazingira hayo kifungu cha 37 kifungu kidogo cha 3 cha Sheria ya Uchaguzi kinamtaka kumtaarifu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC) cha kufanya.

“Sababu ni mbili kutotoa taarifa za mahali alipo na kutotoa tamko la mali na madeni kama ibara ya 71 ( 1g) inavyotaka,”.

“Napenda kuwafahamisha kuwa nimemwandikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwamba Jimbo la Singida Mashariki lipo wazi, alijaze kwa mujibu wa sheria zetu” alisema Ndugai  

 “Narudia kwa kumalizia maana kuna baadhi ya magazeti yataandika spika amfukuza hapana!

“Katiba yetu inasema katika mazingira yale yote mawili ubunge wake utakoma na ataacha kiti chake kwa hiyo unakwenda kinyume, hufukuzwi na yeyote ni kama ‘option’ (chaguo) uliyoichagua mwenyewe wajibu wa Spika ni kumwandia tu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi,”alisema Ndugai.

Kabla ya uamuzi alioutangaza jana Ndugai, Lissu ambaye amekuwa mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, amejikuta akiingia kwenye mgogoro na Spika Ndugai kutokana na malipo ya matibabu yake na pili kusudio lake la kutaka kumsitishia msharaha.

Kusudio la Ndugai kumfutia Lissu Mshahara, lilitokana na baadhi ya wabunge waliohoji juu ya yeye kuendelea kulipwa mshahara ilihali ahudhurii bungeni badala yake anaitukana Serikali nje ya nchi.

Hata hivyo hoja hiyo ya iliondoka Aprili, baada ya Lissu mwenyewe kutamka kuwa, “Spika Ndugai na watu wake wamelipa mshahara wangu wa tangu Januari hadi Machi waliokuwa wameuzuia kiharamia tu, kwa maoni yangu kilichowafanya wakubali yaishe ni ujasiri wenu, na wa watu wengine wengi, mlioamua kunichangia.”

SELASINI :NI UONEVU

Akizungumzia uamuzi wa kumvua ubunge Lissu, Mnadhimu wa Kambi ya  Upinzani Bungeni, Joseph Selasini (Chadema) alisema ni  uonevu na kama Bunge litatumika kuonea watu litakuwa la jabu na ambalo kila mmoja atalishangaa.

Mbunge huyo wa Rombo (Chadema) Selasini ambaye alikuwa akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge, jana jioni.

Kwa hiyo nadhani zaidi chama kitasema au yeye mwenyewe atasema…ni uamuzi ambao ulitegemewa tangu mwanzo wa mwaka huu, kwenye Bunge la Februari nilisikia wabunge wa CCM wakihoji ni kwanini Lissu anapata mshahara wakati hayupo bungeni, sasa hakuna Mtanzania yeyote ama Mbunge ambaye hajui kwamba alikuwa kwenye matibabu Ubelgiji,”.

Alisema mwenye mamlaka ya kusema kwamba Lissu amepona ni Daktari wake na sio mtu mwingine yoyete.

Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana alipokuwa akitokea bungeni, mchana wa Septemba 7, 2017 alipokuwa amewasili nyumbani kwake.

Baada ya kupata huduma ya kwanza katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, alihamishiwa katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwa ndege ya kukodi Septemba 8, 2017.

Kufuatia tukio lililowashtua wengi, Spika wa Bunge, Job Ndugai alitoa taarifa kwa ufupi kuhusu tukio hilo kabla ya kuendelea kwa mkutano wa nane wa Bunge mjini Dodoma.
Akimnukuu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Spika Ndugai alisema kuwa, katika tukio la kushambuliwa kwa Mbunge Tundu Lissu, kati ya risasi 28 hadi 32 zilifyatuliwa katika gari lake.

Januari 6, 2018 aliondolewa katika Hospitali ya Nairobi alikokuwa akipatiwa matibabu maalumu na kupelekwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi.

Lissu alipelekwa Ubelgiji kwa Ndege ya Shirika la Kenya akiambatana na mke wake, Alicia ambapo alisindikizwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta na watoto wake pacha, Augustino na Edward, ndugu zake, viongozi na wanachama wa Chadema.

Machi 19 mwaka huu, aliwaelekeza mawakili wake kuanza mchakato wa kufungua mashauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania, ili kudai uongozi wa Bunge urejeshe stahili zake zote zilizozuiliwa, nakulizuia lisiziingilie au kuziathiri tena kwa namna nyingine yoyote.

Lissu alisema uamuzi wa kumfutia mshahara na posho za kibunge ambazo kila Mbunge hulipwa, awe anaumwa au mzima, awe amehudhuria vikao vya Bunge au hajahudhuria, ni uthibitisho mwingine wa ukiukaji wa Katiba, Sheria na taratibu.

Katika waraka wake alioutoa kwa njia ya picha ya video akiwa nchini Ubelgiji alisema”Uamuzi wa Bunge kunifutia mshahara na posho zangu ulifanyika kabla hata ya Spika Ndugai kuombwa, na kutoa,mwongozo huo. Ndio kusema kwamba Bunge la Spika Ndugai na Katibu wa Bunge Kagaigai limezuia mshahara na posho za kibunge tangu mwezi Januari,” alieleza Lissu.

Hatua hii ilikuja baada ya mwezi Februari mwaka huu, Mbunge wa Geita vijijini (CCM) Joseph Kisheku maarufu kama Msukuma kutoa hoja bungeni kuhoji uhalali wa Tundu Lissu kuendelea kupata mshahara huku akiwa hahudhurii vikao kwa sababu ambazo hazijulikani.

Hoja hiyo ya Musukuma ilijibiwa na Lissu mwenyewe aliyeeleza kwa ufupi kuwa anayeweza kuthibitisha kama bado ni mgonjwa na anasthahili kuendelea kupata matibabu nchini Ubelgiji ni daktari wake.

Kwamba hata ziara aliyoifanya na kuzungumza na  vyombo vya habari vya Kimataifa ilikuwa ni sehemu ya matibabu yake.

Habari hii imeandaliwa na ELIZABETH HOMBO Na ANDREW MSECHU (DAR)  Na RAMADHAN HASSAN (DODOMA)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles